Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 15:1-18

Kutoka 15:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Hapo, Mose pamoja na Waisraeli wakamwimbia Mwenyezi-Mungu wimbo huu, “Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu kwani ameshinda kwa fahari, farasi na mpandafarasi wake amewatosa baharini. Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu na uwezo, yeye mwenyewe ndiye anayeniokoa. Yeye ni Mungu wangu nami nitamsifu, ni Mungu wa baba yangu nami nitamtukuza. Mwenyezi-Mungu ni shujaa vitani; Mwenyezi-Mungu ndilo jina lake. “Magari na majeshi ya Farao ameyatumbukiza baharini, maofisa wake wateule wamezama katika bahari ya Shamu. Vilindi vya maji vimewafunika, wameporomoka baharini kama jiwe. “Mkono wako wa kulia ee Mwenyezi-Mungu watukuka kwa nguvu; kwa mkono wako wa kulia ee Mwenyezi-Mungu wawaponda adui. Kwa wingi wa ukuu wako wawaangamiza wapinzani wako; wawapulizia ghadhabu yako nayo yawateketeza kama makapi. Kwa pumzi ya pua yako maji yalirundikana, mawimbi yakasimama wima kama ukuta; vilindi katikati ya bahari vikagandamana. Adui alijisemea, ‘Nitawafuata na kuwakamata; nitagawanya nyara mpaka hamu yangu iishe. Tutaufuta upanga wetu, tutawaangamiza kwa mkono wetu.’ Lakini wewe uliuvumisha upepo wako, nayo bahari ikawafunika. Walizama majini kama risasi. “Ewe Mwenyezi-Mungu, ni nani kati ya miungu anayelingana nawe? Ni nani aliye kama wewe uliye mtakatifu mkuu, utishaye kwa matendo matukufu, unayetenda mambo ya ajabu? Uliunyosha mkono wako wa kulia, nayo nchi ikawameza maadui zetu. “Kwa fadhili zako kuu umewaongoza watu uliowakomboa, kwa nguvu yako umewaongoza kwenye makao yako matakatifu. Watu wa mataifa wamesikia hayo wakatetemeka; wakazi wa Filistia wamekumbwa na kitisho. Wakuu wa Edomu wamefadhaishwa; viongozi wa Moabu wamekumbwa na woga mkuu; wakazi wote wa Kanaani wamevunjika moyo. Kitisho na hofu vimewavamia. Kwa sababu ya ukuu wa nguvu zako, wao wamenyamaza kimya kama jiwe, mpaka watu wako ee Mwenyezi-Mungu, wapite, naam, mpaka watu hao uliowakomboa wamewapita. Wewe utawaleta watu wako na kuwapanda mlimani pako; pale ulipochagua ee Mwenyezi-Mungu pawe makao yako, mahali patakatifu ee Mwenyezi-Mungu ulipojenga kwa mikono yako. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, watawala milele na milele.”

Shirikisha
Soma Kutoka 15

Kutoka 15:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia BWANA wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia BWANA, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza. BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake. Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, Maofisa wake wateule wamezama katika Bahari ya Shamu. Vilindi vimewafunikiza, Walizama vilindini kama jiwe. BWANA, mkono wako wa kulia umepata fahari ya uwezo, BWANA, mkono wako wa kulia wawasetaseta adui. Kwa wingi wa ukuu wako wawaangusha chini wanaokupinga, Huwatumia hasira yako nayo huwateketeza kama mabua makavu. Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa, Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa kilima, Vilindi vikagandamana katikati ya bahari. Adui akasema, Nitafuata, nitapata, nitagawanya nyara, Nafsi yangu itashibishwa na wao; Nitaufuta upanga wangu, mkono wangu utawaangamiza. Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza; Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu. Ee BWANA, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu? Ulinyosha mkono wako wa kulia, Nchi ikawameza. Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa, Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu. Makabila ya watu wamesikia, wanatetemeka, Wakazi wa Ufilisti uchungu umewashika. Ndipo majumbe wa Edomu wakashangaa, Watu wa Moabu wenye nguvu tetemeko limewapata, Watu wote wakaao Kanaani wameyeyuka. Hofu na woga zimewaangukia; Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe; Hata watakapovuka watu wako, Ee BWANA, Hata watakapovuka watu wako uliowanunua. Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee BWANA, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, BWANA, kwa mikono yako. BWANA atatawala milele na milele.

Shirikisha
Soma Kutoka 15

Kutoka 15:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia BWANA wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia BWANA, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza. BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake. Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu. Vilindi vimewafunikiza, Walizama vilindini kama jiwe. BWANA, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo, BWANA, mkono wako wa kuume wawaseta-seta adui. Kwa wingi wa ukuu wako wawaangusha chini wanaokuondokea, Wapeleka hasira yako, nayo huwateketeza kama mabua makavu. Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa, Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa chungu, Vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari. Adui akasema, Nitafuatia, nitapata, nitagawanya nyara, Nafsi yangu itashibishwa na wao; Nitaufuta upanga wangu, mkono wangu utawaangamiza. Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza; Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu. Ee BWANA, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu? Ulinyosha mkono wako wa kuume, Nchi ikawameza. Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa, Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu. Kabila za watu wamesikia, wanatetemeka, Wakaao Ufilisti utungu umewashika. Ndipo majumbe wa Edomu wakashangaa, Watu wa Moabu wenye nguvu tetemeko limewapata, Watu wote wakaao Kanaani wameyeyuka. Hofu na woga umewaangukia; Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe; Hata watakapovuka watu wako, Ee BWANA, Hata watakapovuka watu wako uliowanunua. Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee BWANA, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, BWANA, kwa mikono yako. BWANA atatawala milele na milele.

Shirikisha
Soma Kutoka 15

Kutoka 15:1-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ndipo Musa na Waisraeli wakamwimbia BWANA wimbo huu: “Nitamwimbia BWANA, kwa kuwa ametukuzwa sana. Farasi na mpanda farasi amewatosa baharini. “BWANA ni nguvu zangu na wimbo wangu; amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu, Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza. BWANA ni shujaa wa vita; BWANA ndilo jina lake. Magari ya vita ya Farao na jeshi lake amewatosa baharini. Maafisa wa Farao walio bora sana wamezamishwa katika Bahari ya Shamu. Maji yenye kina yamewafunika, wamezama vilindini kama jiwe. Mkono wako wa kuume, Ee BWANA ulitukuka kwa uweza. Mkono wako wa kuume, Ee BWANA, ukamponda adui. “Katika ukuu wa utukufu wako, ukawaangusha chini wale waliokupinga. Uliachia hasira yako kali, ikawateketeza kama kapi. Kwa pumzi ya pua yako maji yalijilundika. Mawimbi ya maji yakasimama imara kama ukuta, vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari. Adui alijivuna, ‘Nitawafuatia, nitawapata. Nitagawanya nyara; nitajishibisha kwao. Nitafuta upanga wangu na mkono wangu utawaangamiza.’ Lakini ulipuliza kwa pumzi yako, bahari ikawafunika. Wakazama kama risasi kwenye maji makuu. Ni nani miongoni mwa miungu aliye kama wewe, Ee BWANA? Ni nani kama Wewe: uliyetukuka katika utakatifu, utishaye katika utukufu, ukitenda maajabu? “Uliunyoosha mkono wako wa kuume na nchi ikawameza. Katika upendo wako usiokoma utawaongoza watu uliowakomboa. Katika nguvu zako utawaongoza hadi makao yako matakatifu. Mataifa watasikia na kutetemeka, uchungu utawakamata Wafilisti. Wakuu wa Edomu wataogopa, viongozi wa Moabu watatetemeka kwa hofu, Wakanaani watayeyuka, vitisho na hofu vitawaangukia. Kwa nguvu ya mkono wako watatulia kama jiwe, hadi watu wako wapite, Ee BWANA, hadi watu uliowanunua wapite. Utawaingiza na kuwapandikiza juu ya mlima wa urithi wako: hapo mahali, Ee BWANA, ulipopafanya kuwa makao yako, mahali patakatifu, Ee BWANA, ulipopajenga kwa mikono yako. “BWANA atatawala milele na milele.”

Shirikisha
Soma Kutoka 15