Kutoka 22:1-6
Kutoka 22:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mtu akiiba ng'ombe au kondoo na kumchinja au kumwuza, atatozwa ng'ombe watano kwa kila ng'ombe, na kondoo wanne kwa kila kondoo. Mwizi akipatikana anavunja nyumba, akapigwa hata akafa, aliyemuua hana hatia ya mauaji. Lakini mwizi huyo akishikwa wakati jua limechomoza na kuuawa, aliyemuua atakuwa na hatia. Huyo mwizi anapaswa kulipa. Ikiwa hana kitu cha kulipa, basi, yeye mwenyewe atauzwa ili kulipia wizi wake. Kama mnyama aliyeibiwa atapatikana kwa huyo mwizi akiwa hai, basi, mwizi atalipa mara mbili, awe ni ng'ombe, punda au kondoo. “Mtu akiwalisha wanyama wake katika shamba la mizabibu au kumwachia mnyama wake kula katika shamba la mtu mwingine, atalipa hasara hiyo kwa mazao bora ya shamba lake mwenyewe au shamba lake la mizabibu. “Mtu akiwasha moto nao ukachoma miti ya miiba na kusambaa hadi kuteketeza miganda ya nafaka, au nafaka ya mtu mwingine ambayo bado haijavunwa, au shamba lote likateketea, aliyewasha moto huo lazima alipe hasara hiyo yote.
Kutoka 22:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mtu akiiba ng'ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng'ombe watano badala ya ng'ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja. Mwizi akipatikana akiwa yu hali ya kuvunja mahali, naye akapigwa hata akafa, hapatakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake. Lakini kama jua limekucha juu yake, ndipo patakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake; ingempasa kutoa malipo kamili; akiwa hana kitu, na auzwe kwa ajili ya wizi wake. Kama hicho kitu kilichoibwa chapatikana hai mkononi mwake, kama ni ng'ombe, au punda, au kondoo; atalipa thamani yake mara mbili. Mtu akilisha mifugo kama shamba, au shamba la mizabibu, akimwacha mnyama wake, akala katika shamba la mtu mwingine; atalipa katika vitu vilivyo vizuri vya shamba lake mwenyewe, au vya mizabibu yake. Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa.
Kutoka 22:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mtu akiiba ng’ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng’ombe watano badala ya ng’ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja. Mwivi akipatikana akiwa yu hali ya kuvunja mahali, naye akapigwa hata akafa, hapatakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake. Lakini kama jua limekucha juu yake, ndipo patakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake; ingempasa kutoa malipo kamili; akiwa hana kitu, na auzwe kwa ajili ya wivi wake. Kama hicho kitu kilichoibwa chapatikana hai mkononi mwake, kama ni ng’ombe, au punda, au kondoo; atalipa thamani yake mara mbili. Mtu akilisha katika shamba, au shamba la mizabibu, akimwacha mnyama wake, akala katika shamba la mtu mwingine; atalipa katika vitu vilivyo vizuri vya shamba lake mwenyewe, au vya mizabibu yake. Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa.
Kutoka 22:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Mtu yeyote akiiba maksai au kondoo na kumchinja au kumuuza, ni lazima alipe ngʼombe watano badala ya maksai mmoja na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja. “Mwizi akishikwa akivunja nyumba akapigwa hata akafa, aliyemuua hana hatia ya kumwaga damu; lakini jambo hilo likitokea wakati jua limechomoza, huyo mtu atakuwa na hatia ya kumwaga damu. “Mwizi huyo sharti alipe, lakini kama hana kitu, lazima auzwe ili alipe kwa ajili ya wizi wake. “Mnyama aliyeibwa akikutwa hai mkononi mwake, iwe ni maksai au punda au kondoo, lazima alipe mara mbili. “Mtu akichunga mifugo yake katika shamba au shamba la mizabibu, na akawaachia walishe katika shamba la mtu mwingine, ni lazima alipe vitu bora kutoka shamba lake mwenyewe au kutoka shamba lake la mizabibu. “Moto ukiwaka na kuenea kwenye vichaka vya miiba na kuteketeza miganda ya nafaka au nafaka ambayo haijavunwa, au kuteketeza shamba lote, mtu yule aliyewasha moto lazima alipe.