Kutoka 2:1-14
Kutoka 2:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa Walawi aliyemwoa mwanamke mmoja ambaye pia alikuwa wa ukoo wa Walawi. Basi, mama huyu akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Alipoona kwamba mtoto huyo mchanga alikuwa mzuri, akamficha kwa muda wa miezi mitatu. Lakini kwa vile hakuweza kumficha zaidi ya muda huo, alitengeneza namna ya kikapu cha mafunjo, akakipaka namna ya lami, akamtia huyo mtoto ndani. Kisha akakiweka kikapu kando ya mto Nili kwenye majani. Dada yake huyo mtoto akajificha karibu na mahali hapo ili aone yatakayompata nduguye. Basi, binti Farao akashuka mtoni kuoga, na watumishi wake wakawa wanatembeatembea kandokando ya mto. Binti Farao akakiona kile kikapu katika majani, akamtuma mjakazi wake akichukue. Alipokifungua, alimwona yule mtoto mchanga, analia. Basi, akamwonea huruma, akasema, “Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania.” Papo hapo dada yake yule mtoto akajitokeza, akamwambia binti Farao, “Je, niende nikakutafutie yaya miongoni mwa wanawake wa Kiebrania akulelee mtoto huyu?” Binti Farao akamwambia, “Naam; nenda.” Basi, huyo msichana akaenda, akamwita mama yake huyo mtoto. Binti Farao akamwambia huyo mama, “Mtunze mtoto huyu, umlee kwa niaba yangu, nami nitakulipa mshahara wako.” Basi, huyo mama akamchukua mtoto, akamlea. Mtoto alipokuwa mkubwa kiasi, mama yake akampeleka kwa binti Farao, naye akamchukua na kumfanya mwanawe. Binti Farao akasema, “Nimemtoa majini,” kwa hiyo akampa mtoto huyo jina Mose. Siku moja, Mose alipokuwa mtu mzima, aliwaendea Waebrania wenzake ili kujionea taabu zao. Basi, akamwona Mmisri mmoja anampiga Mwebrania, mmoja wa ndugu zake Mose. Mose akatazama huku na huko, na alipoona kwamba hakuna mtu karibu, alimuua yule Mmisri na kumficha mchangani. Kesho yake, Mose alitoka tena, akaona Waebrania wawili wanapigana. Basi, akamwuliza yule aliyekosea, “Kwa nini unampiga mwenzako?” Naye akamjibu, “Nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi wetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Hivyo, Mose aliogopa na kufikiri, “Bila shaka jambo hilo limejulikana!”
Kutoka 2:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaenda akaoa binti mmoja wa Lawi. Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akamtengenezea kikapu cha mafunjo akakitaliza kwa sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka kwenye nyasi kando ya mto. Dada yake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata. Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kikapu katika nyasi, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta. Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. Basi dada yake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu? Binti Farao akamwambia, Haya! Nenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto. Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa. Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. Basi akatazama huku na huko, na alipoona ya kuwa hapakuwapo mtu, akampiga na kumwua Mmisri yule, akamfukia mchangani. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako? Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana.
Kutoka 2:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi. Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akampatia kisafina cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto. Umbu lake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata. Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta. Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu? Binti Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto. Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini. Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani ya mchanga. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako? Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana.
Kutoka 2:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaoa mwanamke Mlawi, naye mwanamke huyo akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume. Alipoona mtoto huyo ni mzuri, akamficha kwa miezi mitatu. Lakini alipoona hawezi kuendelea kumficha, akamtengenezea kisafina cha mafunjo, akakipaka lami. Kisha akamweka huyo mtoto ndani yake, akakificha kwenye matete kando ya ukingo wa Mto Naili. Dada ya huyo mtoto akasimama mbali ili kuona kitakachompata mtoto. Ndipo binti Farao akateremka kwenye Mto Naili kuoga, nao wahudumu wake wakawa wanatembea ukingoni mwa mto. Binti Farao akaona kisafina kwenye matete, akamtuma mmoja wa wajakazi wake kukichukua. Alifungua kisafina akaona mtoto ndani yake. Mtoto alikuwa akilia, akamhurumia. Akasema, “Huyu ni mmoja wa watoto wa Waebrania.” Ndipo dada wa huyo mtoto akamuuliza binti Farao, “Je, niende nikakutafutie mmoja wa wanawake wa Waebrania akulelee huyu mtoto?” Binti Farao akamjibu, “Ndiyo, nenda.” Yule msichana akaenda akamleta mama wa mtoto. Binti Farao akamwambia, “Mchukue huyu mtoto unisaidie kumlea, nami nitakulipa.” Basi yule mwanamke akamchukua mtoto na kumlea. Mtoto alipokua, akampeleka kwa binti Farao, naye akawa mwanawe. Akamwita jina Musa, akisema, “Nilimtoa kwenye maji.” Siku moja, Musa alipokuwa mtu mzima, alienda mahali walipokuwa ndugu zake, na akaona jinsi walivyokuwa wakifanyishwa kazi ngumu. Akamwona Mmisri akimpiga Mwebrania, mmoja wa watu wake. Musa akatazama huku na huko asione mtu yeyote, akamuua yule Mmisri, akamficha kwenye mchanga. Kesho yake akatoka, akaona Waebrania wawili wakipigana. Akamuuliza yule aliyekosa, “Mbona unampiga Mwebrania mwenzako?” Yule mtu akamjibu, “Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Ndipo Musa akaogopa na kuwaza, “Jambo lile nililofanya lazima limefahamika.”