Kutoka 12:21-28
Kutoka 12:21-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Mose akawaita wazee wote wa Waisraeli, akawaambia, “Chagueni kila mmoja wenu, kulingana na jamaa yake, mwanakondoo na kumchinja kwa sikukuu ya Pasaka. Mtachukua majani ya husopo na kuyachovya katika damu ndani ya birika na kupaka kwenye vizingiti na miimo yote miwili ya milango ya nyumba zenu. Mtu yeyote asitoke nje ya nyumba usiku huo hadi asubuhi. Maana mimi Mwenyezi-Mungu nitapita kuwaua Wamisri. Lakini nitakapoiona damu iliyopakwa kwenye vizingiti na miimo ya nyumba zenu, nitazipita na wala sitamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwaua. Shikeni jambo hilo nyinyi na wazawa wenu kama agizo la milele. Mtakapoingia katika nchi ile ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nitawapa, kama nilivyoahidi, ni lazima kulitekeleza. Kila wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Jambo hili lina maana gani?’ Nyinyi mtawajibu, ‘Hii ni tambiko ya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu alizipita nyumba za Waisraeli nchini Misri alipowaua Wamisri, lakini sisi hakutuua.’” Waisraeli wakainamisha vichwa na kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Kisha Waisraeli wakaenda, wakafanya kama walivyoambiwa na Mose na Aroni kulingana na amri ya Mwenyezi-Mungu.
Kutoka 12:21-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje kondoo wa Pasaka. Nanyi twaeni tawi la hisopo, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu yeyote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi. Kwa kuwa BWANA atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, BWANA atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mharibifu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi. Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa ni amri kwako na kwa wanao milele. Itakuwa hapo mtakapoifikia hiyo nchi, BWANA atakayowapa, kama alivyoahidi, ndipo mtakapoushika utumishi huu. Kisha itakuwa, hapo watoto wenu watakapowauliza, Ni nini maana yake utumishi huu kwenu? Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya Pasaka ya BWANA, kwa kuwa alipita juu ya nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa nyumba zetu. Hao watu wakainamisha vichwa na kusujudia. Basi wana wa Israeli wakaenda na kufanya mambo hayo; vile vile kama BWANA alivyowaamuru Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya.
Kutoka 12:21-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje pasaka. Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu ye yote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi. Kwa kuwa BWANA atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, BWANA atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi. Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa ni amri kwako na kwa wanao milele. Itakuwa hapo mtakapoifikilia hiyo nchi, BWANA atakayowapa, kama alivyoahidi, ndipo mtakapoushika utumishi huu. Kisha itakuwa, hapo watoto wenu watakapowauliza, N’nini maana yake utumishi huu kwenu? Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya pasaka ya BWANA, kwa kuwa alipita juu ya nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa nyumba zetu. Hao watu wakainama vichwa na kusujudia. Basi wana wa Israeli wakaenda na kufanya mambo hayo; vile vile kama BWANA alivyowaamuru Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya.
Kutoka 12:21-28 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Musa akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka. Chukueni kitawi cha hisopo, mkichovye kwenye damu iliyopo kwenye sinia, na kuipaka sehemu ya hiyo damu kwenye vizingiti, na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu yeyote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake hadi asubuhi. BWANA apitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi. “Shikeni maagizo haya yawe kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu. Mtakapoingia katika nchi BWANA atakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii. Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’ Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa BWANA, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri, na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo Waisraeli walisujudu na kuabudu. Waisraeli wakafanya kama vile BWANA alivyomwagiza Musa na Haruni.