Kutoka 20:1-26
Kutoka 20:1-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alizungumza maneno haya yote, akasema, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekutoa nchini Misri, ambako ulikuwa mtumwa. “Usiwe na miungu mingine ila mimi. “Usijifanyie sanamu ya miungu wa uongo, au kinyago cha chochote kilicho mbinguni, katika nchi au majini chini ya dunia. Usiisujudie wala kuitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu. Nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha hao wanichukiao. Lakini nawafadhili maelfu ya wale wanipendao na kuzishika amri zangu. “Usilitaje bure jina langu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Maana mimi Mwenyezi-Mungu sitaacha kumwadhibu anayetumia jina langu vibaya. “Usisahau kuiweka takatifu siku ya Sabato. Siku sita fanya kazi na tenda mambo yako yote. Lakini siku ya saba ni Sabato ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala watumishi wako wa kike, wala mnyama wako wa kufugwa, wala mgeni aliye nyumbani mwako. Maana kwa siku sita mimi Mwenyezi-Mungu niliziumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo, kisha nikapumzika siku ya saba. Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu niliibariki siku ya Sabato, nikaitakasa. “Waheshimu baba yako na mama yako, ili uishi maisha marefu katika nchi ninayokupa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. “Usiue. “Usizini. “Usiibe. “Usimshuhudie jirani yako uongo. “Usiitamani nyumba ya jirani yako, wala mke wake, wala mtumwa wake wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala chochote kilicho mali ya jirani yako.” Watu waliposikia ngurumo na kuona umeme ukiwaka na kuisikia sauti ya parapanda juu ya mlima uliokuwa unafuka moshi, wote waliogopa na kutetemeka. Wote walisimama mbali, wakamwambia Mose, “Ongea nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza, lakini Mwenyezi-Mungu asiongee nasi, tusije tukafa.” Mose akawaambia, “Msiogope, maana Mungu amekuja kuwajaribu ili mpate kumcha yeye daima na msitende dhambi.” Watu wote walisimama mbali wakati Mose alipokaribia lile wingu zito alimokuwamo Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli: ‘Mmejionea nyinyi wenyewe kwamba nimeongea nanyi kutoka mbinguni. Mtaniheshimu mimi peke yangu wala msijifanyie miungu ya fedha wala ya dhahabu. Nyinyi mtanijengea madhabahu ya udongo ambayo juu yake mtanitambikia kondoo wenu na ng'ombe wenu kama sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Mahali popote nitakapowakumbusha watu jina langu, papo hapo mimi mwenyewe nitawajia na kuwabariki. Kama mkinijengea madhabahu ya mawe, msiitengeneze kwa mawe ya kuchonga, maana mkitumia vyombo vya kuchongea mawe, mtaitia najisi. Wala msitengeneze madhabahu yenye ngazi za kupandia, mtu asije akauona uchi wa huyo anayepanda juu yake.’
Kutoka 20:1-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mungu akanena maneno haya yote akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako, maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure. Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa. Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako. Usiue. Usizini. Usiibe. Usimshuhudie jirani yako uongo. Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala chochote alicho nacho jirani yako. Watu wote wakaona umeme na ngurumo na sauti ya baragumu, na ule mlima kutoka moshi; na watu walipoona hayo wakatetemeka, wakasimama mbali. Wakamwambia Musa, Sema nasi wewe, nasi tutasikia, bali Mungu asiseme nasi, tusije tukafa. Musa akawaambia watu, Msiogope, maana Mungu amekuja ili awajaribu, na utisho wake uwe mbele yenu, ili kwamba msifanye dhambi. Basi hao watu wakasimama mbali, naye Musa akalikaribia lile giza kuu Mungu alipokuwapo. BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli hivi, Ninyi wenyewe mmeona ya kuwa nimenena nanyi kutoka mbinguni. Msifanye miungu mingine pamoja nami; miungu ya fedha, wala miungu ya dhahabu, msijifanyie. Utanifanyia madhabahu ya udongo, nawe utatoa dhabihu zako juu yake; sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani, kondoo wako, na ng'ombe wako, kila mahali nitakapotia ukumbusho wa jina langu, hapo ndipo nitakapokujilia na kukubarikia. Nawe ukinifanyia madhabahu ya mawe, hutaijenga ya mawe yaliyochongwa; kwa kuwa ukiwa umetumia chombo chako katika kuichonga umeitia unajisi. Tena hutapanda kwenda madhabahuni kwangu kwa daraja, uchi wako usidhihirike juu yake.
Kutoka 20:1-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mungu akanena maneno haya yote akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako, maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure. Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa. Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako. Usiue. Usizini. Usiibe. Usimshuhudie jirani yako uongo. Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako. Watu wote wakaona umeme na ngurumo na sauti ya baragumu, na ule mlima kutoka moshi; na watu walipoona hayo wakatetemeka, wakasimama mbali. Wakamwambia Musa, Sema nasi wewe, nasi tutasikia, bali Mungu asiseme nasi, tusije tukafa. Musa akawaambia watu, Msiogope, maana Mungu amekuja ili awajaribu, na utisho wake uwe mbele yenu, ili kwamba msifanye dhambi. Basi hao watu wakasimama mbali, naye Musa akalikaribia lile giza kuu Mungu alipokuwapo. BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli hivi, Ninyi wenyewe mmeona ya kuwa nimenena nanyi kutoka mbinguni. Msifanye miungu mingine pamoja nami; miungu ya fedha, wala miungu ya dhahabu, msijifanyie. Utanifanyia madhabahu ya udongo, nawe utatoa dhabihu zako juu yake; sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani, kondoo zako, na ng’ombe zako, kila mahali nitakapotia ukumbusho wa jina langu, hapo ndipo nitakapokujilia na kukubarikia. Nawe ukinifanyia madhabahu ya mawe, hutaijenga ya mawe yaliyochongwa; kwa kuwa ukiwa wewe umetumia chombo chako katika kuichonga umeitia unajisi. Tena hutapanda kwenda madhabahuni kwangu kwa daraja, uchi wako usidhihirike juu yake.
Kutoka 20:1-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Mungu akasema maneno haya yote: “Mimi ndimi BWANA Mungu wako, niliyekutoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. “Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni, au duniani chini, au ndani ya maji. Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, BWANA Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanaonichukia, lakini ninaonesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaonipenda na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure jina la BWANA Mungu wako, kwa kuwa BWANA hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure. Ikumbuke siku ya Sabato, uitakase. Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote, lakini siku ya saba ni Sabato kwa BWANA Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wako wa kiume au wa kike, wala wanyama wako, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Kwa kuwa kwa siku sita, BWANA aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo BWANA akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu. Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa BWANA Mungu wako. Usiue. Usizini. Usiibe. Usimshuhudie jirani yako uongo. Usiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake wa kiume au wa kike, wala ngʼombe wake au punda wake, wala chochote kile alicho nacho jirani yako.” Watu walipoona ngurumo na radi, na kusikia mlio wa tarumbeta, na kuuona mlima katika moshi, walitetemeka kwa woga. Wakasimama mbali na wakamwambia Musa, “Sema nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza. Lakini usimwache Mungu aseme nasi, la sivyo tutakufa.” Musa akawaambia watu, “Msiogope! Mungu amekuja kuwajaribu, ili hofu ya Mungu iwe nanyi kuwasaidia msitende dhambi.” Watu wakabaki mbali, wakati Musa alipolisogelea lile giza nene mahali pale Mungu alipokuwa. Kisha BWANA akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli hivi: ‘Mmejionea wenyewe kwamba nimesema nanyi kutoka mbinguni: Msijifanyizie miungu yoyote na kuilinganisha nami, msijitengenezee miungu ya fedha wala miungu ya dhahabu. “ ‘Utanitengenezea madhabahu ya udongo, na juu yake utoe sadaka za kuteketezwa kwa moto na sadaka za amani, kondoo na mbuzi, na ngʼombe wako. Popote nitakapofanya Jina langu liheshimiwe, nitakuja kwenu na kuwabariki. Ikiwa unanitengenezea madhabahu ya mawe, usiijenge kwa mawe ya kuchonga, maana mkitumia chombo cha kuchongea mtaitia unajisi. Usitumie ngazi kupanda kwenye madhabahu yangu, uchi wako usije ukadhihirika kwa chini.’