Kutoka 10:1-29
Kutoka 10:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao. Mimi nimemfanya kuwa mkaidi na maofisa wake ili nipate kutenda ishara hizi miongoni mwao, ili nyinyi mpate kuwasimulia watoto wenu na wajukuu wenu, jinsi nilivyowadhihaki Wamisri kwa kuzifanya ishara hizo miongoni mwao. Hivyo mtatambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mose na Aroni wakamwendea Farao na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, anasema hivi, ‘Mpaka lini utakataa kujinyenyekesha mbele yangu? Waache watu wangu waondoke ili wapate kunitumikia. Ukikataa kuwaacha watu wangu waondoke, basi, kesho nitaleta nzige waivamie nchi yako. Nchi yote ya Misri itakuwa giza kwa sababu ya nzige hao. Watakula kila kitu kilichosalimika baada ya ile mvua ya mawe; pia hawataacha chochote juu ya miti inayoota mashambani. Nzige hao watajaa katika nyumba zako, nyumba za maofisa wako na za Wamisri wote; watakuwa wengi kiasi ambacho hata wazee wenu hawajapata kuona tangu walipozaliwa, hadi leo.’” Basi, Mose akatoka kwa Farao. Viongozi wa Farao wakamwuliza, “Je, mtu huyu atatusumbua mpaka lini? Waache watu hawa waende zao wakamtumikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Je, hujali kwamba nchi ya Misri inaangamia?” Hapo, Mose na Aroni wakaitwa warudi kwa Farao, naye akawaambia, “Nendeni mkamtumikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Lakini, nauliza: Ni kina nani watakaokwenda pamoja nanyi?” Mose akamjibu, “Kila mtu: Vijana na wazee, tutaondoka na watoto wetu wa kiume na wa kike, kondoo na mbuzi wetu na ng'ombe; kwa maana ni lazima tumfanyie sikukuu Mwenyezi-Mungu.” Kwa kuwapuuza, Farao akawaambia, “Ehe! Mwenyezi-Mungu awe nanyi kama nitawaruhusu kamwe mwende zenu na watoto wenu. Ni dhahiri kwamba mnayo nia mbaya moyoni mwenu. La hasha! Ni wanaume tu watakaokwenda kumtumikia Mwenyezi-Mungu, maana hilo ndilo mnalotaka.” Hapo Mose na Aroni wakafukuzwa mbele ya Farao. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri, nzige watokee ili waingie na kula mimea yote nchini na vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe.” Basi, Mose akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri. Mwenyezi-Mungu akaleta upepo toka mashariki, ukavuma juu ya nchi mchana kutwa na usiku kucha. Kulipokucha, ule upepo ukawa umeleta nzige. Hao nzige wakaenea kila mahali nchini Misri, wakatua juu ya ardhi yote. Nzige hao walikuwa kundi kubwa kupindukia, kiasi ambacho hakijapata kutokea wala hakitatokea tena. Waliifunika nchi yote ya Misri, hata ardhi ikaonekana kuwa giza. Walikula mimea yote na matunda yote yaliyosalia wakati wa ile mvua ya mawe. Hakuna hata jani moja lililosalia nchini. Hakuna jani lolote lililosalia juu ya miti wala mimea popote katika nchi yote ya Misri. Hapo Farao akawaita Mose na Aroni kwa haraka, akawaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na dhidi yenu. Kwa hiyo sasa ninawasihi mnisamehe dhambi yangu, mara hii moja tu, mkaniombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki.” Basi, Mose akaondoka kwa Farao, akaenda kumwomba Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu akaleta upepo mkali toka magharibi, ukawainua wale nzige na kuwasukumia kwenye bahari ya Shamu. Hakuna hata nzige mmoja aliyebaki katika nchi nzima ya Misri. Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, naye hakuwaachia Waisraeli waondoke. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu mbinguni ili giza nene litokee nchini Misri, giza nene ambalo mtu ataweza kulipapasa.” Basi, Mose akanyosha mkono wake juu mbinguni, kukawa na giza nene kote nchini Misri kwa muda wa siku tatu. Watu hawakuweza kuonana wala kuondoka mahali walipokuwa kwa muda huo wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga huko Gosheni walimokuwa wanakaa. Kisha, Farao akamwita Mose, akamwambia, “Nendeni mkamtumikie Mwenyezi-Mungu. Watoto wenu pia wanaweza kwenda pamoja nanyi. Lakini kondoo na mbuzi, na ng'ombe wenu wabaki.” Lakini Mose akamwambia, “Ni lazima uturuhusu kuchukua wanyama wa tambiko na sadaka za kuteketezwa ili tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Ngombe wetu ni lazima pia tuwachukue wala hakuna hata ukwato mmoja utakaobaki nyuma, kwa sababu kutoka katika mifugo yetu wenyewe, tutamtumikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wala sisi hatujui ni mnyama yupi tutakayemtolea Mwenyezi-Mungu tambiko mpaka tutakapofika huko.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, akakataa kuwaachia Waisraeli waondoke. Farao akamwambia Mose, “Toka mbele yangu. Jihadhari sana. Usije kuniona tena, maana siku utakapokuja tena mbele yangu, utakufa!” Mose naye akamwambia, “Sawa! Kama ulivyosema sitakuja kukuona tena.”
Kutoka 10:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Musa, Ingia wewe kwa Farao; kwa kuwa mimi nimeufanya moyo wake mzito, nipate kuzionesha ishara zangu hizi kati yao; nawe upate kusema masikioni mwa mwanao, na masikioni mwa mjukuu wako, ni mambo gani niliyotenda juu ya Misri, na ishara zangu nilizozifanya kati yao; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, na kumwambia, BWANA, Mungu wa Waebrania, asema hivi, Je! Utakataa hata lini kujinyenyekeza mbele zangu? Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie. Au, kwamba wakataa kuwapa hao watu wangu ruhusa waende zao, tazama, kesho nitaleta nzige waingie ndani ya mipaka yako; nao wataufunika uso wa nchi, mtu asipate kuona hiyo nchi; nao watakula mabaki ya hayo yaliyopona yaliyowasalia baada ya ile mvua ya mawe, watakula kila mti umeao kwa ajili yenu mashambani; na nyumba zako, na nyumba za watumishi wako, na nyumba za Wamisri wote zitajawa na nzige; mfano wake baba zako wala baba za baba zako hawakuona, tangu siku walipoanza kuwapo juu ya nchi hadi hivi leo. Basi akageuka na kutoka kwa Farao. Ndipo watumishi wa Farao wakamwambia, Mtu huyu atakuwa tanzi kwetu sisi hadi lini? Wape hawa watu ruhusa waende zao, wamtumikie BWANA, Mungu wao; hujatambua bado ya kuwa Misri imekwisha haribika? Musa na Haruni wakaletwa tena kwa Farao; naye akawaambia, Nendeni, mkamtumikie BWANA, Mungu wenu; lakini ni kina nani watakaokwenda? Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng'ombe zetu; kwa kuwa inatupasa kumfanyia BWANA sikukuu. Lakini akawaambia, Ehe, BWANA na awe pamoja nanyi, kama nitakavyowapa ruhusa kwenda zenu pamoja na watoto wenu; angalieni, kwa kuwa pana uovu huko mbele yenu. Sivyo; endeni ninyi mlio watu wazima, mkamtumikie BWANA; kwa kuwa ndilo jambo mtakalo. Nao walifukuzwa usoni pa Farao. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri kwa hao nzige, ili wakwee juu ya nchi ya Misri, waile mimea yote ya nchi, yaani, vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe. Basi Musa akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri, na BWANA akaleta upepo kutoka mashariki juu ya nchi, mchana kutwa, na usiku kucha; kulipopambazuka ule upepo wa mashariki ukawaleta nzige. Na hao nzige wakakwea juu ya nchi yote ya Misri, wakatua ndani ya mipaka yote ya Misri, walikuwa wabaya mno; hawajakuwapo nzige kama hao majira yoyote, wala baada yao hawatakuwa wengine jinsi hiyo. Kwa kuwa waliufunika uso wote wa nchi, hata nchi iliingia giza; wakala mimea yote ya nchi, na matunda yote ya miti yaliyosazwa na ile mvua ya mawe; hapakusalia hata jani moja, mti wala mmea wa mashamba, katika nchi yote ya Misri. Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni haraka; akasema, Nimemfanyia dhambi BWANA, Mungu wenu na ninyi pia. Basi sasa, nawasihi, nisameheni dhambi yangu mara hii moja tu, mkamwombe BWANA, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki tu. Akatoka kwa Farao, na kumwomba BWANA. BWANA akaugeuza upepo wa magharibi wenye nguvu nyingi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka katika Bahari ya Shamu; hakusalia hata nzige mmoja ndani ya mipaka yote ya Misri. Lakini BWANA akaufanya ule moyo wa Farao uwe mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa waende zao. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, kuwe giza juu ya nchi ya Misri, watu wapapasepapase gizani. Basi Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; kukawa na giza nene katika nchi yote ya Misri muda wa siku tatu; hawakupata kuonana mtu na mwenziwe, wala hakuondoka mtu mahali alipokuwa muda wa siku tatu; lakini wana wa Israeli wote walikuwa na mwanga makaoni mwao. Farao akamwita Musa, na kumwambia, Haya, nendeni, mkamtumikie BWANA; kondoo zenu na ng'ombe zenu tu na waachwe; watoto wenu nao na waende pamoja nanyi. Musa akasema, Ni lazima utupe mikononi mwetu na wanyama wa dhabihu na wa sadaka za kuteketezwa, ili tupate kumchinjia BWANA Mungu wetu dhabihu. Makundi yetu pia watakwenda pamoja nasi; hautasalia nyuma hata ukwato mmoja; kwa maana inampasa kutwaa katika hao tupate kumtumikia BWANA, Mungu wetu; nasi hatujui, hata tutakapofika huko, ni kitu gani ambacho kwa hicho inatupasa kumtumikia BWANA. Lakini BWANA akaufanya kuwa mgumu moyo wa Farao, asikubali kuwapa ruhusa waende zao. Farao akamwambia Musa, Nenda zako, ujiangalie, usinione uso tena; kwani siku hiyo utakayoniangalia uso wangu utakufa. Musa akasema, Umenena vema; mimi sitakuangalia uso wako tena.
Kutoka 10:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Musa, Ingia wewe kwa Farao; kwa kuwa mimi nimeufanya moyo wake mzito, nipate kuzionyesha ishara zangu hizi kati yao; nawe upate kusema masikioni mwa mwanao, na masikioni mwa mjukuu wako, ni mambo gani niliyotenda juu ya Misri, na ishara zangu nilizozifanya kati yao; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, na kumwambia, BWANA, Mungu wa Waebrania, asema hivi, Je! Utakataa hata lini kujinyenyekeza mbele zangu? Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie. Au, kwamba wakataa kuwapa hao watu wangu ruhusa waende zao, tazama, kesho nitaleta nzige waingie ndani ya mipaka yako; nao wataufunika uso wa nchi, mtu asipate kuona hiyo nchi; nao watakula mabaki ya hayo yaliyopona yaliyowasalia baada ya ile mvua ya mawe, watakula kila mti umeao kwa ajili yenu mashambani; na nyumba zako, na nyumba za watumishi wako, na nyumba za Wamisri wote zitajawa na nzige; mfano wake baba zako wala baba za baba zako hawakuona, tangu siku walipoanza kuwapo juu ya nchi hata hivi leo. Basi akageuka na kutoka kwa Farao. Ndipo watumishi wa Farao wakamwambia, Mtu huyu atakuwa tanzi kwetu sisi hata lini? Wape hawa watu ruhusa waende zao, wamtumikie BWANA, Mungu wao; hujatambua bado ya kuwa Misri imekwisha haribika? Musa na Haruni wakaletwa tena kwa Farao; naye akawaambia, Nendeni, mkamtumikie BWANA, Mungu wenu; lakini ni kina nani watakaokwenda? Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng’ombe zetu; kwa kuwa inatupasa kumfanyia BWANA sikukuu. Lakini akawaambia, Ehe, BWANA na awe pamoja nanyi, kama nitakavyowapa ruhusa kwenda zenu pamoja na watoto wenu; angalieni, kwa kuwa pana uovu huko mbele yenu. Sivyo; endeni ninyi mlio watu wazima, mkamtumikie BWANA; kwa kuwa ndilo jambo mtakalo. Nao walifukuzwa usoni pa Farao. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri kwa hao nzige, ili wakwee juu ya nchi ya Misri, waile mimea yote ya nchi, yaani, vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe. Basi Musa akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri, na BWANA akaleta upepo kutoka mashariki juu ya nchi, mchana kutwa, na usiku kucha; kulipopambazuka ule upepo wa mashariki ukawaleta nzige. Na hao nzige wakakwea juu ya nchi yote ya Misri, wakatua ndani ya mipaka yote ya Misri, walikuwa wabaya mno; hawajakuwapo nzige kama hao majira yo yote, wala baada yao hawatakuwa wengine jinsi hiyo. Kwa kuwa waliufunika uso wote wa nchi, hata nchi iliingia giza; wakala mimea yote ya nchi, na matunda yote ya miti yaliyosazwa na ile mvua ya mawe; hapakusalia hata jani moja, mti wala mmea wa mashamba, katika nchi yote ya Misri. Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni haraka; akasema, Nimemfanyia dhambi BWANA, Mungu wenu na ninyi pia. Basi sasa, nawasihi, nisameheni dhambi yangu mara hii moja tu, mkamwombe BWANA, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki tu. Akatoka kwa Farao, na kumwomba BWANA. BWANA akaugeuza upepo wa magharibi wenye nguvu nyingi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka katika Bahari ya Shamu; hakusalia hata nzige mmoja ndani ya mipaka yote ya Misri. Lakini BWANA akaufanya ule moyo wa Farao uwe mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa waende zao. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, kuwe giza juu ya nchi ya Misri, watu wapapase-papase gizani. Basi Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; kukawa na giza nene katika nchi yote ya Misri muda wa siku tatu; hawakupata kuonana mtu na mwenziwe, wala hakuondoka mtu mahali alipokuwa muda wa siku tatu; lakini wana wa Israeli wote walikuwa na mwanga makaoni mwao. Farao akamwita Musa, na kumwambia, Haya, nendeni, mkamtumikie BWANA; kondoo zenu na ng’ombe zenu tu na waachwe; watoto wenu nao na waende pamoja nanyi. Musa akasema, Ni lazima utupe mikononi mwetu na wanyama wa dhabihu na wa sadaka za kuteketezwa, ili tupate kumchinjia BWANA Mungu wetu dhabihu. Makundi yetu pia watakwenda pamoja nasi; hautasalia nyuma hata ukwato mmoja; kwa maana inampasa kutwaa katika hao tupate kumtumikia BWANA, Mungu wetu; nasi hatujui, hata tutakapofika huko, ni kitu gani ambacho kwa hicho inatupasa kumtumikia BWANA. Lakini BWANA akaufanya kuwa mgumu moyo wa Farao, asikubali kuwapa ruhusa waende zao. Farao akamwambia Musa, Nenda zako, ujiangalie, usinione uso tena; kwani siku hiyo utakayoniangalia uso wangu utakufa. Musa akasema, Umenena vema; mimi sitakuangalia uso wako tena.
Kutoka 10:1-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo BWANA akamwambia Musa, “Nenda kwa Farao, kwa kuwa nimeufanya moyo wake kuwa mgumu na mioyo ya maafisa wake ili nipate kutenda ishara hizi zangu za ajabu miongoni mwao, ili upate kuwaeleza watoto wako na wajukuu wako jinsi nilivyowatendea Wamisri kwa ukali, na jinsi nilivyofanya ishara zangu miongoni mwao, nanyi mpate kujua kuwa Mimi ndimi BWANA.” Kwa hiyo Musa na Haruni wakaenda kwa Farao na kumwambia, “Hili ndilo BWANA, Mungu wa Waebrania, asemalo: ‘Utaendelea hata lini kukataa kunyenyekea mbele yangu? Waachie watu wangu waende, ili waniabudu. Ukikataa kuwaachia waende, kesho nitaleta nzige katika nchi yako. Nao watafunika uso wa ardhi hata usionekane. Watatafuna mabaki machache yaliyobakizwa baada ya ile mvua ya mawe, yaani pamoja na kila mti unaoota katika mashamba yenu. Nzige hao watajaza nyumba zako, za maafisa wako wote na za Wamisri wote. Jambo ambalo baba zenu wala babu zenu hawajapata kuona tangu siku ile walipoanza kuishi katika nchi hii hadi leo.’ ” Ndipo Musa akageuka na kumwacha Farao. Maafisa wa Farao wakamwambia, “Hadi lini huyu mtu atakuwa tanzi kwetu? Waachie hao watu waende zao, ili wapate kumwabudu BWANA Mungu wao. Je, bado hutambui kuwa Misri imeangamia?” Ndipo Musa na Haruni wakaletwa kwa Farao. Farao akawaambia, “Nendeni, mkamwabudu BWANA Mungu wenu. Lakini ni nani hasa watakaoenda?” Musa akajibu, “Tutaenda na vijana wetu na wazee, pamoja na wana wetu na binti zetu, pia pamoja na mbuzi, kondoo, na ngʼombe wetu kwa sababu tutaadhimisha sikukuu kwa BWANA.” Farao akasema, “Kama kweli nitawaruhusu mwondoke pamoja na wanawake wenu na watoto wenu, BWANA awe pamoja nanyi! Ni wazi kwamba mna makusudi mabaya. La hasha! Wanaume peke yao na waende, wakamwabudu BWANA, kwa kuwa hilo ndilo mmekuwa mkiomba.” Kwa hiyo Musa na Haruni wakaondolewa mbele ya Farao. Basi BWANA akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako juu ya Misri, ili kundi la nzige liweze kuvamia nchi na kutafuna kila kitu kinachoota katika mashamba na kila kitu kilichosazwa na ile mvua ya mawe.” Kwa hiyo Musa akanyoosha fimbo yake juu ya Misri, BWANA akauleta upepo wa mashariki ukavuma katika nchi yote mchana wote na usiku kucha, kufikia asubuhi upepo ukawa umeleta nzige. Wakaivamia Misri yote na kukaa katika kila eneo la nchi kwa wingi. Kamwe halijapata kutokea pigo la nzige kama hilo, wala halitakuwa tena. Wakafunika ardhi yote hata ardhi ikawa nyeusi. Wakatafuna kila kilichokuwa kimebakizwa na ile mvua ya mawe: kila kitu kilichoota shambani, pamoja na matunda kwenye miti. Hakuna kitu chochote cha kijani kilichosalia katika miti au mmea katika nchi yote ya Misri. Farao akawaita Musa na Haruni kwa haraka na kuwaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya BWANA Mungu wenu na dhidi yenu pia. Sasa unisamehe dhambi yangu mara moja tena na umwombe BWANA Mungu wako aondoe pigo hili baya kwangu.” Kisha Musa akaondoka kwa Farao akamwomba BWANA. Naye BWANA akaugeuza upepo kuwa upepo mkali sana kutoka magharibi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka kwenye Bahari ya Shamu. Hakuna nzige hata mmoja aliyebaki popote katika nchi ya Misri. Lakini BWANA akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke. Kisha BWANA akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili giza litande katika nchi ya Misri, giza ambalo watu wanaweza kulipapasa na kulihisi.” Kwa hiyo Musa akaunyoosha mkono wake kuelekea angani, na giza nene likafunika pote katika nchi ya Misri kwa muda wa siku tatu. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumwona mwenzake, wala kuondoka mahali alipokuwa kwa muda wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga katika maeneo waliyokuwa wanaishi. Ndipo Farao akamwita Musa na kusema, “Nendeni, mkamwabudu BWANA. Hata wanawake na watoto wenu mwaweza kwenda nao pia, lakini kondoo, mbuzi na ngʼombe wenu waacheni.” Lakini Musa akasema, “Huna budi kuturuhusu tuwe na dhabihu, na sadaka za kuteketezwa za kutoa mbele za BWANA Mungu wetu. Sisi ni lazima tuondoke na mifugo yetu pia, wala hakuna ukwato utakaoachwa nyuma. Inatupasa kutumia baadhi ya hiyo mifugo katika kumwabudu BWANA Mungu wetu, kwa kuwa hadi tutakapofika huko, hatutakuwa tumefahamu ni nini tutakachotumia katika kumwabudu BWANA.” Lakini BWANA akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, hakuwa radhi kuwaachia waondoke. Farao akamwambia Musa, “Ondoka mbele yangu! Hakikisha kuwa hutakuja mbele yangu tena! Siku ile utakapouona uso wangu utakufa.” Musa akamjibu, “Iwe kama ulivyosema! Kamwe sitauona uso wako tena.”