Kutoka 14:13-22
Kutoka 14:13-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Mose akawaambia Waisraeli, “Msiogope! Kaeni imara! Leo mtaona jinsi Mwenyezi-Mungu atakavyowaokoa. Maana, hawa Wamisri mnaowaona leo, hamtawaona tena. Mwenyezi-Mungu atawapigania; nyinyi mnachotakiwa kufanya ni kutulia tu.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa nini mnanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele. Inua fimbo yako na kuinyosha juu ya bahari. Maji yatagawanyika na Waisraeli wataweza kuvuka katikati ya bahari mahali pakavu. Mimi nitawafanya Wamisri kuwa wakaidi, nao watawafuatia katikati ya bahari; nami nitajipatia utukufu kutokana na kuangamizwa kwa Farao na jeshi lake, magari yake ya vita pamoja na wapandafarasi wake. Naam, nitatukuka kwa kumwangamiza Farao na jeshi lake, pamoja na magari yake na wapandafarasi; nao Wamisri watajua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, malaika wa Mungu aliyekuwa mbele ya kundi la Waisraeli aliondoka akakaa nyuma yao. Na ule mnara wa wingu pia uliondoka mbele ukasimama nyuma yao, ukakaa katikati ya Waisraeli na Wamisri. Lile wingu likawatia Wamisri giza, lakini likawaangazia Waisraeli usiku. Kwa hiyo, makundi hayo mawili, jeshi la Farao na kundi la Waisraeli, hayakukaribiana usiku kucha. Mose akaunyosha mkono wake juu ya bahari, naye Mwenyezi-Mungu akaisukuma bahari nyuma kwa upepo mkali toka mashariki. Upepo huo ulivuma usiku kucha, ukaigawa bahari sehemu mbili na katikati kukatokeza nchi kavu. Waisraeli wakapita katikati ya bahari mahali pakavu, kuta za maji zikiwa upande wao wa kulia na wa kushoto.
Kutoka 14:13-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya. BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi wake. Kisha malaika wa Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akaenda nyuma yao; na ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao, ikasimama nyuma yao; ikawa katikati ya jeshi la Misri na jeshi la Israeli; napo palikuwa na lile wingu na lile giza, lakini lilitoa nuru wakati wa usiku; na hawa hawakuwakaribia hawa usiku kucha. Musa; akanyosha mkono wake juu ya bahari; BWANA akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika. Wana wa Israeli wakaenda ndani wakipita kwenye nchi kavu ndani ya bahari; huku maji yakiwa ukuta kwao mkono wa kulia na mkono wa kushoto.
Kutoka 14:13-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya. BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi zake. Kisha malaika wa Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akaenda nyuma yao; na ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao, ikasimama nyuma yao; ikafika kati ya jeshi la Misri na jeshi la Israeli; napo palikuwa na lile wingu na lile giza, lakini lilitoa nuru wakati wa usiku; na hawa hawakuwakaribia hawa usiku kucha. Musa; akanyosha mkono wake juu ya bahari; BWANA akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika. Wana wa Israeli wakaenda ndani kati ya bahari katika nchi kavu; nayo maji yalikuwa ukuta kwao mkono wa kuume, na mkono wa kushoto.
Kutoka 14:13-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Musa akawajibu Waisraeli, “Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovu BWANA atakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu.” Ndipo BWANA akamwambia Musa, “Kwa nini wewe unanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele. Inua fimbo yako na unyooshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, ili Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini. Nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake. Nao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimi BWANA nitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.” Ndipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma, ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha. Ndipo Musa akanyoosha mkono wake juu ya bahari, naye BWANA akayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika, nao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.