Kutoka 3:1-7
Kutoka 3:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, Mose alikuwa anachunga kundi la kondoo la baba mkwe wake, Yethro, kuhani wa Midiani. Mose alilipeleka kundi hilo upande wa magharibi wa jangwa, akaufikia mlima Horebu, mlima wa Mungu. Basi, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea katika mwali wa moto katikati ya kichaka. Mose akaangalia, akashangaa kuona kichaka kinawaka moto na wala hakiungui. Basi, akajisemea, “Hiki ni kioja! Kichaka kuwaka moto na kisiungue? Hebu nitazame vizuri.” Mwenyezi-Mungu alipoona kwamba Mose amegeuka kukiangalia kichaka, akamwita pale kichakani, “Mose! Mose!” Mose akaitika, “Naam! Nasikiliza!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Usije karibu! Vua viatu vyako kwa sababu mahali unaposimama ni mahali patakatifu.” Kisha Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako; Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo.” Mose akaufunika uso wake kwa kuwa aliogopa kumwangalia Mungu. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nimeyaona mateso ya watu wangu walioko nchini Misri na nimekisikia kilio chao kinachosababishwa na wanyapara wao. Najua mateso yao
Kutoka 3:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kichaka; akatazama, na kumbe! Kile kichaka kiliwaka moto, nacho kichaka hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa niende nione kioja hiki, kwa nini kichaka hiki hakiteketei. BWANA alipoona ya kuwa ameenda ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kichaka, akasema, Musa! Musa! Akaitika, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni mahali patakatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akafunika uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao
Kutoka 3:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao
Kutoka 3:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi Musa alikuwa anachunga mifugo ya Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani. Musa akapeleka mifugo mbali nyuma ya jangwa, naye akafika Horebu, mlima wa Mungu. Huko malaika wa BWANA akamtokea Musa katika mwali wa moto kutoka kichakani. Musa akaona kwamba ingawa kile kichaka kilikuwa kinawaka moto, kilikuwa hakiteketei. Ndipo Musa akawaza, “Nitageuka sasa nione kitu hiki cha ajabu, nami nione ni kwa nini kichaka hiki hakiteketei.” BWANA alipoona kuwa amegeuka ili aone, Mungu akamwita kutoka ndani ya kile kichaka, “Musa! Musa!” Naye Musa akajibu, “Mimi hapa.” Mungu akamwambia, “Usikaribie zaidi. Vua viatu vyako, kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu.” Kisha akamwambia, “Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.” Musa aliposikia hayo, akafunika uso wake kwa sababu aliogopa kumtazama Mungu. BWANA akamwambia, “Hakika nimeona mateso ya watu wangu katika Misri. Nimesikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao, nami nimeguswa na mateso yao.