Kutoka 12:1-6
Kutoka 12:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, walipokuwa bado nchini Misri, “Mwezi huu utakuwa kwenu mwezi wa kwanza wa mwaka. Iambieni jumuiya yote ya Waisraeli kwamba mnamo siku ya kumi ya mwezi huu, mtachukua mwanakondoo mmoja kwa kila jamaa moja. Kama jamaa moja ni ndogo mno hata isiweze kumaliza kondoo mmoja, itashirikiana na jamaa jirani kadiri ya idadi ya watu wake; kisha watachagua mnyama ambaye kila mtu ataweza kula. Mwanakondoo huyo asiwe na kilema chochote, awe wa kiume na wa mwaka mmoja. Anaweza kuwa mwanakondoo au mwanambuzi. Mtamweka mnyama huyo mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi huu. Siku hiyo, jumuiya yote ya Waisraeli watawachinja wanyama hao wakati wa jioni.
Kutoka 12:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. Waambieni mkutano wote, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana dosari, wa kiume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.
Kutoka 12:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.
Kutoka 12:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA akamwambia Musa na Haruni katika nchi ya Misri, “Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu, yaani mwezi wa kwanza wa mwaka wenu. Iambie jumuiya yote ya Israeli kwamba katika siku ya kumi ya mwezi huu, kila mtu atatwaa mwana-kondoo mmoja kwa ajili ya jamaa yake, mmoja kwa kila nyumba. Ikiwa nyumba yoyote ina watu wachache wasioweza kumaliza huyo mwana-kondoo mzima, nyumba hiyo itabidi ishirikiane na nyumba ya jirani wa karibu, baada ya kuzingatia idadi ya watu waliomo. Mtaangalia ni kiasi gani cha nyama kitahitajika kulingana na mahitaji ya kila mtu. Wanyama mtakaowachagua, lazima wawe wa kiume wa umri wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari, mwaweza kuwachukua kati ya kondoo au mbuzi. Tunzeni wanyama hao hadi siku ya kumi na nne ya mwezi, ambapo lazima watu wa jumuiya yote ya Israeli wachinje wanyama hao wakati wa jioni.