Kutoka 22:1-31
Kutoka 22:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mtu akiiba ng'ombe au kondoo na kumchinja au kumwuza, atatozwa ng'ombe watano kwa kila ng'ombe, na kondoo wanne kwa kila kondoo. Mwizi akipatikana anavunja nyumba, akapigwa hata akafa, aliyemuua hana hatia ya mauaji. Lakini mwizi huyo akishikwa wakati jua limechomoza na kuuawa, aliyemuua atakuwa na hatia. Huyo mwizi anapaswa kulipa. Ikiwa hana kitu cha kulipa, basi, yeye mwenyewe atauzwa ili kulipia wizi wake. Kama mnyama aliyeibiwa atapatikana kwa huyo mwizi akiwa hai, basi, mwizi atalipa mara mbili, awe ni ng'ombe, punda au kondoo. “Mtu akiwalisha wanyama wake katika shamba la mizabibu au kumwachia mnyama wake kula katika shamba la mtu mwingine, atalipa hasara hiyo kwa mazao bora ya shamba lake mwenyewe au shamba lake la mizabibu. “Mtu akiwasha moto nao ukachoma miti ya miiba na kusambaa hadi kuteketeza miganda ya nafaka, au nafaka ya mtu mwingine ambayo bado haijavunwa, au shamba lote likateketea, aliyewasha moto huo lazima alipe hasara hiyo yote. “Mtu akimwachia mwenzake fedha au mali nyingine amtunzie, kisha ikaibiwa nyumbani mwake, mwizi akipatikana lazima alipe thamani yake mara mbili. Lakini mwizi asipopatikana, mwenye nyumba atakaribia mbele za Mungu ili kuthibitisha kwamba hakuhusika na wizi wa mali ya mwenzake. “Pakiwa na ubishi juu ya ng'ombe, au punda, au kondoo, au mavazi, au kitu chochote kilichopotea ambacho kila mmoja anadai ni chake, wanaohusika wataletwa mbele za Mungu. Yule ambaye Mungu ataamua amekosa, atamlipa mwenzake mara mbili. “Mtu akimkabidhi mwenzake punda, ng'ombe, kondoo au mnyama mwingine yeyote amtunzie, na mnyama huyo akafa au akaumia au akachukuliwa bila mtu yeyote kushuhudia, kiapo mbele ya Mwenyezi-Mungu kitaamua kati yao, kuonesha kwamba huyo aliyekabidhiwa hakuhusika na wizi wa mali ya mwenzake. Mwenye mnyama huyo atakubali hicho kiapo, na huyo mwenzake hatalipa malipo yoyote. Lakini kama aliibiwa kwake, ni lazima amlipe mwenyewe. Kama huyo mnyama aliraruliwa na wanyama wa porini, huyo mtu aliyekuwa amekabidhiwa lazima amlete kama ushahidi. Hatalipa malipo yoyote kwa ajili ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama wa porini. “Mtu akiazima mnyama kwa mwenzake, kisha mnyama huyo akaumia au akafa wakati mwenyewe hayuko, aliyeazima mnyama huyo ni lazima alipe kikamilifu. Lakini kama mwenyewe alikuwako, basi aliyemwazima hatalipa chochote. Kama alikuwa ni mnyama aliyekodishwa, mwenyewe ataikubali tu bei ya kukodisha. “Mtu akimshawishi bikira ambaye hajaposwa, akalala naye, lazima atoe mahari na kumwoa msichana huyo. Baba wa huyo msichana akikataa katakata kumwoza binti yake, mtu huyo atalipa fedha ya mahari inayostahili msichana aliye bikira. “Usimwache mwanamke mchawi aishi. “Anayezini na mnyama lazima auawe. “Anayemtolea tambiko mungu mwingine badala ya Mwenyezi-Mungu pekee, lazima aangamizwe kabisa. “Msimdhulumu mgeni wala kumtesa, maana nanyi pia mlikuwa wageni nchini Misri. Msimtese mjane au yatima. Kama mkiwadhulumu hao nao wakanililia, hakika nitakisikiliza kilio chao, na hasira yangu itawaka, nami nitawaueni kwa upanga, na wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu yatima. “Ukimkopesha fedha mtu yeyote miongoni mwa watu wangu walio maskini, usiwe kwake kama mdai, wala usimtoze riba. Ukilichukua vazi la mwenzako kuliweka rehani, lazima umrudishie kabla ya jua kutua, kwa kuwa hiyo ndiyo nguo yake ya pekee; ndiyo atakayojifunika nayo. Au wadhani atalalia nini? Akinililia nitamsikiliza, maana mimi ni mwenye huruma. “Usimtukane Mungu, wala kumlaani mkuu wa watu wako. “Usikawie kunitolea sehemu yangu kutokana na wingi wa mazao yako na divai yako. Mtanipa wazaliwa wenu wa kwanza wa kiume. Mtafanya vivyo hivyo kuhusu wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na kondoo wenu. Mtamwacha kila mzaliwa wa kwanza na mama yake kwa siku saba, na siku ya nane mtanitolea. Nyinyi mtakuwa watu waliowekwa wakfu kwangu. Kwa hiyo hamtakula nyama ya mnyama aliyeuawa na mnyama wa porini. Nyama hiyo mtawatupia mbwa.
Kutoka 22:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mtu akiiba ng'ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng'ombe watano badala ya ng'ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja. Mwizi akipatikana akiwa yu hali ya kuvunja mahali, naye akapigwa hata akafa, hapatakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake. Lakini kama jua limekucha juu yake, ndipo patakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake; ingempasa kutoa malipo kamili; akiwa hana kitu, na auzwe kwa ajili ya wizi wake. Kama hicho kitu kilichoibwa chapatikana hai mkononi mwake, kama ni ng'ombe, au punda, au kondoo; atalipa thamani yake mara mbili. Mtu akilisha mifugo kama shamba, au shamba la mizabibu, akimwacha mnyama wake, akala katika shamba la mtu mwingine; atalipa katika vitu vilivyo vizuri vya shamba lake mwenyewe, au vya mizabibu yake. Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa. Mtu akimpa mwenziwe amana ya fedha au vitu vingine amtunzie, na vitu vile vikaibwa katika nyumba ya mtu huyo; mwizi akipatikana, atalipa thamani yake mara mbili. Mwizi asipopatikana, ndipo mwenye nyumba atakaribia mbele ya Mungu, ionekane kwamba si yeye aliyetia mkono na kutwaa vyombo vya mwenziwe. Kila jambo la kukosana, kama ni la ng'ombe, au la punda, au la kondoo, au la mavazi, au la kitu chochote kilichopotea, ambacho mtu mmoja asema ni chake, hilo jambo la watu wote wawili litaletwa mbele ya Mungu; na yeye atakayehukumiwa na Mungu kuwa ni mkosa atamlipa mwenziwe thamani yake mara mbili. Mtu akimpa mwenziwe punda, au ng'ombe, au kondoo, au mnyama yeyote, ili amtunzie; yule mnyama akafa, au akaumia, au akachukuliwa mtu asione; patakuwa na kiapo cha BWANA katikati ya watu hao wawili, kwamba alipeleka mkono wake kutwaa mali ya mwenziwe, na mwenyewe atakubali hayo, wala hatalipa. Lakini kwamba aliibiwa mnyama huyo, sharti amlipe yule mwenyewe. Kama aliraruliwa na mnyama mkali, na amlete uwe ushahidi; hatalipa kwa ajili ya mnyama aliyeraruliwa. Mtu akiazima mnyama kwa mwenziwe, naye akaumia huyo mnyama, au akafa, mwenyewe asipokuwapo, lazima atalipa. Kama huyo mwenyewe alikuwapo pamoja na mnyama wake, hatalipa; kama ni mnyama wa kukodisha ni gharama ya kukodisha tu atakayepewa mwenyewe. Mtu akimshawishi mwanamwali, aliyeposwa na mume, na kulala naye, lazima atatoa mahari kwa ajili yake ili awe mkewe. Ikiwa baba yake huyo mwanamwali akataa kabisa kumpa, atalipa fedha kama hesabu ya mahari ya mwanamwali ilivyo. Usimwache mwanamke mchawi kuishi. Mtu yeyote alalaye na mnyama sharti atauawa. Mtu atakayemchinjia sadaka mungu yeyote, isipokuwa ni yeye BWANA peke yake, na angamizwe kabisa. Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Usimtese mjane yeyote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao katika neno lolote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima. Ukimkopesha mtu aliye maskini, katika watu wangu walio pamoja nawe; usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia faida. Ikiwa wewe kwa njia yoyote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima utamrudishia mbele ya jua kuchwa; maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake; je! Atalalia nini? Itakuwa, hapo atakaponililia mimi, nitasikia; kwa kuwa mimi ni mwenye rehema. Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa watu wako. Usikawie kuleta malimbuko ya matunda yako na ya vinywaji vyako. Mzaliwa wa kwanza katika wanao wanaume utanipa mimi. Nawe utafanya vivyo hivyo katika ng'ombe wako, na kondoo wako; utamwacha siku saba pamoja na mama yake; siku ya nane utanipa mimi. Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yoyote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo.
Kutoka 22:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mtu akiiba ng’ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng’ombe watano badala ya ng’ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja. Mwivi akipatikana akiwa yu hali ya kuvunja mahali, naye akapigwa hata akafa, hapatakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake. Lakini kama jua limekucha juu yake, ndipo patakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake; ingempasa kutoa malipo kamili; akiwa hana kitu, na auzwe kwa ajili ya wivi wake. Kama hicho kitu kilichoibwa chapatikana hai mkononi mwake, kama ni ng’ombe, au punda, au kondoo; atalipa thamani yake mara mbili. Mtu akilisha katika shamba, au shamba la mizabibu, akimwacha mnyama wake, akala katika shamba la mtu mwingine; atalipa katika vitu vilivyo vizuri vya shamba lake mwenyewe, au vya mizabibu yake. Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa. Mtu akimpa mwenziwe amana ya fedha au vitu vingine amtunzie, na vitu vile vikaibwa katika nyumba ya mtu huyo; mwivi akipatikana, atalipa thamani yake mara mbili. Mwivi asipopatikana, ndipo mwenye nyumba atakaribia mbele ya Mungu, ionekane kwamba si yeye aliyetia mkono na kutwaa vyombo vya mwenziwe. Kila jambo la kukosana, kama ni la ng’ombe, au la punda, au la kondoo, au la mavazi, au la kitu cho chote kilichopotea, ambacho mtu mmoja asema ni chake, hilo jambo la watu wote wawili litaletwa mbele ya Mungu; na yeye atakayehukumiwa na Mungu kuwa ni mkosa atamlipa mwenziwe thamani yake mara mbili. Mtu akimpa mwenziwe punda, au ng’ombe, au kondoo, au mnyama ye yote, ili amtunzie; yule mnyama akafa, au akaumia, au akachukuliwa mtu asione; patakuwa na kiapo cha BWANA katikati ya watu hao wawili, kwamba alipeleka mkono wake kutwaa mali ya mwenziwe, na mwenyewe atakubali hayo, wala hatalipa. Lakini kwamba aliibiwa mnyama huyo, sharti amlipe yule mwenyewe. Kwamba aliraruliwa na mnyama mkali, na amlete uwe ushahidi; hatalipa kwa ajili ya mnyama aliyeraruliwa. Mtu akiazima mnyama kwa mwenziwe, naye akaumia huyo mnyama, au akafa, mwenyewe asipokuwapo, lazima atalipa. Kama huyo mwenyewe alikuwapo pamoja na mnyama wake, hatalipa; kama ni mnyama aliyeajiriwa, alikwenda kwa ajili ya ujira wake. Mtu akimshawishi mwanamwali, aliyeposwa na mume, na kulala naye, lazima atatoa mahari kwa ajili yake ili awe mkewe. Ikiwa baba yake huyo mwanamwali akataa kabisa kumpa, atalipa fedha kama hesabu ya mahari ya mwanamwali ilivyo. Usimwache mwanamke mchawi kuishi. Mtu awaye yote alalaye na mnyama sharti atauawa. Mtu atakayemchinjia sadaka mungu ye yote, isipokuwa ni yeye BWANA peke yake, na angamizwe kabisa. Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao katika neno lo lote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima. Ukimkopesha mtu aliye maskini, katika watu wangu walio pamoja nawe; usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia faida. Ikiwa wewe kwa njia yo yote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima utamrudishia mbele ya jua kuchwa; maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake; je! Atalalia nini? Itakuwa, hapo atakaponililia mimi, nitasikia; kwa kuwa mimi ni mwenye rehema. Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa watu wako. Usikawie kuleta malimbuko ya matunda yako na ya vinywaji vyako. Mzaliwa wa kwanza katika wanao waume utanipa mimi. Nawe utafanya vivyo katika ng’ombe zako, na kondoo zako; utamwacha siku saba pamoja na mama yake; siku ya nane utanipa mimi. Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yo yote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo.
Kutoka 22:1-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Mtu yeyote akiiba maksai au kondoo na kumchinja au kumuuza, ni lazima alipe ngʼombe watano badala ya maksai mmoja na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja. “Mwizi akishikwa akivunja nyumba akapigwa hata akafa, aliyemuua hana hatia ya kumwaga damu; lakini jambo hilo likitokea wakati jua limechomoza, huyo mtu atakuwa na hatia ya kumwaga damu. “Mwizi huyo sharti alipe, lakini kama hana kitu, lazima auzwe ili alipe kwa ajili ya wizi wake. “Mnyama aliyeibwa akikutwa hai mkononi mwake, iwe ni maksai au punda au kondoo, lazima alipe mara mbili. “Mtu akichunga mifugo yake katika shamba au shamba la mizabibu, na akawaachia walishe katika shamba la mtu mwingine, ni lazima alipe vitu bora kutoka shamba lake mwenyewe au kutoka shamba lake la mizabibu. “Moto ukiwaka na kuenea kwenye vichaka vya miiba na kuteketeza miganda ya nafaka au nafaka ambayo haijavunwa, au kuteketeza shamba lote, mtu yule aliyewasha moto lazima alipe. “Mtu akimpa jirani yake fedha au mali nyingine amtunzie, vitu vile vikiibwa kutoka nyumba ya huyo jirani, kama mwizi akishikwa, lazima alipe mara mbili. Lakini mwizi asipopatikana, mwenye nyumba atafika mbele ya waamuzi ili kuthibitisha kuwa hakuchukua mali ya mwenzake. Pakiwepo jambo lolote la mali isiyo halali, iwe ni maksai, punda, kondoo, mavazi, ama mali yoyote iliyopotea, ambayo mtu fulani atasema, ‘Hii ni mali yangu,’ kila upande utaleta shauri lake mbele ya waamuzi. Yule ambaye waamuzi watathibitisha kuwa ana hatia atamlipa jirani yake mara mbili. “Mtu akimpa jirani yake punda, ngʼombe, kondoo au mnyama mwingine yeyote amtunzie, yule mnyama akifa, au akijeruhiwa, au akiibiwa bila mtu kuona, jambo hili kati yao wawili litaamuliwa kwa kuapa mbele za BWANA, kwamba huyo jirani hakuhusika na wizi wa mali ya jirani yake. Mwenye mali itampasa akubali jambo hili, na hakuna malipo yatakayohitajika. Lakini kama mnyama aliibwa kwa jirani, itampasa amlipe mwenye mnyama. Kama ameraruliwa na mnyama pori, ataleta mabaki ya mnyama kama ushahidi, naye hatadaiwa mnyama aliyeraruliwa. “Mtu akiazima mnyama kutoka kwa jirani yake, huyo mnyama akiumia au akafa na mwenye mnyama hayupo, lazima amlipe huyo mnyama. Lakini mwenye mnyama akiwa bado ako na mnyama wake, aliyeazima hatalazimika kumlipa. Kama mnyama alikuwa amekodishwa, fedha iliyolipwa kwa kukodisha inatosha kwa kufidia hasara. “Mtu akimshawishi bikira ambaye hajaposwa na akalala naye, lazima alipe mahari, kisha atamwoa msichana huyo. Baba wa msichana akikataa katakata kumpa huyo mtu binti yake, bado ni lazima huyo mtu atalipa mahari kama inavyostahili malipo ya ubikira. “Usiruhusu mwanamke mchawi aishi. “Mtu yeyote aziniye na mnyama lazima auawe. “Mtu yeyote anayemtolea mungu mwingine dhabihu isipokuwa BWANA, lazima aangamizwe. “Usimtendee mgeni vibaya au kumdhulumu, kwa kuwa nanyi mlikuwa wageni huko Misri. “Usimdhulumu mjane wala yatima. Ukifanya hivyo nao wakinililia, hakika nitasikia kilio chao. Hasira yangu itawaka, nami nitawaua kwa upanga, wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu watakuwa yatima. “Ukimkopesha mmoja wa watu wangu fedha ambaye ni mhitaji, usiwe kama mtu mkopesha fedha; usimtoze riba. Ukichukua vazi la jirani kama rehani, ulirudishe kwake kabla jua kuzama, kwa kuwa vazi lake ndilo pekee alilo nalo la kumfunika mwili wake. Ni nini kingine atajifunika nacho? Atakaponililia, nitasikia, kwa kuwa nina huruma. “Usimkufuru Mungu au kumlaani mtawala wa watu wako. “Usiache kutoa sadaka kutoka ghala lako au mapipa yako. “Lazima unipe mzaliwa wa kwanza wa wana wako. Ufanye vivyo hivyo kwa ngʼombe wako na kwa kondoo wako. Waache wakae na mama zao kwa siku saba, lakini siku ya nane unipe. “Ninyi mtakuwa watu wangu watakatifu. Kwa hiyo msile nyama ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama pori; mtupieni mbwa.