Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 32:19-35 - Compare All Versions

Kutoka 32:19-35 BHN (Biblia Habari Njema)

Mara tu walipoikaribia kambi walipomwona yule ndama na watu wakicheza; hapo hasira ya Mose ikawaka kama moto, akavitupa chini vile vibao kutoka mikononi mwake na kuvivunja pale chini ya mlima. Basi, akamchukua yule ndama akamchoma moto, akamsaga mpaka akawa unga, akaukoroga unga huo katika maji na kuwalazimisha Waisraeli wanywe. Mose akamwuliza Aroni, “Walikufanya nini watu hawa hata ukawaingiza katika dhambi kubwa hivyo?” Aroni akamjibu, “Nakuomba ee bwana wangu hasira yako isiniwakie mimi mtumishi wako. Unawafahamu jinsi watu hawa walivyo tayari kutenda maovu. Walikuja wakaniambia, ‘Tufanyie miungu ambayo itatuongoza kwani huyo Mose aliyetutoa nchini Misri hatujui lililompata’. Nami nikawaambia, kila mmoja aliye na vito vya dhahabu na avilete. Basi, wakaniletea, nami nikaviyeyusha motoni na huyu ndama akatokea.” Basi, Mose alipoona kuwa watu wameasi na kufanya wapendavyo (kwa kuwa Aroni aliwafanya waasi na kufanya wapendavyo, na kujiletea aibu mbele ya adui zao), Mose akasimama mbele ya lango la kambi na kuuliza, “Ni nani aliye upande wa Mwenyezi-Mungu? Na aje kwangu.” Wana wote wa Lawi wakakusanyika pamoja mbele yake. Akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: ‘Kila mtu na ajifunge upanga wake kiunoni, azunguke kila mahali kambini, kutoka lango moja hadi lingine, na kila mmoja amuue ndugu yake, rafiki yake na jirani yake.’” Wana wa Lawi wakafanya kama Mose alivyowaagiza. Siku hiyo waliuawa watu wapatao 3,000. Mose akasema, “Leo mmejiweka wakfu nyinyi wenyewe kumhudumia Mwenyezi-Mungu, kwa vile hamkusita hata kuwaua watoto wenu au ndugu zenu. Mungu awajalie baraka leo hii.” Kesho yake Mose akawaambia watu, “Mmetenda dhambi kubwa! Sasa nitamwendea Mwenyezi-Mungu juu mlimani; labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.” Hivyo Mose akarudi kwa Mwenyezi-Mungu, akamwambia, “Nasikitika! Watu hawa wametenda dhambi kubwa; wamejifanyia wenyewe miungu ya dhahabu. Lakini sasa, nakuomba uwasamehe dhambi yao. Ikiwa hutawasamehe, nakusihi unifute mimi katika kitabu chako ulichowaandika watu wako.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nitamfuta katika kitabu changu mtu yeyote aliyenitendea dhambi. Lakini sasa nenda ukawaongoze watu mpaka mahali nilipokuambia. Tazama, malaika wangu atakutangulia. Hata hivyo, siku nitakapowajia, nitawaadhibu kwa sababu ya dhambi yao.” Mwenyezi-Mungu akawapelekea watu ugonjwa wa tauni, kwa kuwa walimwomba Aroni awafanyie yule ndama wa dhahabu.

Shirikisha
Kutoka 32 BHN

Kutoka 32:19-35 SRUV (Swahili Revised Union Version)

Hata alipokaribia kambini akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima. Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli. Musa akamwambia Haruni Watu hawa wamekufanya nini hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao? Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake, wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya. Maana waliniambia, Katufanyie miungu, itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata. Nikawaambia, Mtu yeyote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu. Basi Musa alipoona ya kuwa watu hawa wameasi, maana Haruni amewaacha waasi, na kuwa dhihaka kati ya adui zao, ndipo Musa akasimama katika mlango wa kambi, akasema, Mtu yeyote aliye upande wa BWANA, na aje kwangu. Wana wa Lawi wote wakamkusanyikia Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila mtu na ajifunge upanga wake pajani mwake, akapite huku na huko toka mlango hata mlango kati kambi, mkamchinje kila mtu ndugu yake, na kila mtu mwenziwe na kila mtu jirani yake. Na hao wana wa Lawi wakafanya kama vile alivyosema Musa, wakaanguka siku ile kama watu elfu tatu. Musa akasema, Jiwekeni wakfu kwa BWANA leo, kila mtu juu ya mwanawe na juu ya ndugu yake; ili awape baraka leo. Hata asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa BWANA, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu. Musa akarejea kwa BWANA akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu. Lakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika. BWANA akamwambia Musa, Mtu yeyote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekwambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao. BWANA akawapiga hao watu, kwa tauni kwa kuifanya ile ndama, ambayo Haruni aliifanya.

Shirikisha
Kutoka 32 SRUV

Kutoka 32:19-35 SUV (Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia)

Hata alipoyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima. Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli. Musa akamwambia Haruni Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao? Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake, wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya. Maana waliniambia, Katufanyie miungu, itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata. Nikawaambia, Mtu ye yote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu. Basi Musa alipoona ya kuwa watu hawa wameasi, maana Haruni amewaacha waasi, ili wawe dhihaka kati ya adui zao, ndipo Musa akasimama katika mlango wa marago, akasema, Mtu awaye yote aliye upande wa BWANA, na aje kwangu. Wana wa Lawi wote wakamkusanyikia Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila mtu na ajifunge upanga wake pajani mwake, akapite huko na huko toka mlango hata mlango kati ya marago, mkamchinje kila mtu ndugu yake, na kila mtu mwenziwe na kila mtu jirani yake. Na hao wana wa Lawi wakafanya kama vile alivyosema Musa, wakaanguka siku ile kama watu elfu tatu. Musa akasema, Jiwekeni wakfu kwa BWANA leo, naam, kila mtu juu ya mwanawe na juu ya ndugu yake; ili awape baraka leo. Hata asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa BWANA, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu. Musa akarejea kwa BWANA akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu. Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika. BWANA akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekwambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao. BWANA akawapiga hao watu, kwa walivyoifanya ile ndama, ambayo Haruni aliifanya.

Shirikisha
Kutoka 32 SUV

Kutoka 32:19-35 NEN (Neno)

Musa alipoikaribia kambi na kuona yule ndama na ile michezo, hasira yake ikawaka, akatupa vile vibao vilivyokuwa mikononi mwake, akavipasua vipande vipande pale chini ya mlima. Kisha akamchukua yule ndama waliokuwa wamemtengeneza na kumchoma kwenye moto, kisha akamsaga kuwa unga, akanyunyiza kwenye maji na kuwafanya Waisraeli wanywe. Musa akamwambia Haruni, “Watu hawa walikufanyia nini, hata ukawaongoza kufanya dhambi kubwa hivyo?” Haruni akamwambia, “Usikasirike bwana wangu. Unajua jinsi watu hawa walivyo tayari kwa maovu. Waliniambia, ‘Tufanyie miungu itakayotuongoza. Kwa kuwa huyu jamaa yetu Musa aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui yaliyompata.’ Kwa hiyo nikawaambia, ‘Yeyote aliye na kito chochote cha dhahabu avue.’ Kisha wakanipa hiyo dhahabu, nami nikaitupa motoni, akatokea huyu ndama!” Musa akaona kuwa watu wameasi, kwa kuwa Haruni alikuwa amewaacha waasi, na hivyo kuwa kichekesho kwa adui zao. Kwa hiyo Musa akasimama kwenye ingilio la kambi, akasema, “Yeyote aliye upande wa BWANA, aje upande wangu.” Walawi wote wakamjia. Ndipo alipowaambia, “Hili ndilo BWANA, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kila mmoja wenu ajifunge upanga wake kiunoni aende huku na huko kambi yote mwisho hadi mwisho mwingine, kila mmoja amuue ndugu yake, na rafiki yake na jirani yake.’ ” Walawi wakafanya kama Musa alivyoamuru, siku ile wakafa watu wapatao elfu tatu. Kisha Musa akasema, “Leo mmewekwa wakfu kwa BWANA, kwa kuwa mlikuwa kinyume na wana wenu wenyewe na ndugu zenu, naye Mungu amewabariki leo.” Siku iliyofuata Musa akawaambia watu, “Mmefanya dhambi kubwa. Lakini sasa nitapanda juu kwa BWANA, labda nitaweza kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.” Hivyo Musa akarudi kwa BWANA na kumwambia, “Lo! Hawa watu wamefanya dhambi kubwa namna gani! Wamejitengenezea miungu ya dhahabu. Lakini sasa nakusihi, wasamehe dhambi yao; lakini kama sivyo, basi nifute kutoka kitabu ulichoandika.” BWANA akamjibu Musa, “Yeyote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta kutoka kitabu changu. Sasa nenda, uongoze hao watu hadi mahali nilipokuambia, naye malaika wangu atakutangulia. Pamoja na hayo, wakati utakapofika wa mimi kuwaadhibu, nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi yao.” Ndipo BWANA akawapiga watu kwa ugonjwa wa tauni kwa sababu ya yale waliyoyafanya na ndama yule ambaye alitengenezwa na Haruni.

Shirikisha
Kutoka 32 NEN