Kutoka 16:13-18
Kutoka 16:13-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, mnamo wakati wa jioni kukaja kware wengi, wakafunika kambi ya Waisraeli. Asubuhi yake kukatokea umande, ukatanda kandokando ya kambi yao. Umande huo ulipotoweka, kukabaki huko nyikani kitu kama mkate mwembamba na mwepesi. Waisraeli walipoona kitu hicho walishangaa, wakaulizana, “Nini hiki?” Hawakujua kilikuwa kitu gani. Basi, Mose akawaambia, “Huu ni mkate ambao Mwenyezi-Mungu amewapa mle. Mwenyezi-Mungu ameamuru mfanye hivi: Kila mtu na akusanye chakula kiasi anachoweza kula; ataokota kiasi cha pishi moja kwa kila mtu hemani mwake.” Basi, Waisraeli wakafanya hivyo, na ikawa kwamba, wengine waliokota kwa wingi na wengine kidogo. Lakini wote walipokipima kipimo walichookota katika pishi, waligundua kuwa aliyeokota kingi hakuwa na cha ziada, na aliyeokota kidogo, hakupungukiwa. Kila mmoja alikuwa ameokota kiasi alichoweza kula.
Kutoka 16:13-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa wakati wa jioni, kware wakaja, wakaifunikiza kambi; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo. Na ulipokauka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama barafu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa ninyi, mle. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kila mtu pishi moja kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake. Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua. Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa.
Kutoka 16:13-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa wakati wa jioni, kware wakakaribia, wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo. Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa ninyi, mle. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake. Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua. Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa.
Kutoka 16:13-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na utando wa umande kuzunguka kambi. Umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya mchanga wa jangwa. Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani. Musa akawaambia, “Huu ndio mkate ambao BWANA amewapa mle. Hivi ndivyo BWANA ameamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi moja kwa kila mtu mliye naye katika hema lenu.’ ” Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa; baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu. Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji.