Kutoka 1:1-14
Kutoka 1:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Haya ndiyo majina ya watoto wa kiume wa Israeli, ambao walikwenda Misri, kila mmoja na jamaa yake: Reubeni, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Zebuluni, Benyamini, Dani, Naftali, Gadi na Asheri. Wazawa wote wa Yakobo walikuwa watu 70. Wakati huo Yosefu alikuwa amekwisha tangulia kukaa huko Misri. Baadaye, Yosefu alifariki, hali kadhalika ndugu zake na kizazi kile chote. Lakini wazawa wa Israeli waliongezeka sana, wakawa wengi na wenye nguvu mno, wakaenea kila mahali nchini Misri. Basi, akatokea mfalme mwingine huko Misri ambaye hakumjua Yosefu. Naye akawaambia watu wake, “Tazameni jinsi Waisraeli walivyo wengi na wenye nguvu kuliko sisi. Ni lazima tutafute hila ya kuwapunguza na kuzuia wasiongezeke; la sivyo, kama vita vikitokea watajiunga na adui zetu na kuitoroka nchi.” Basi, Wamisri wakawateua wanyapara wawasimamie Waisraeli na kuwatesa kwa kazi ngumu. Waisraeli wakafanya kazi ya kumjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kadiri walivyoteswa ndivyo Waisraeli walivyozidi kuongezeka na kuenea nchini. Hivyo Wamisri wakawaogopa sana watu wa Israeli. Basi, Wamisri wakawatumikisha Waisraeli kikatili, wakayafanya maisha yao kuwa magumu kwa kazi ngumu ya kutengeneza chokaa na kufyatua matofali, na kazi zote za shambani. Katika kazi hizo zote, Waisraeli walitumikishwa kwa ukatili.
Kutoka 1:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi majina ya wana wa Israeli walioingia Misri ni haya; kila mtu pamoja na jamaa zake walikuja pamoja na Yakobo. Reubeni, na Simeoni na Lawi, na Yuda; na Isakari, na Zabuloni, na Benyamini; na Dani, na Naftali, na Gadi, na Asheri. Na wale watu wote waliotokana na uzao wa Yakobo walikuwa watu sabini; na huyo Yusufu alikuwa huko ndani ya Misri tangu hapo. Yusufu akafa, na ndugu zake wote, na watu wote wa kizazi kile. Na wana wa Israeli walikuwa na uzazi sana, na kuongezeka mno, na kuzidi kuwa wengi, nao wakaendelea na kuongezeka nguvu; na ile nchi ilikuwa imejawa na wao. Basi akatokea mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii. Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Ndipo Wamisri wakaogopa kwa sababu ya wana wa Israeli. Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya maisha yao kuwa machungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali.
Kutoka 1:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi majina ya wana wa Israeli walioingia Misri ni haya; kila mtu pamoja na jamaa zake walikuja pamoja na Yakobo. Reubeni, na Simeoni na Lawi, na Yuda; na Isakari, na Zabuloni, na Benyamini; na Dani, na Naftali, na Gadi, na Asheri. Na nafsi zile zote zilizotoka viunoni mwa Yakobo zilikuwa ni nafsi sabini; na huyo Yusufu alikuwa huko ndani ya Misri tangu hapo. Yusufu akafa, na ndugu zake wote, na watu wote wa kizazi kile. Na wana wa Israeli walikuwa na uzazi sana, na kuongezeka mno, na kuzidi kuwa wengi, nao wakaendelea na kuongezeka nguvu; na ile nchi ilikuwa imejawa na wao. Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii. Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli. Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali.
Kutoka 1:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, kila mmoja na jamaa yake: Reubeni, Simeoni, Lawi na Yuda; Isakari, Zabuloni na Benyamini; Dani na Naftali, Gadi na Asheri. Wazao wote wa Yakobo walikuwa watu sabini; Yusufu alikuwa tayari yuko Misri. Basi Yusufu na kaka zake wote na kizazi kile chote walikufa, lakini Waisraeli walikuwa wamezaana na kuongezeka sana, idadi yao ikawa kubwa mno, hadi wakaijaza nchi. Kisha mfalme mwingine ambaye hakufahamu habari za Yusufu akatawala Misri. Akawaambia watu wake, “Tazameni, Waisraeli wamekuwa wengi mno kwa idadi kuliko sisi. Njooni, ni lazima tuwashughulikie kwa uangalifu, la sivyo watazidi kuwa wengi zaidi, na ikiwa patatokea vita, watajiunga na adui zetu kupigana nasi, na kuondoka katika nchi hii.” Basi Wamisri wakaweka wasimamizi wa kuwasimamia na kuwatesa Waisraeli kwa kazi ngumu, nao wakajenga miji ya Pithomu na Ramesesi ya kuweka akiba ya Farao. Lakini walivyozidi kuteswa, ndivyo walivyozidi kuongezeka na kuenea katika nchi. Wamisri wakawaogopa Waisraeli, kwa hiyo wakawatumikisha kwa ukatili. Wakafanya maisha ya Waisraeli kuwa machungu kwa kufanya kazi ngumu ya kutengeneza lami na kufyatua matofali, na kazi zote za mashambani; katika kazi zao zote ngumu, Wamisri waliwatumia Waisraeli kwa ukatili.