Kutoka 2:1-25
Kutoka 2:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa Walawi aliyemwoa mwanamke mmoja ambaye pia alikuwa wa ukoo wa Walawi. Basi, mama huyu akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Alipoona kwamba mtoto huyo mchanga alikuwa mzuri, akamficha kwa muda wa miezi mitatu. Lakini kwa vile hakuweza kumficha zaidi ya muda huo, alitengeneza namna ya kikapu cha mafunjo, akakipaka namna ya lami, akamtia huyo mtoto ndani. Kisha akakiweka kikapu kando ya mto Nili kwenye majani. Dada yake huyo mtoto akajificha karibu na mahali hapo ili aone yatakayompata nduguye. Basi, binti Farao akashuka mtoni kuoga, na watumishi wake wakawa wanatembeatembea kandokando ya mto. Binti Farao akakiona kile kikapu katika majani, akamtuma mjakazi wake akichukue. Alipokifungua, alimwona yule mtoto mchanga, analia. Basi, akamwonea huruma, akasema, “Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania.” Papo hapo dada yake yule mtoto akajitokeza, akamwambia binti Farao, “Je, niende nikakutafutie yaya miongoni mwa wanawake wa Kiebrania akulelee mtoto huyu?” Binti Farao akamwambia, “Naam; nenda.” Basi, huyo msichana akaenda, akamwita mama yake huyo mtoto. Binti Farao akamwambia huyo mama, “Mtunze mtoto huyu, umlee kwa niaba yangu, nami nitakulipa mshahara wako.” Basi, huyo mama akamchukua mtoto, akamlea. Mtoto alipokuwa mkubwa kiasi, mama yake akampeleka kwa binti Farao, naye akamchukua na kumfanya mwanawe. Binti Farao akasema, “Nimemtoa majini,” kwa hiyo akampa mtoto huyo jina Mose. Siku moja, Mose alipokuwa mtu mzima, aliwaendea Waebrania wenzake ili kujionea taabu zao. Basi, akamwona Mmisri mmoja anampiga Mwebrania, mmoja wa ndugu zake Mose. Mose akatazama huku na huko, na alipoona kwamba hakuna mtu karibu, alimuua yule Mmisri na kumficha mchangani. Kesho yake, Mose alitoka tena, akaona Waebrania wawili wanapigana. Basi, akamwuliza yule aliyekosea, “Kwa nini unampiga mwenzako?” Naye akamjibu, “Nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi wetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Hivyo, Mose aliogopa na kufikiri, “Bila shaka jambo hilo limejulikana!” Naye Farao aliposikia juu ya tukio hilo akakusudia kumuua Mose. Lakini Mose alimkimbia Farao, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani. Siku moja, Mose alikuwa ameketi kando ya kisima cha maji. Basi, binti saba wa kuhani mmoja wa huko Midiani walifika kuchota maji na kuwanywesha kondoo na mbuzi wa baba yao. Wachungaji wengine wakaja na kuwafukuza hao binti. Lakini Mose akawasaidia binti hao na kuwanywesha wanyama wao. Walipomrudia baba yao Reueli, yeye akawauliza, “Mbona leo mmerudi upesi hivyo?” Nao wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa mikononi mwa wale wachungaji, naye mwenyewe akachota maji na kuwanywesha wanyama wetu.” Baba yao akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha huko? Mwiteni aje ale chakula.” Mose akakubali kukaa kwa huyo mtu. Basi, huyo mtu akampa Mose binti yake aitwaye Zipora awe mke wake. Zipora akamzalia mtoto wa kiume. Mose akasema, “Nimekimbilia katika nchi ya kigeni”, kwa hiyo akampa huyo mtoto jina Gershomu. Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakapiga kite na kulia kutokana na hali yao ya utumwa, na kilio chao kikamfikia Mungu juu. Mungu akasikia kilio chao, naye akakumbuka agano alilofanya na Abrahamu, na Isaka na Yakobo. Mungu aliwaangalia Waisraeli, akaona kuwa hali yao ni mbaya.
Kutoka 2:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaenda akaoa binti mmoja wa Lawi. Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akamtengenezea kikapu cha mafunjo akakitaliza kwa sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka kwenye nyasi kando ya mto. Dada yake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata. Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kikapu katika nyasi, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta. Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. Basi dada yake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu? Binti Farao akamwambia, Haya! Nenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto. Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa. Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. Basi akatazama huku na huko, na alipoona ya kuwa hapakuwapo mtu, akampiga na kumwua Mmisri yule, akamfukia mchangani. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako? Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana. Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia kutoka kwa Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima. Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao. Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao. Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo? Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi. Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula. Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora. Huyo akamzalia mtoto wa kiume, akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni. Na kisha baada ya muda, yule mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa Mungu kwa sababu ya ule utumwa. Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Abrahamu na Isaka na Yakobo. Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.
Kutoka 2:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi. Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akampatia kisafina cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto. Umbu lake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata. Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta. Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu? Binti Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto. Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini. Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani ya mchanga. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako? Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana. Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima. Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao. Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao. Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo? Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi. Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula. Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora. Huyo akamzalia mwana, akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni. Hata baada ya siku zile nyingi mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa Mungu kwa sababu ya ule utumwa. Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo. Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.
Kutoka 2:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaoa mwanamke Mlawi, naye mwanamke huyo akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume. Alipoona mtoto huyo ni mzuri, akamficha kwa miezi mitatu. Lakini alipoona hawezi kuendelea kumficha, akamtengenezea kisafina cha mafunjo, akakipaka lami. Kisha akamweka huyo mtoto ndani yake, akakificha kwenye matete kando ya ukingo wa Mto Naili. Dada ya huyo mtoto akasimama mbali ili kuona kitakachompata mtoto. Ndipo binti Farao akateremka kwenye Mto Naili kuoga, nao wahudumu wake wakawa wanatembea ukingoni mwa mto. Binti Farao akaona kisafina kwenye matete, akamtuma mmoja wa wajakazi wake kukichukua. Alifungua kisafina akaona mtoto ndani yake. Mtoto alikuwa akilia, akamhurumia. Akasema, “Huyu ni mmoja wa watoto wa Waebrania.” Ndipo dada wa huyo mtoto akamuuliza binti Farao, “Je, niende nikakutafutie mmoja wa wanawake wa Waebrania akulelee huyu mtoto?” Binti Farao akamjibu, “Ndiyo, nenda.” Yule msichana akaenda akamleta mama wa mtoto. Binti Farao akamwambia, “Mchukue huyu mtoto unisaidie kumlea, nami nitakulipa.” Basi yule mwanamke akamchukua mtoto na kumlea. Mtoto alipokua, akampeleka kwa binti Farao, naye akawa mwanawe. Akamwita jina Musa, akisema, “Nilimtoa kwenye maji.” Siku moja, Musa alipokuwa mtu mzima, alienda mahali walipokuwa ndugu zake, na akaona jinsi walivyokuwa wakifanyishwa kazi ngumu. Akamwona Mmisri akimpiga Mwebrania, mmoja wa watu wake. Musa akatazama huku na huko asione mtu yeyote, akamuua yule Mmisri, akamficha kwenye mchanga. Kesho yake akatoka, akaona Waebrania wawili wakipigana. Akamuuliza yule aliyekosa, “Mbona unampiga Mwebrania mwenzako?” Yule mtu akamjibu, “Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Ndipo Musa akaogopa na kuwaza, “Jambo lile nililofanya lazima limefahamika.” Farao aliposikia jambo hili, alijaribu kumuua Musa, lakini Musa akamkimbia Farao na kwenda kuishi katika nchi ya Midiani, akaketi kando ya kisima. Kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja kisimani ili kuchota maji na kujaza birika kwa ajili ya kunyweshea mifugo ya baba yao. Baadhi ya wachungaji wakaja wakawafukuza hao wasichana. Ndipo Musa akainuka, akawasaidia kunywesha mifugo yao. Wasichana hao waliporudi nyumbani, baba yao Reueli akawauliza, “Imekuwaje leo mmerudi mapema hivyo?” Wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa kutoka mikono ya wachungaji. Pia mtu huyo alituchotea maji na kunywesha mifugo.” Akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha? Mkaribisheni ale chakula.” Musa akakubali kukaa kwa huyo mtu, ambaye alimpa Musa binti yake aliyeitwa Sipora amwoe. Sipora alizaa mtoto wa kiume, naye Musa akamwita jina Gershomu, akisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.” Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakalia kwa huzuni katika utumwa wao, walilia na kilio chao cha kutaka msaada kwa ajili ya utumwa kikamfikia Mungu. Mungu akasikia kilio chao cha huzuni, akakumbuka agano alilofanya na Abrahamu pamoja na Isaka na Yakobo. Kwa hiyo Mungu akawaangalia Waisraeli na kuwahurumia.