Kutoka 29:37-45
Kutoka 29:37-45 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa siku saba utaifanyia madhabahu upatanisho na kuiweka wakfu. Baada ya hayo, madhabahu itakuwa takatifu kabisa na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu. “Kila siku, wakati wote ujao, utatolea sadaka juu ya madhabahu: Wanakondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja. Mwanakondoo mmoja utamtoa sadaka asubuhi na mwingine jioni. Pamoja na mwanakondoo wa kwanza, utatoa kilo moja ya unga laini uliochanganywa na lita moja ya mafuta safi, na lita moja ya divai kama sadaka ya kinywaji. Hali kadhalika na yule mwanakondoo mwingine wa jioni utamtolea tambiko pamoja na sadaka ya nafaka na ya kinywaji kama ulivyofanya asubuhi; harufu ya tambiko hiyo inayotolewa kwa moto itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. Sadaka hii ya kuteketezwa itatolewa daima, kizazi hata kizazi, mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu, mbele ya mlango wa hema la mkutano ambapo mimi nitakutana nanyi na kuongea nanyi. Hapo ndipo nitakapokutana na Waisraeli na utukufu wangu utapafanya pawe patakatifu. Hema la mkutano na madhabahu nitavifanya vitakatifu; vilevile Aroni na wanawe nitawaweka wakfu ili wanitumikie kama makuhani. Nitaishi kati ya Waisraeli, nami nitakuwa Mungu wao.
Kutoka 29:37-45 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Utafanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu muda wa siku saba, na kuitakasa; ndipo madhabahu itakapokuwa takatifu sana; kila kitu kiigusacho madhabahu kitakuwa kitakatifu. Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja kila siku. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni; tena, pamoja na mwana-kondoo mmoja utatoa vibaba vitatu vya unga mzuri uliochanganyika na mafuta yaliyopondwa, kiasi cha kibaba na robo kibaba; na divai kiasi cha kibaba na robo kibaba, iwe sadaka ya kinywaji. Na huyo mwana-kondoo wa pili utamchinja wakati wa jioni, na utamtoa dhabihu pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji kama asubuhi, ili itoe harufu nzuri, iwe dhabihu ya kusogeswa kwa Bwana kwa njia ya moto. Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya BWANA; hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo. Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo, na hiyo Hema itafanywa takatifu na utukufu wangu. Nami nitaitakasa hiyo hema ya kukutania, na hiyo madhabahu; pia Haruni na wanawe nitawatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Na mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao.
Kutoka 29:37-45 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Utafanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu muda wa siku saba, na kuitakasa; ndipo madhabahu itakapokuwa takatifu sana; kila kitu kiigusacho madhabahu kitakuwa kitakatifu. Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku daima. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni; tena, pamoja na mwana-kondoo mmoja utatoa vibaba vitatu vya unga mzuri uliochanganyika na mafuta yenye kupondwa, kiasi cha kibaba na robo kibaba; na divai kiasi cha kibaba na robo kibaba, iwe sadaka ya kinywaji. Na huyo mwana-kondoo wa pili utamchinja wakati wa jioni, nawe utamfanyia vivyo kama ile sadaka ya unga ya asubuhi, na kama ile sadaka yake ya kinywaji, iwe harufu nzuri, ni dhabihu ya kusongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya BWANA; hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo. Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo, na hiyo Hema itafanywa takatifu na utukufu wangu. Nami nitaitakasa hiyo hema ya kukutania, na hiyo madhabahu; pia Haruni na wanawe nitawatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Na mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao.
Kutoka 29:37-45 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa muda wa siku saba fanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu na kuiweka wakfu. Ndipo madhabahu itakuwa takatifu sana na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu. “Kwa kawaida hiki ndicho utakachotoa juu ya madhabahu kila siku: wana-kondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja. Utamtoa mmoja asubuhi na huyo mwingine jioni. Pamoja na mwana-kondoo wa kwanza utatoa efa moja ya unga wa ngano laini uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta yaliyokamuliwa, pamoja na robo ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji. Huyo mwana-kondoo mwingine mtoe dhabihu wakati wa machweo pamoja na sadaka za unga na za kinywaji kama vile ulivyofanya asubuhi, kuwa harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto. “Kwa vizazi vijavyo itakuwa kawaida kutoa sadaka hii ya kuteketezwa kila mara kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za BWANA. Hapo ndipo nitakapokutana na ninyi na kusema nanyi, Huko ndipo nitakapokutana na Waisraeli, nalo Hema la Kukutania litatakaswa na utukufu wangu. “Kwa hiyo nitaliweka wakfu Hema la Kukutania pamoja na madhabahu, nami nitamweka wakfu Haruni na wanawe ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani. Ndipo nitakapofanya makao miongoni mwa Waisraeli na kuwa Mungu wao.