Kutoka 26:1-37
Kutoka 26:1-37 Biblia Habari Njema (BHN)
“Zaidi ya hayo yote, utatengeneza hema takatifu kwa mapazia kumi ya kitani safi iliyosokotwa, na kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu. Mapazia hayo utayapamba kwa michoro ya viumbe wenye mabawa waliotariziwa. Kila pazia litakuwa na urefu wa mita 12 na upana wa mita 2. Mapazia hayo yawe ya kipimo kimoja. Utaunganisha mapazia matano yawe kipande kimoja na mapazia mengine matano yawe kipande cha pili. Utashonea vitanzi vya buluu upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, hali kadhalika utashonea vitanzi mwishoni mwa pindo la nje la kipande kingine cha pazia. Utatia vitanzi hamsini katika pazia moja na vitanzi vingine hamsini kwenye utepe wa pazia la pili; vitanzi vyote vielekeane. Kisha utatengeneza kulabu hamsini za dhahabu ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia, hivyo hema litakuwa kitu kimoja. “Pia utatengeneza kifuniko cha hema kwa mapazia kumi na moja ya manyoya ya mbuzi. Kila pazia litakuwa na urefu wa mita 13, na upana wa mita 2. Mapazia yote hayo 11 yatakuwa na kipimo kilekile. Utaunga mapazia matano pamoja, na mapazia sita pamoja. Pazia la sita utalikunja mara mbili mbele ya hema. Kisha utafanya vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha pili. Utatengeneza kulabu hamsini za shaba na kuziingiza katika vile vitanzi hamsini ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia na hivyo kufanya pazia moja la hema. Ile nusu ya pazia iliyobaki utaitundika upande wa nyuma wa hema. Nusu mita ya urefu wa mapazia iliyo ya ziada utaikunja ininginie pande zote mbavuni mwa hema ili kulifunika. Utatengeneza pia kifuniko kingine cha hema kilichofanywa kwa ngozi laini ya kondoo dume na ngozi laini ya mbuzi. “Utatengeneza mbao za mjohoro za kusimama wima kwa ajili ya hema. Kila ubao utakuwa na urefu wa mita 4, na upana wa sentimita 66. Kila ubao utakuwa na ndimi mbili za kuunganishia. Utazifanyia mbao zote ndimi mbili. Basi, utatengeneza hizo mbao za hema hivi: Mbao ishirini kwa ajili ya upande wa kusini, na vikalio arubaini vya fedha chini ya hizo mbao ishirini, vikalio viwili chini kwa kila ubao ili kushikilia zile ndimi zake mbili na vikalio viwili viwe chini ya ubao mwingine ili kushikilia zile ndimi zake mbili. Upande wa kaskazini wa hema, utatengeneza mbao ishirini, na vikalio vyake arubaini vya fedha, vikalio viwili chini ya kila ubao. Kwa upande wa nyuma, ulio magharibi ya hema, utatengeneza mbao sita. Utatengeneza pia mbao mbili kwa ajili ya pembe za hema upande wake wa nyuma. Mbao hizo za pembeni ziachane chini lakini zishikamanishwe kwa juu kwenye pete ya kwanza. Mbao zote za pembeni zifanywe vivyo hivyo ili zifanye pembe mbili. Hivyo kutakuwa na mbao nane pamoja na vikalio vyake kumi na sita vya fedha: Vikalio viwili chini ya kila mbao na vikalio viwili chini ya ubao mwingine. “Utatengeneza pau za mjohoro; pau tano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa hema, na pau tano kwa ajili ya upande wa pili wa hema, na pau tano kwa ajili ya mbao za upande wa nyuma wa hema, ulio magharibi. Upau wa katikati uliofika nusu ya jengo la hema utapenya katikati toka mwisho huu hadi mwisho mwingine wa hema. Mbao zote utazipaka dhahabu na kuzifanyia pete za dhahabu zitakazoshikilia hizo pau, ambazo pia utazipaka dhahabu. Hivyo utalitengeneza hema hilo kulingana na mfano niliokuonesha mlimani. “Utatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Pazia hilo utalitarizi kwa ustadi kwa viumbe wenye mabawa. Utalitundika pazia kwenye nguzo nne za mjohoro zilizopakwa dhahabu, zenye kulabu za dhahabu na vikalio vinne vya fedha. Utalitundika pazia hilo kwenye vifungo, kisha ulilete lile sanduku la ushuhuda humo ndani kukiwa na vibao viwili vya mawe, nyuma ya pazia hilo. Pazia hilo litatenga mahali patakatifu na mahali patakatifu sana. Ndani ya mahali patakatifu utakiweka kile kiti cha rehema juu ya sanduku la maamuzi. Ile meza ya mjohoro utaiweka upande wa nje wa pazia hilo, na kile kinara cha taa utakiweka upande wa kusini wa hema, mkabala wa meza. Meza hiyo itakuwa upande wa kaskazini. “Kwa ajili ya mlango wa hema utatengeneza pazia zito kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kutariziwa vizuri. Vilevile utatengeneza nguzo tano za mjohoro na kuzipaka dhahabu. Nguzo hizo zitakuwa na kulabu za dhahabu, na kila moja itakuwa na tako la shaba.
Kutoka 26:1-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha fanya hiyo maskani iwe na mapazia kumi; ifanye ya nguo ya kitani nzuri ya kusokota, pamoja na nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, pamoja na makerubi; kazi ya fundi stadi. Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa ishirini na nane, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne; mapazia yote yatakuwa ya kipimo kimoja. Mapazia matano yataungwa pamoja, hili na hili; na mapazia matano mengine yataungwa pamoja, hili na hili. Kisha utafanya tanzi za rangi ya samawati upande wa mwisho wa pazia moja katika ule upindo wa fungu lake, vivyo hivyo utafanya upande wa mwisho wa ile pazia iliyo, katika fungu la pili. Fanya matanzi hamsini katika pazia moja, na matanzi hamsini katika upande wa mwisho wa ile pazia iliyo katika kuungana kwa pili; hizo tanzi zitaelekeana. Kisha ufanye vifungo hamsini vya dhahabu, na kuunganisha hayo mapazia pamoja kwa vile vifungo; na hiyo maskani itakuwa ni moja. Nawe fanya mapazia ya singa za mbuzi yawe hema juu ya maskani; fanya mapazia kumi na moja. Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa thelathini, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne; hayo mapazia kumi na moja yatakuwa ya kipimo kimoja. Kisha utaunganisha mapazia matano mbali, na mapazia sita mbali, na lile pazia la sita utalikunja hapo upande wa mbele wa ile hema. Fanya tanzi hamsini upande wa mwisho wa pazia lile lililo la mwisho katika hayo yaliyounganywa pamoja, na tanzi hamsini upande wa mwisho wa lile pazia lililo nje katika hayo ya pili yaliyounganywa pamoja. Tena ufanye vifungo hamsini vya shaba, na kuvitia vile vifungo katika zile tanzi, na kuiunganya ile hema pamoja, ili iwe hema moja. Na kipande kile kilichosalia, kile kiangukacho, cha yale mapazia ya hema, ile nusu ya pazia iliyosalia, itaanguka huko upande wa nyuma wa maskani. Na hiyo dhiraa moja upande mmoja, na ile dhiraa moja upande wa pili, ya urefu wa mapazia ya hema uliosalia, zitaanguka katika ubavu wa maskani upande huu na upande huu, ili kuifunika. Nawe fanya kifuniko cha ile hema, cha ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo. Nawe fanya hizo mbao za maskani za mti wa mjohoro, zenye kusimama. Kila ubao utakuwa na urefu wa dhiraa kumi, na upana wake kila ubao utakuwa dhiraa moja na nusu. Kila ubao utakuwa na ndimi mbili, zenye kuunganishwa huu na huu; ndivyo utakavyozifanya mbao zote za maskani. Kisha ufanye zile mbao za maskani, mbao ishirini kwa upande wa kusini kuelekea kusini. Nawe ufanye vitako arubaini vya fedha chini ya zile mbao ishirini, vitako viwili chini ya ubao mmoja, kupokea zile ndimi zake mbili, na vitako viwili chini ya ubao mwingine kupokea zile ndimi zake mbili; na upande wa pili wa maskani, upande wa kaskazini, mbao ishirini; na vitako vyake vya fedha arubaini; vitako viwili chini ya ubao mmoja, na vitako viwili chini ya ubao mwingine. Kisha ufanye mbao sita kwa ajili ya upande wa nyuma wa maskani kuelekea magharibi. Tena ufanye mbao mbili kwa ajili ya hizo pembe za maskani zilizo upande wa nyuma. Upande wa chini zitakuwa ni mbili mbili; vivyo hivyo zitaunganishwa pamoja mbao pacha hata ncha ya juu katika pete ya kwanza; zote mbili ndivyo zitakavyokuwa; zitakuwa kwa ajili ya hizo pembe mbili. Mbao zitakuwa ni nane, na vitako vyake vya fedha, vitako kumi na sita; vitako viwili chini ya ubao mmoja, na vitako viwili chini ya ubao wa pili. Nawe fanya mataruma ya mti wa mshita; mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa maskani, na mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande wa pili wa maskani, na mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande wa maskani ulio nyuma kuelekea magharibi. Na hilo taruma la katikati, lililo katikati ya zile mbao litapenya toka mwisho huu hata mwisho huu. Na hizo mbao utazifunika dhahabu, na pete zake za kutilia yale mataruma utazifanya za dhahabu; na hayo mataruma utayafunika dhahabu. Nawe utaisimamisha hiyo maskani sawasawa na mfano wake uliooneshwa mlimani. Nawe fanya pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na nguo za kitani nzuri zenye kusokotwa, litafumwa na kutiwa makerubi, kazi ya fundi stadi; kisha litungike katika nguzo nne za mti wa mshita zilizofunikwa dhahabu, vifungo vyake vitakuwa vya dhahabu, katika vitako vya fedha vinne. Nawe tungika lile pazia chini ya vile vifungo, nawe lete lile sanduku la ushuhuda na kulitia humo nyuma ya pazia; na lile pazia litawagawanyia kati ya patakatifu, na mahali patakatifu sana. Nawe utaweka kiti cha rehema juu ya lile sanduku la ushuhuda ndani ya mahali pale patakatifu sana. Na ile meza utaiweka nje ya pazia, na kinara cha taa kuikabili ile meza upande wa maskani wa kuelekea kusini; na ile meza utaiweka upande wa kaskazini. Kisha utafanya kisitiri kwa mlango wa Hema, cha nyuzi za rangi ya buluu, zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa, kazi ya mshonaji wa taraza. Nawe fanya nguzo tano za mti wa mshita kwa kile kisitiri, na kuzifunika dhahabu; kulabu zake zitakuwa za dhahabu; nawe utasubu vitako vya shaba vitano kwa ajili yake.
Kutoka 26:1-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha fanya hiyo maskani iwe na mapazia kumi; ifanye ya nguo ya kitani nzuri ya kusokota, pamoja na nyuzi za rangi ya samawi, na ya zambarau, na nyekundu, pamoja na makerubi; kazi ya fundi stadi. Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa ishirini na nane, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne; mapazia yote yatakuwa ya kipimo kimoja. Mapazia matano yataungwa pamoja, hili na hili; na mapazia matano mengine yataungwa pamoja, hili na hili. Kisha utafanya tanzi za rangi ya samawi upande wa mwisho wa pazia moja katika ule upindo wa fungu lake, vivyo utafanya upande wa mwisho wa ile pazia iliyo, katika fungu la pili. Fanya matanzi hamsini katika pazia moja, na matanzi hamsini katika upande wa mwisho wa ile pazia iliyo katika kuungana kwa pili; hizo tanzi zitaelekeana. Kisha ufanye vifungo hamsini vya dhahabu, na kuunganya hayo mapazia pamoja kwa vile vifungo; na hiyo maskani itakuwa ni moja. Nawe fanya mapazia ya singa za mbuzi yawe hema juu ya maskani; fanya mapazia kumi na moja. Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa thelathini, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne; hayo mapazia kumi na moja yatakuwa ya kipimo kimoja. Kisha utaunganya mapazia matano mbali, na mapazia sita mbali, na lile pazia la sita utalipeta hapo upande wa mbele wa ile hema. Fanya tanzi hamsini upande wa mwisho wa pazia lile lililo la mwisho katika hayo yaliyounganywa pamoja, na tanzi hamsini upande wa mwisho wa lile pazia lililo nje katika hayo ya pili yaliyounganywa pamoja. Tena ufanye vifungo hamsini vya shaba, na kuvitia vile vifungo katika zile tanzi, na kuiunganya ile hema pamoja, ili iwe hema moja. Na kipande kile kilichosalia, kile kiangukacho, cha yale mapazia ya hema, ile nusu ya pazia iliyosalia, itaanguka huko upande wa nyuma wa maskani. Na hiyo dhiraa moja upande mmoja, na ile dhiraa moja upande wa pili, ya urefu wa mapazia ya hema uliosalia, zitaanguka katika ubavu wa maskani upande huu na upande huu, ili kuifunika. Nawe fanya kifuniko cha ile hema, cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo. Nawe fanya hizo mbao za maskani za mti wa mshita, zenye kusimama. Kila ubao utakuwa na urefu wa dhiraa kumi, na upana wake kila ubao utakuwa dhiraa moja na nusu. Kila ubao utakuwa na ndimi mbili, zenye kuunganywa huu na huu; ndivyo utakavyozifanya mbao zote za maskani. Kisha ufanye zile mbao za maskani, mbao ishirini kwa upande wa kusini kuelekea kusini. Nawe ufanye matako arobaini ya fedha chini ya zile mbao ishirini, matako mawili chini ya ubao mmoja, kupokea zile ndimi zake mbili, na matako mawili chini ya ubao mwingine kupokea zile ndimi zake mbili; na upande wa pili wa maskani, upande wa kaskazini, mbao ishirini; na matako yake ya fedha arobaini; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao mwingine. Kisha ufanye mbao sita kwa ajili ya upande wa nyuma wa maskani kuelekea magharibi. Tena ufanye mbao mbili kwa ajili ya hizo pembe za maskani zilizo upande wa nyuma. Upande wa chini zitakuwa ni mbili mbili; vivyo zitaungwa pamoja mbao pacha hata ncha ya juu katika pete ya kwanza; zote mbili ndivyo zitakavyokuwa; zitakuwa kwa ajili ya hizo pembe mbili. Mbao zitakuwa ni nane, na matako yake ya fedha, matako kumi na sita; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao wa pili. Nawe fanya mataruma ya mti wa mshita; mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa maskani, na mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande wa pili wa maskani, na mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande wa maskani ulio nyuma kuelekea magharibi. Na hilo taruma la katikati, lililo katikati ya zile mbao litapenya toka mwisho huu hata mwisho huu. Na hizo mbao utazifunika dhahabu, na pete zake za kutilia yale mataruma utazifanya za dhahabu; na hayo mataruma utayafunika dhahabu. Nawe utaisimamisha hiyo maskani sawasawa na mfano wake ulioonyeshwa mlimani. Nawe fanya pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na nguo za kitani nzuri zenye kusokotwa, litafumwa na kutiwa makerubi, kazi ya fundi stadi; kisha litungike katika nguzo nne za mti wa mshita zilizofunikwa dhahabu, vifungo vyake vitakuwa vya dhahabu, katika matako ya fedha manne. Nawe tungika lile pazia chini ya vile vifungo, nawe lete lile sanduku la ushuhuda na kulitia humo nyuma ya pazia; na lile pazia litawagawanyia kati ya patakatifu, na mahali patakatifu sana. Nawe utaweka kiti cha rehema juu ya lile sanduku la ushuhuda ndani ya mahali pale patakatifu sana. Na ile meza utaiweka nje ya pazia, na kinara cha taa kuikabili ile meza upande wa maskani wa kuelekea kusini; na ile meza utaiweka upande wa kaskazini. Kisha utafanya kisitiri kwa mlango wa Hema, cha nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa, kazi ya mshona taraza. Nawe fanya nguzo tano za mti wa mshita kwa kile kisitiri, na kuzifunika dhahabu; kulabu zake zitakuwa za dhahabu; nawe utasubu matako ya shaba matano kwa ajili yake.
Kutoka 26:1-37 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Tengeneza maskani ya Mungu kwa mapazia kumi ya kitani iliyosokotwa vizuri na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, naye fundi stadi atatarizi makerubi kwenye mapazia hayo. Mapazia yote yatatoshana kwa ukubwa: kila moja litakuwa na urefu wa dhiraa ishirini na nane, na upana wa dhiraa nne. Unganisha mapazia matano pamoja; fanya vivyo hivyo kwa hayo mengine matano. Tengeneza vitanzi vya kitambaa cha buluu kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu la kwanza, na ufanye vivyo hivyo na pazia la fungu la mwisho. Fanya vitanzi hamsini katika pazia mmoja, na vitanzi vingine hamsini kwenye pazia la mwisho la fungu hilo lingine, navyo vitanzi vyote vielekeane. Kisha tengeneza vifungo hamsini vya dhahabu ili vitumike kufunga na kuunganisha mapazia pamoja kufanya maskani ya Mungu iwe kitu kimoja. “Tengeneza mapazia kumi na moja ya singa za mbuzi kwa ajili ya kufunika Maskani. Mapazia hayo kumi na moja yatakuwa na kipimo sawa, yaani urefu wa dhiraa thelathini, na upana wa dhiraa nne. Unganisha hayo mapazia matano yawe fungu moja, na hayo mengine sita yawe fungu lingine. Kunja hilo pazia la sita mara mbili mbele ya Maskani. Tengeneza vitanzi hamsini kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu moja, na vivyo hivyo kwenye upindo wa pazia la mwisho la fungu hilo lingine. Kisha tengeneza vifungo hamsini vya shaba, uviingize katika vile vitanzi ili kukaza hema pamoja kuwa kitu kimoja. Kuhusu kile kipande cha ziada cha pazia za hema, nusu ya hilo pazia lililobaki litaningʼinizwa upande wa nyuma wa maskani ya Mungu. Mapazia ya hema yatakuwa na urefu wa dhiraa moja zaidi pande zote, sehemu itakayobaki itaningʼinia pande zote za Maskani ili kuifunika. Tengeneza kifuniko cha hema kwa ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo. “Tengeneza mihimili ya kusimamisha ya mti wa mshita kwa ajili ya maskani ya Mungu. Kila mhimili uwe na urefu wa dhiraa kumi na upana wa dhiraa moja na nusu, zikiwa na ndimi mbili zilizo sambamba kila mmoja na mwingine. Tengeneza mihimili yote ya Maskani jinsi hii. Tengeneza mihimili ishirini kwa ajili ya upande wa kusini wa Maskani, kisha tengeneza vitako arobaini vya fedha vya kuweka chini ya hiyo mihimili, vitako viwili kwa kila mhimili, kimoja chini ya kila ulimi. Kuhusu upande wa kaskazini wa Maskani, tengeneza mihimili ishirini na vitako arobaini vya fedha, viwili chini ya kila mhimili. Kisha tengeneza mihimili sita kwa mwisho ulio mbali, yaani upande wa magharibi wa Maskani, na pia utengeneze mihimili miwili ya pembe za upande ulio mbali. Katika pembe hizi mbili ni lazima mihimili yake iwe miwili kuanzia chini hadi juu, na iingizwe kwenye pete moja; mihimili ya pembe hizi mbili itafanana. Kwa hiyo kutakuwa mihimili nane, na vitako kumi na sita vya fedha, viwili chini ya kila mhimili. “Pia tengeneza mataruma ya mti wa mshita: matano kwa ajili ya mihimili ya upande mmoja wa Maskani, matano kwa ajili ya mihimili ya upande mwingine, na matano kwa ajili ya mihimili ya upande wa magharibi, mwisho kabisa mwa Maskani. Taruma la katikati litapenya katikati ya mihimili kutoka mwisho mmoja hadi mwisho mwingine. Funika hiyo mihimili kwa dhahabu, kisha tengeneza pete za dhahabu ambazo zitashikilia hayo mataruma. Pia funika hayo mataruma kwa dhahabu. “Simamisha maskani ya Mungu sawasawa na mfano uliooneshwa kule mlimani. “Tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, naye fundi stadi atirizi makerubi kwenye hilo pazia. Litundike kwa kulabu za dhahabu kwenye nguzo nne za mti wa mshita ambazo zimefunikwa kwa dhahabu, zikiwa zimesimamishwa kwenye vitako vinne vya fedha. Ningʼiniza pazia hilo kwenye vifungo, kisha weka Sanduku la Ushuhuda nyuma ya pazia. Pazia litatenganisha Mahali Patakatifu kutoka Patakatifu pa Patakatifu. Weka kifuniko cha kiti cha rehema juu ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Patakatifu pa Patakatifu. Weka meza nje ya pazia upande wa kaskazini wa maskani ya Mungu, kisha weka kinara cha taa upande wa kusini wa maskani. “Kwa ajili ya ingilio la hema, tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi. Tengeneza kulabu za dhahabu kwa ajili ya hilo pazia, na nguzo tano za mshita zilizofunikwa kwa dhahabu. Kisha subu vitako vitano vya shaba kwa ajili yake.