Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 1:8-21

Kutoka 1:8-21 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, akatokea mfalme mwingine huko Misri ambaye hakumjua Yosefu. Naye akawaambia watu wake, “Tazameni jinsi Waisraeli walivyo wengi na wenye nguvu kuliko sisi. Ni lazima tutafute hila ya kuwapunguza na kuzuia wasiongezeke; la sivyo, kama vita vikitokea watajiunga na adui zetu na kuitoroka nchi.” Basi, Wamisri wakawateua wanyapara wawasimamie Waisraeli na kuwatesa kwa kazi ngumu. Waisraeli wakafanya kazi ya kumjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kadiri walivyoteswa ndivyo Waisraeli walivyozidi kuongezeka na kuenea nchini. Hivyo Wamisri wakawaogopa sana watu wa Israeli. Basi, Wamisri wakawatumikisha Waisraeli kikatili, wakayafanya maisha yao kuwa magumu kwa kazi ngumu ya kutengeneza chokaa na kufyatua matofali, na kazi zote za shambani. Katika kazi hizo zote, Waisraeli walitumikishwa kwa ukatili. Kisha, mfalme wa Misri akawaambia wakunga wa Misri, Shifra na Pua, ambao waliwahudumia wanawake wa Kiebrania, “Mnapowahudumia wanawake wa Kiebrania wanapojifungua, ikiwa mtoto anayezaliwa ni wa kiume, muueni. Lakini ikiwa ni wa kike, mwacheni aishi.” Lakini kwa kuwa wakunga hao walimcha Mungu, hawakufanya kama walivyoamriwa na mfalme wa Misri, bali waliwaacha watoto wa kiume wa Waisraeli waishi. Basi, mfalme wa Misri akawaita wakunga hao, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivyo? Mbona mmewaacha watoto wa kiume waishi?” Wao wakamjibu Farao, “Wanawake wa Kiebrania si sawa na wanawake wa Misri. Wao ni hodari; kabla mkunga hajafika, wao huwa wamekwisha jifungua.” Basi, Mungu akawajalia mema wakunga hao, nao Waisraeli wakazidi kuongezeka na kuwa na nguvu sana. Na kwa vile wakunga hao walimcha Mungu, Mungu akawajalia kupata jamaa zao wenyewe.

Shirikisha
Soma Kutoka 1

Kutoka 1:8-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi akatokea mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii. Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Ndipo Wamisri wakaogopa kwa sababu ya wana wa Israeli. Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya maisha yao kuwa machungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali. Kisha mfalme wa Misri akawaambia wakunga wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua; akasema, Wakati mnapowazalisha wanawake wa Kiebrania na kuona kuwa ni mtoto wa kiume basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto wa kike, na aishi. Lakini hao wakunga walikuwa wacha Mungu, hawakufanya kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale watoto wa kiume. Basi mfalme wa Misri akawaita wale wakunga na kuwauliza, Kwa nini kufanya jambo hili la kuwahifadhi watoto wa kiume wawe hai? Wakunga wakamwambia Farao, Ni kwa sababu hao wanawake wa Kiebrania si kama wanawake wa Kimisri; kwa kuwa ni hodari hao, nao huzaa kabla mkunga hajapata kuwafikia. Basi Mungu akawatendea mema wale wakunga; na hao watu wakaongezeka sana, wakaendelea na kuzidi kuwa na nguvu nyingi. Ilikuwa kwa sababu wale wakunga walikuwa wakimcha Mungu, akawasimamishia nyumba.

Shirikisha
Soma Kutoka 1

Kutoka 1:8-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii. Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli. Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali. Kisha mfalme wa Misri akasema na wazalisha wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua; akasema, Wakati mwazalishapo wanawake wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume, basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto mwanamke, na aishi. Lakini wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale wanaume. Basi mfalme wa Misri akawaita wale wazalisha na kuwauliza, Kwa nini kufanya jambo hili, na kuwahifadhi watoto waume wawe hai? Wazalisha wakamwambia Farao, Ni kwa sababu hao wanawake wa Kiebrania si kama wanawake wa Kimisri; kwa kuwa ni hodari hao, nao huzaa kabla mzalisha hajapata kuwafikilia. Basi Mungu akawatendea mema wale wazalisha; na hao watu wakaongezeka sana, wakaendelea na kuzidi kuwa na nguvu nyingi. Ilikuwa kwa sababu wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, akawasimamishia nyumba.

Shirikisha
Soma Kutoka 1

Kutoka 1:8-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kisha mfalme mwingine ambaye hakufahamu habari za Yusufu akatawala Misri. Akawaambia watu wake, “Tazameni, Waisraeli wamekuwa wengi mno kwa idadi kuliko sisi. Njooni, ni lazima tuwashughulikie kwa uangalifu, la sivyo watazidi kuwa wengi zaidi, na ikiwa patatokea vita, watajiunga na adui zetu kupigana nasi, na kuondoka katika nchi hii.” Basi Wamisri wakaweka wasimamizi wa kuwasimamia na kuwatesa Waisraeli kwa kazi ngumu, nao wakajenga miji ya Pithomu na Ramesesi ya kuweka akiba ya Farao. Lakini walivyozidi kuteswa, ndivyo walivyozidi kuongezeka na kuenea katika nchi. Wamisri wakawaogopa Waisraeli, kwa hiyo wakawatumikisha kwa ukatili. Wakafanya maisha ya Waisraeli kuwa machungu kwa kufanya kazi ngumu ya kutengeneza lami na kufyatua matofali, na kazi zote za mashambani; katika kazi zao zote ngumu, Wamisri waliwatumia Waisraeli kwa ukatili. Mfalme wa Misri akawaita wakunga waliowazalisha Waebrania, ambao majina yao yalikuwa Shifra na Pua, akawaambia, “Mtakapowazalisha wanawake Waebrania, chunguzeni wanapojifungua. Ikiwa ni mtoto wa kiume, muueni; lakini ikiwa ni msichana, mwacheni aishi.” Lakini hao wakunga walimcha Mungu na hawakufanya kile mfalme wa Misri alichowaambia kufanya, bali wakawaacha watoto wa kiume waishi. Ndipo mfalme wa Misri akawaita hao wakunga, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivi? Mbona mmeacha watoto wa kiume waishi?” Wakunga wakamjibu Farao, “Wanawake wa Waebrania ni tofauti na wanawake wa Misri; wao wana nguvu, nao hujifungua watoto kabla wakunga hawajafika.” Kwa hiyo Mungu akawatendea mema wakunga hao. Waisraeli wakaongezeka na kuendelea kuwa wengi zaidi. Kwa vile hao wakunga walimcha Mungu, Mungu akawajalia kuwa na jamaa zao wenyewe.

Shirikisha
Soma Kutoka 1