Kutoka 19:14-25
Kutoka 19:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Mose akashuka mlimani na kuwaendea watu, akawatakasa, nao wakayafua mavazi yao. Kisha akawaambia watu wote, “Kesho kutwa muwe tayari, na mwanamume yeyote asimkaribie mwanamke.” Basi, siku ya tatu asubuhi, kukatokea ngurumo na umeme na wingu zito juu ya mlima. Ikasikika pia sauti kubwa ya mbiu ambayo iliwatetemesha watu wote kambini. Kisha Mose akawaongoza watu wote kutoka kambini, wakaenda kukutana na Mungu. Wote walikwenda wakajipanga chini ya mlima. Mlima wa Sinai ulikuwa umefunikwa na moshi kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alishuka juu yake katika moto. Moshi wa moto huo ulipanda juu kama moshi wa tanuri kubwa na mlima wote ulitetemeka kwa nguvu. Sauti ya mbiu ilizidi kuongezeka, na Mose akaongea na Mungu. Mungu naye akamjibu katika ngurumo. Mwenyezi-Mungu alishuka juu ya mlima Sinai, akamwita Mose kutoka huko juu, naye Mose akapanda mlimani. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Shuka chini ukawaonye watu wote wasije kunitazama; la sivyo wengi wao wataangamia. Hata makuhani ambao hunikaribia wanapaswa kujitakasa; la sivyo nitawaadhibu.” Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Watu hawa hawawezi kuupanda mlima wa Sinai kwani wewe mwenyewe ulituamuru tuweke mpaka kuuzunguka mlima.” Mwenyezi-Mungu akasema, “Teremka chini kisha urudi pamoja na Aroni. Lakini usiwaruhusu makuhani na watu wengine wapite mpaka na kuja kwangu, la sivyo nitawaadhibu.” Basi, Mose akashuka na kuwaambia Waisraeli mambo yote aliyoagizwa.
Kutoka 19:14-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Musa akateremka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao. Akawaambia watu; Muwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke. Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka. Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima. Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu BWANA alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuri, mlima wote ukatetemeka sana. Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti. BWANA akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; BWANA akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu. Ndipo BWANA akamwambia Musa, Shuka chini, uwaonye watu wasije wakafanya njia kuja kwa BWANA kutazama, kisha wengi miongoni mwao wakaangamia. Makuhani nao, wamkaribiao BWANA, na wajitakase, BWANA asije akawakasirikia. Musa akamwambia BWANA, Watu hawa hawawezi kuukaribia mlima wa Sinai; kwa kuwa wewe ulituusia, ukisema, Wekeni mipaka kandokando ya mlima, na kuutenga. BWANA akamwambia, Nenda, ushuke wewe; nawe utakwea, wewe, na Haruni pamoja nawe; lakini wale makuhani na watu wasipenye kumkaribia BWANA, asije yeye akawafurikia juu yao. Basi Musa akawateremkia hao watu na kuwaambia hayo.
Kutoka 19:14-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Musa akatelemka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao. Akawaambia watu; Mwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke. Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka. Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima. Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu BWANA alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana. Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti. BWANA akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; BWANA akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu. Ndipo BWANA akamwambia Musa, Shuka chini, uwaonye watu wasije wakapasua njia waje kwa BWANA kutazama, kisha wengi miongoni mwao wakaangamia. Makuhani nao, wamkaribiao BWANA, na wajitakase, BWANA asije akawafurikia. Musa akamwambia BWANA, Watu hawa hawawezi kuukaribia mlima wa Sinai; kwa kuwa wewe ulituusia, ukisema, Wekeni mipaka kando-kando ya mlima, na kuutenga. BWANA akamwambia, Nenda, ushuke wewe; nawe utakwea, wewe, na Haruni pamoja nawe; lakini wale makuhani na watu wasipenye kumkaribia BWANA, asije yeye akawafurikia juu yao. Basi Musa akawatelemkia hao watu na kuwaambia hayo.
Kutoka 19:14-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya Musa kushuka kutoka mlimani akawaendea watu na kuwaweka wakfu, wakafua nguo zao. Kisha akawaambia watu, “Jitayarisheni kwa ajili ya siku ya tatu. Mwanaume yeyote asimkaribie mwanamke.” Asubuhi ya siku ya tatu kulikuwa na ngurumo na radi pamoja na wingu nene juu ya mlima na mlio mkubwa sana wa tarumbeta. Kila mmoja aliyekuwa kambini akatetemeka. Kisha Musa akawaongoza watu kutoka kambini kukutana na Mungu, nao wakasimama chini ya mlima. Mlima Sinai ulikuwa umefunikwa na moshi, kwa sababu BWANA alishuka juu yake katika moto. Moshi wa moto huo ulipanda juu kama moshi kutoka tanuru kubwa, na mlima wote ukatetemeka kwa kishindo, nayo sauti ya tarumbeta ikawa kubwa zaidi na zaidi. Kisha Musa akazungumza, nayo sauti ya Mungu ikamjibu. BWANA akashuka juu ya Mlima Sinai na akamwita Musa apande juu mlimani. Kwa hiyo Musa akapanda juu, naye BWANA akamwambia Musa, “Shuka ukawaonye watu ili wasijipenyeze kutafuta kumwona BWANA, na wengi wao wakaangamia. Hata makuhani, watakaomkaribia BWANA ni lazima wajiweke wakfu, la sivyo BWANA atawaadhibu.” Musa akamwambia BWANA, “Watu hawawezi kupanda Mlima Sinai kwa sababu wewe mwenyewe ulituonya ukisema, ‘Wekeni mipaka kuuzunguka mlima na kuutenga kama patakatifu.’ ” BWANA akajibu, “Shuka ukamlete Haruni pamoja nawe. Lakini makuhani pamoja na watu wasije wakalazimisha kuja kwa BWANA, nisije nikawaadhibu.” Basi Musa akashuka kwa watu na kuwaambia lile aliloambiwa.