Kutoka 18:13-27
Kutoka 18:13-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Kesho yake, Mose aliketi kuamua matatizo ya Waisraeli, nao wakasimama wakiwa wamemzunguka, tangu asubuhi mpaka jioni. Yethro, baba mkwe wa Mose, alipoyaona mambo yote ambayo Mose aliwafanyia Waisraeli, alimwuliza, “Kwa nini unawafanyia watu mambo haya? Mbona unaketi peke yako huku watu wamekuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?” Mose akamjibu mkwewe, “Kwa sababu watu huja kwangu kuuliza matakwa ya Mungu. Wakiwa na ugomvi wowote ule wao huja kwangu nami huamua kati ya mtu na mwenzake, na kuwafunza amri za Mungu na maamuzi yake.” Basi, Yethro akamwambia Mose, “Unavyofanya si vizuri! Utajidhuru mwenyewe na hawa watu kwa uchovu, kwani hii ni kazi ngumu usiyoweza kuifanya peke yako. Sikiliza shauri langu kwako, na Mungu awe pamoja nawe. Wewe utawawakilisha watu mbele ya Mungu na kumletea Mungu matatizo yao. Hali kadhalika utawafundisha amri na maamuzi ya Mungu na kuwaonesha jinsi inavyowapasa kuishi na kufanya. Lakini kuhusu mambo mengine, chagua miongoni mwa watu wote, watu wanaostahili, watu wanaomcha Mungu, waaminifu na wanaochukia kuhongwa. Wape hao mamlaka, wawe na jukumu la kuwasimamia watu katika makundi ya watu elfu, mia, hamsini na kumikumi. Hao ndio watakaokuwa na vikao kila siku kutatua matatizo ya watu. Matatizo magumu watakuletea wewe, lakini yale madogomadogo watayaamua wenyewe. Kwa njia hiyo utaweza kurahisisha kazi yako kwa vile watashirikiana nawe katika jukumu hilo. Ukifanya hivyo, na kama ndivyo atakavyo Mungu, utaweza kustahimili na watu hawa wote wataweza kurudi makwao kwa amani.” Mose alilisikiliza shauri hilo la mkwewe na kufanya kama alivyoshauriwa. Basi, akawateua watu wenye uwezo kati ya Waisraeli, akawafanya kuwa viongozi wa makundi ya watu elfu, watu mia, watu hamsini na watu kumikumi. Nao wakawa wanaamua matatizo ya watu kila wakati. Matatizo magumu walimletea Mose, lakini yale madogomadogo waliyatatua wao wenyewe. Baada ya kufanya hivyo, Mose na mkwewe wakaagana naye Yethro akarudi nchini kwake.
Kutoka 18:13-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni. Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni? Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu; wakiwa na neno, hunijia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajulisha amri za Mungu, na sheria zake. Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. Kwa kweli utajidhoofisha mwenyewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako. Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao; nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya. Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mamia, na wakuu wa hamsini hamsini, na wakuu wa kumi kumi; nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe. Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani. Basi Musa akasikiza neno la mkwewe, akayafanya yote aliyokuwa amemwambia. Musa akawachagua watu wenye uwezo katika Israeli yote, akawaweka wawe vichwa juu ya watu, wakuu wa maelfu, na wakuu wa mamia, na wakuu wa hamsini hamsini, na wakuu wa kumi kumi. Nao wakawaamua watu sikuzote; mashauri magumu wakamletea Musa, lakini kila neno dogo wakaliamua wenyewe. Kisha Musa akaagana na mkwewe; naye akaenda zake, mpaka nchi yake mwenyewe.
Kutoka 18:13-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni. Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni? Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu; wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake. Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako. Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao; nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya. Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi; nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe. Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani. Basi Musa akasikiza neno la mkwewe, akayafanya yote aliyokuwa amemwambia. Musa akawachagua watu wenye uwezo katika Israeli yote, akawaweka wawe vichwa juu ya watu, wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi. Nao wakawaamua watu sikuzote; mashauri magumu wakamletea Musa, lakini kila neno dogo wakaliamua wenyewe. Kisha Musa akaagana na mkwewe; naye akaenda zake, mpaka nchi yake mwenyewe.
Kutoka 18:13-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku iliyofuata, Musa akachukua nafasi yake kama hakimu wa watu, nao wakasimama kumzunguka kuanzia asubuhi hadi jioni. Baba mkwe wake alipoona yote Musa anayowafanyia watu, akasema, “Ni nini hiki unachowafanyia watu? Kwa nini wewe unakuwa mwamuzi wa watu hawa peke yako, wakati watu hawa wamesimama wakikuzunguka tangu asubuhi hadi jioni?” Musa akamjibu, “Kwa sababu watu wananijia kutaka mapenzi ya Mungu. Kila wakiwa na shauri huletwa kwangu, nami huamua kati ya mtu na mwenzake, na kuwaeleza hukumu na sheria zake Mungu.” Baba mkwe wa Musa akamjibu, “Unachofanya sio kizuri. Wewe pamoja na watu hawa wanaokujia mtajichosha bure. Kazi ni nzito sana kwako, huwezi kuibeba mwenyewe. Sasa nisikilize mimi, nitakupa ushauri, naye Mungu na awe pamoja nawe. Yapasa wewe uwe mwakilishi wa watu mbele za Mungu na ulete mashauri yao kwake. Wafundishe hukumu na sheria zake, na uwaoneshe jinsi wanavyopaswa kuishi, na jinsi wanavyopaswa kuenenda. Lakini uchague watu wenye uwezo miongoni mwa watu wote, watu wanaomwogopa Mungu, watu waaminifu wanaochukia mali ya dhuluma, uwateuwe wawe maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. Waweke wawe waamuzi wa watu kwa wakati wote, lakini waambie wakuletee kila shauri lililo gumu; yale yaliyo rahisi wayaamue wao wenyewe. Hii itafanya mzigo wako kuwa mwepesi, kwa sababu watashirikiana nawe. Ukifanya hivi, na ikiwa Mungu ameagiza hivyo, utaweza kushinda uchovu, nao watu hawa wote watarudi nyumbani wameridhika.” Musa akamsikiliza baba mkwe wake na kufanya kila kitu alichosema. Musa akawachagua watu wenye uwezo kutoka Israeli yote, akawafanya wawe viongozi wa watu, maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. Wakatumika kama waamuzi wa watu kwa wakati wote. Mashauri magumu wakayaleta kwa Musa, lakini yale yaliyo rahisi wakayaamua wenyewe. Kisha Musa akaagana na Yethro baba mkwe wake, naye akarudi kwa nchi yake.