Kutoka 24:9-18
Kutoka 24:9-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Mose, Aroni, Nadabu na Abihu na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya johari ya rangi ya samawati, kikiwa safi kama mbingu angavu. Na Mungu hakuwadhuru hao viongozi wa watu wa Israeli. Walimwona Mungu, wakala na kunywa. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Njoo kwangu juu mlimani, ungoje huko. Mimi nitakupa vibao viwili vya mawe vyenye sheria na amri nilizoandika kwa ajili ya kuwafunza Waisraeli.” Basi, Mose akaondoka pamoja na Yoshua, mtumishi wake, akaenda kwenye mlima wa Mungu. Mose aliwaambia wale wazee, “Tungojeni hapa mpaka tutakapowarudia. Aroni na Huri wako pamoja nanyi; yeyote aliye na tatizo na awaendee wao.” Basi, Mose akaenda mlimani, na wingu likaufunika mlima. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukatua juu ya mlima Sinai na wingu likaufunika mlima kwa muda wa siku sita. Siku ya saba Mungu akamwita Mose kutoka katikati ya lile wingu. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulionekana mbele ya macho ya watu wa Israeli kama moto unaowaka juu ya mlima. Mose akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani. Alikaa huko kwa muda wa siku arubaini, mchana na usiku.
Kutoka 24:9-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo akakwea juu, Musa, na Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa. BWANA akamwambia Musa, Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa vibao vya mawe na ile sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe. Musa akaondoka na Yoshua, mtumishi wake, Musa akapanda mlimani kwa Mungu. Akawaambia hao wazee, Tungojeeni hapa, mpaka tutakaporudi kwenu; na tazameni, Haruni na Huri wapo pamoja nanyi; kila mtu aliye na jambo na awaendee. Musa akapanda mlimani, lile wingu likaufunikiza mlima. Na huo utukufu wa BWANA ukakaa juu ya mlima wa Sinai; lile wingu likaufunikiza siku sita; na siku ya saba akamwita Musa toka kati ya lile wingu. Na kuonekana kwake ule utukufu wa BWANA kulikuwa kama moto uteketezao, juu ya mlima machoni pa wana wa Israeli. Musa akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani; Musa akawa humo katika ule mlima siku arubaini, mchana na usiku.
Kutoka 24:9-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo akakwea juu, Musa, na haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa. BWANA akamwambia Musa, Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe. Musa akaondoka na Yoshua, mtumishi wake, Musa akapanda mlimani kwa Mungu. Akawaambia hao wazee, Tungojeeni hapa, mpaka tutakaporudi kwenu; na tazameni, Haruni na Huri wapo pamoja nanyi; kila mtu aliye na neno na awaendee. Musa akapanda mlimani, lile wingu likaufunikiza mlima. Na huo utukufu wa BWANA ukakaa juu ya mlima wa Sinai; lile wingu likaufunikiza siku sita; na siku ya saba akamwita Musa toka kati ya lile wingu. Na kuonekana kwake ule utukufu wa BWANA kulikuwa kama moto uteketezao, juu ya mlima machoni pa wana wa Israeli. Musa akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani; Musa akawa humo katika ule mlima siku arobaini, mchana na usiku.
Kutoka 24:9-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Musa na Haruni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, nao wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya yakuti samawi, iliyo safi kama anga angavu. Lakini Mungu hakuinua mkono wake dhidi ya hawa viongozi wa Waisraeli; walimwona Mungu, nao wakala na kunywa. BWANA akamwambia Musa, “Panda uje kwangu huku mlimani na ukae hapa, nami nitakupa vibao vya mawe, vyenye sheria na amri ambazo nimeziandika ziwe mwongozo wao.” Basi Musa akaondoka na Yoshua mtumishi wake, naye Musa akapanda juu kwenye mlima wa Mungu. Musa akawaambia wazee wa Israeli, “Tungojeni hapa hadi tutakapowarudia. Haruni na Huri wako pamoja nanyi, na kila aliye na shauri aweza kuwaendea wao.” Musa alipopanda juu mlimani, wingu liliufunika huo mlima, nao utukufu wa BWANA ukatua juu ya Mlima Sinai. Kwa muda wa siku sita wingu lilifunika mlima, na siku ya saba BWANA akamwita Musa kutoka kati ya lile wingu. Kwa Waisraeli utukufu wa BWANA ulionekana kama moto uteketezao juu ya mlima. Kisha Musa akaingia ndani ya lile wingu alivyokuwa akipanda mlimani. Naye akakaa huko mlimani kwa muda wa siku arobaini, usiku na mchana.