Kutoka 1:8-14
Kutoka 1:8-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, akatokea mfalme mwingine huko Misri ambaye hakumjua Yosefu. Naye akawaambia watu wake, “Tazameni jinsi Waisraeli walivyo wengi na wenye nguvu kuliko sisi. Ni lazima tutafute hila ya kuwapunguza na kuzuia wasiongezeke; la sivyo, kama vita vikitokea watajiunga na adui zetu na kuitoroka nchi.” Basi, Wamisri wakawateua wanyapara wawasimamie Waisraeli na kuwatesa kwa kazi ngumu. Waisraeli wakafanya kazi ya kumjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kadiri walivyoteswa ndivyo Waisraeli walivyozidi kuongezeka na kuenea nchini. Hivyo Wamisri wakawaogopa sana watu wa Israeli. Basi, Wamisri wakawatumikisha Waisraeli kikatili, wakayafanya maisha yao kuwa magumu kwa kazi ngumu ya kutengeneza chokaa na kufyatua matofali, na kazi zote za shambani. Katika kazi hizo zote, Waisraeli walitumikishwa kwa ukatili.
Kutoka 1:8-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi akatokea mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii. Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Ndipo Wamisri wakaogopa kwa sababu ya wana wa Israeli. Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya maisha yao kuwa machungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali.
Kutoka 1:8-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii. Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli. Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali.
Kutoka 1:8-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha mfalme mwingine ambaye hakufahamu habari za Yusufu akatawala Misri. Akawaambia watu wake, “Tazameni, Waisraeli wamekuwa wengi mno kwa idadi kuliko sisi. Njooni, ni lazima tuwashughulikie kwa uangalifu, la sivyo watazidi kuwa wengi zaidi, na ikiwa patatokea vita, watajiunga na adui zetu kupigana nasi, na kuondoka katika nchi hii.” Basi Wamisri wakaweka wasimamizi wa kuwasimamia na kuwatesa Waisraeli kwa kazi ngumu, nao wakajenga miji ya Pithomu na Ramesesi ya kuweka akiba ya Farao. Lakini walivyozidi kuteswa, ndivyo walivyozidi kuongezeka na kuenea katika nchi. Wamisri wakawaogopa Waisraeli, kwa hiyo wakawatumikisha kwa ukatili. Wakafanya maisha ya Waisraeli kuwa machungu kwa kufanya kazi ngumu ya kutengeneza lami na kufyatua matofali, na kazi zote za mashambani; katika kazi zao zote ngumu, Wamisri waliwatumia Waisraeli kwa ukatili.