Kutoka 23:1-19
Kutoka 23:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
“Usitoe habari za uongo. Usishirikiane na mtu mwovu ili kuwa shahidi mbaya. Usifuate genge la watu kutenda uovu, wala usijumuike na genge la watu kutoa ushahidi mahakamani ili kupotosha haki. Usiwe na upendeleo katika kesi ya maskini. “Ukimkuta ng'ombe au punda wa adui yako amepotea, utamrudishia mwenyewe. Ukimwona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, msaidie mtu huyo kumsimamisha punda wake, wala usimwache na kwenda zako. “Usiipotoshe haki anayostahili maskini katika kesi yake. Jitenge mbali na mashtaka ya uongo wala usiwaue wasio na hatia na waadilifu, maana mimi sitamsamehe mtu mwovu. Usipokee rushwa, maana rushwa huwapofusha wakuu na kupotosha mambo ya wenye haki. “Usimdhulumu mgeni; nyinyi mwajua hali ya kuwa mgeni, maana mlikuwa wageni nchini Misri. “Kwa muda wa miaka sita utapanda mashamba yako na kuvuna mazao yake. Lakini mnamo mwaka wa saba, utayaacha mashamba yako bila kupanda mbegu, ili maskini miongoni mwa watu wako wapate chakula kilichosalia humo, na wanyama wa porini wale. Utafanya vivyo hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni. “Kwa siku sita utafanya kazi zako, lakini siku ya saba utapumzika, ili ng'ombe wako na punda wako pia wapate kupumzika; na watumwa wako na watumishi wa kigeni wapate kustarehe. Yazingatie yote niliyokuambia. Usiyataje hata kidogo majina ya miungu mingine; hayo yasisikike kinywani mwako. “Mara tatu kila mwaka mtafanya sikukuu kwa heshima yangu. Mtaadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu: Kama nilivyowaagiza, mtakula mikate isiyotiwa chachu kwa siku saba wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kwa sababu katika mwezi huo mlitoka Misri. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu. Mtaadhimisha sikukuu ya mavuno ya kwanza ya kazi zenu na ya mavuno ya mashamba yenu. Mtaadhimisha sikukuu ya kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka mnapokusanya mazao ya kazi zenu. Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele zangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu. “Usinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala usiyaache mafuta ya sikukuu yangu yabaki mpaka asubuhi. “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. “Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.
Kutoka 23:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Usivumishe habari za uongo; usishirikiane na mwovu kwa kuwa shahidi wa uongo. Usiwafuate walio wengi kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lolote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu; wala usimpendelee mtu mnyonge katika neno lake. Ukimwona ng'ombe wa adui wako, au punda wake, amepotea, sharti umrudishie mwenyewe tena. Ukimwona punda wake huyo akuchukiaye akiwa ameanguka chini ya mzigo wake, na wewe ungejizuia usimsaidie, lazima umsaidie. Usipotoe hukumu ya mtu maskini katika neno lake. Jitenge mbali na neno la uongo; wala wasio hatia na wenye haki usiwaue; kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu. Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki. Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Utapanda mbegu katika nchi yako muda wa miaka sita na kupata mavuno yake; lakini mwaka wa saba utaiacha nchi ipumzike na kutulia; hao maskini miongoni mwa watu wako wapate kula; na hicho watakachosaza wao, wapate kula wanyama wa kondeni. Utafanya vivyo hivyo katika shamba lako la mizabibu, na katika shamba lako la mizeituni. Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng'ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika. Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako. Mara tatu kila mwaka utaniwekea sikukuu. Utaiweka sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu; utakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba kama nilivyokuagiza, kwa wakati uliowekwa, mwezi wa Abibu (kwa maana ndio mwezi uliotoka Misri); wala hapana mtu atakayeonekana mbele yangu na mikono mitupu; tena, sikukuu ya mavuno, hayo malimbuko ya kazi zako za kupanda mashambani; tena, sikukuu ya kukusanya, mwisho wa mwaka, hapo utakapokusanya hayo uliyoyataabikia shambani. Mara tatu katika mwaka wana wa kiume wako wote watahudhuria mbele ya Bwana MUNGU. Usinitolee damu ya dhabihu zangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala mafuta ya sikukuu yangu usiyaache kusalia hadi asubuhi. Ya kwanza ya malimbuko ya nchi yako utayaleta na kuyatia ndani ya nyumba ya BWANA, Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
Kutoka 23:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu. Usiandamane na mkutano kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lo lote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu; wala usimpendelee mtu mnyonge katika neno lake. Ukimwona ng’ombe wa adui wako, au punda wake, amepotea, sharti umrudishie mwenyewe tena. Ukimwona punda wake huyo akuchukiaye hali ameanguka chini ya mzigo wake, nawe ungejizuia usimsaidie, lazima umsaidie. Usipotoe hukumu ya mtu maskini katika neno lake. Jitenge mbali na neno uongo; wala wasio hatia na wenye haki usiwaue; kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu. Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki. Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Utapanda mbegu katika nchi yako muda wa miaka sita na kuyavuna maongeo yake; lakini mwaka wa saba utaiacha nchi ipumzike na kutulia; hao maskini miongoni mwa watu wako wapate kula; na hicho watakachosaza wao, wapate kula wanyama wa kondeni. Utafanya vivyo katika shamba lako la mizabibu, na katika shamba lako la mizeituni. Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng’ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika. Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako. Mara tatu kila mwaka utaniwekea sikukuu. Utaiweka sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu; utakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba kama nilivyokuagiza, kwa wakati uliowekwa, mwezi wa Abibu (kwa maana ndio mwezi uliotoka Misri); wala hapana mtu atakayeonekana mbele yangu na mikono mitupu; tena, sikukuu ya mavuno, hayo malimbuko ya kazi zako za kupanda mashambani; tena, sikukuu ya kukusanya, mwisho wa mwaka, hapo utakapokusanya hayo uliyoyataabikia shambani. Mara tatu katika mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele ya Bwana MUNGU. Usisongeze damu ya dhabihu zangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala mafuta ya sikukuu yangu usiyaache kusalia hata asubuhi. Ya kwanza ya malimbuko ya nchi yako utayaleta na kuyatia ndani ya nyumba ya BWANA, Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
Kutoka 23:1-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Usieneze habari za uongo. Usimsaidie mtu mwovu kwa kuwa shahidi mwenye nia ya kudhuru wengine. “Usifuate umati wa watu katika kutenda mabaya. Unapotoa ushahidi kwenye mashtaka, usipotoshe haki ukijumuika na umati wa watu, nawe usimpendelee mtu maskini katika mashtaka yake. “Ukikutana na maksai au punda wa adui yako anapotea, hakikisha umemrudisha kwake. Ukiona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, usimwache hapo alipoangukia; hakikisha kuwa umemsaidia. “Usiwanyime haki watu wako walio maskini katika mashtaka yao. Ujiepushe na mashtaka ya uongo, wala usimuue mtu asiye na hatia au mtu mwaminifu, kwa maana sitamhesabia hana hatia yeye aliye na hatia. “Usipokee rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha wale waonao, na kupinda maneno ya wenye haki. “Usimdhulumu mgeni; ninyi wenyewe mnajua jinsi mgeni anavyojisikia, kwa sababu mlikuwa wageni Misri. “Kwa muda wa miaka sita mtapanda mashamba yenu na kuvuna mazao, lakini katika mwaka wa saba usiilime ardhi wala kuitumia, ili watu walio maskini miongoni mwenu waweze kupata chakula kwenye hayo mashamba, nao wanyama pori wapate chakula kwa yale mabaki watakayobakiza. Utafanya hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni. “Kwa siku sita fanya kazi zako, lakini siku ya saba usifanye kazi, ili maksai wako na punda wako wapate kupumzika, naye mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwako, pamoja na mgeni, wapate kuburudishwa. “Uzingatie kutenda kila kitu nilichokuambia. Usiombe kwa majina ya miungu mingine, wala usiyaruhusu kusikika kinywani mwako. “Mara tatu kwa mwaka utanifanyia sikukuu. “Utaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu; kwa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu kama nilivyokuagiza. Fanya jambo hili kwa wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kwa sababu katika mwezi huo ulitoka Misri. “Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu. “Utaadhimisha Sikukuu ya Mavuno kwa malimbuko ya mazao yako uliyopanda katika shamba lako. “Utaadhimisha Sikukuu ya Kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka, unapokusanya mavuno yako toka shambani. “Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakuja mbele za BWANA Mwenyezi. “Msitoe damu ya dhabihu kwangu pamoja na kitu chochote kilicho na chachu. “Mafuta ya mnyama wa sadaka ya sikukuu yangu yasibakizwe hadi asubuhi. “Utaleta malimbuko bora ya ardhi yako katika nyumba ya BWANA Mungu wako. “Usimchemshe mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.