Kutoka 12:3-10
Kutoka 12:3-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Iambieni jumuiya yote ya Waisraeli kwamba mnamo siku ya kumi ya mwezi huu, mtachukua mwanakondoo mmoja kwa kila jamaa moja. Kama jamaa moja ni ndogo mno hata isiweze kumaliza kondoo mmoja, itashirikiana na jamaa jirani kadiri ya idadi ya watu wake; kisha watachagua mnyama ambaye kila mtu ataweza kula. Mwanakondoo huyo asiwe na kilema chochote, awe wa kiume na wa mwaka mmoja. Anaweza kuwa mwanakondoo au mwanambuzi. Mtamweka mnyama huyo mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi huu. Siku hiyo, jumuiya yote ya Waisraeli watawachinja wanyama hao wakati wa jioni. Kisha, watachukua damu ya hao wanyama na kupaka kwenye miimo na vizingiti vya kila nyumba watakamolia wanyama hao. Wataila nyama hiyo usiku huohuo baada ya kuichoma; wataila pamoja na mkate usiotiwa chachu na mboga chungu za majani. Imekatazwa kuila ikiwa mbichi au imechemshwa kwa maji, bali lazima ichomwe yote, pamoja na kichwa, miguu na nyama zake za ndani. Hali kadhalika msibakize nyama yoyote mpaka asubuhi. Nyama yoyote itakayobaki hadi asubuhi mtaiteketeza motoni.
Kutoka 12:3-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Waambieni mkutano wote, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana dosari, wa kiume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani. Wala msisaze kitu chake chochote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto.
Kutoka 12:3-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani. Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto.
Kutoka 12:3-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Iambie jumuiya yote ya Israeli kwamba katika siku ya kumi ya mwezi huu, kila mtu atatwaa mwana-kondoo mmoja kwa ajili ya jamaa yake, mmoja kwa kila nyumba. Ikiwa nyumba yoyote ina watu wachache wasioweza kumaliza huyo mwana-kondoo mzima, nyumba hiyo itabidi ishirikiane na nyumba ya jirani wa karibu, baada ya kuzingatia idadi ya watu waliomo. Mtaangalia ni kiasi gani cha nyama kitahitajika kulingana na mahitaji ya kila mtu. Wanyama mtakaowachagua, lazima wawe wa kiume wa umri wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari, mwaweza kuwachukua kati ya kondoo au mbuzi. Tunzeni wanyama hao hadi siku ya kumi na nne ya mwezi, ambapo lazima watu wa jumuiya yote ya Israeli wachinje wanyama hao wakati wa jioni. Ndipo watakapochukua sehemu ya hiyo damu na kuipaka kwenye vizingiti vya juu, na miimo ya milango ya nyumba ambamo watakula wana-kondoo hao. Usiku huo huo watakula nyama iliyookwa kwenye moto, pamoja na mboga chungu za majani na mikate isiyotiwa chachu. Msile nyama mbichi wala iliyochemshwa, lakini iwe imeokwa kwenye moto, kichwa, miguu na nyama zake za ndani. Msibakize nyama yoyote hadi asubuhi; nazo kama zitabakia hadi asubuhi, lazima mziteketeze kwa moto.