Esta 8:3-6
Esta 8:3-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Esta akazungumza tena na mfalme; akajitupa chini, miguuni pa mfalme, huku analia, akamsihi mfalme aukomeshe mpango mbaya ambao Hamani, wa uzao wa Agagi, alikuwa amepanga dhidi ya Wayahudi. Mfalme akamnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu, naye Esta akasimama na kusema, “Ukipenda, ewe mfalme, na kama unanijali na ukiona inafaa, tafadhali, toa tangazo la kufutilia mbali mipango ambayo Hamani alikuwa ameamuru itekelezwe. Mipango hiyo ni ile ya mwana wa Hamedatha, mzaliwa wa Agagi, aliyopanga ili kuwaangamiza Wayahudi wote katika mikoa yote. Maana, ninawezaje kuvumilia kuona watu wangu wanaangamizwa na jamaa zangu wanauawa?”
Esta 8:3-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena Esta akasema na mfalme mara ya pili, akaanguka miguuni pake, akamsihi kwa machozi ayaondoe madhara ya Hamani, Mwagagi, na shauri alilowafanyia Wayahudi. Ndipo mfalme alipomnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu. Basi Esta akaondoka, akasimama mbele ya mfalme. Akasema, Mfalme akiona vema, nami nikiwa nimepata kibali machoni pake, na neno likionekana jema mbele ya mfalme, nami nikimpendeza machoni pake, na iandikwe amri kuzitangua barua za Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuziandika ili kuwaangamiza Wayahudi walioko katika mikoa yote ya mfalme. Maana, ninawezaje kustahimili kuyaona mabaya yatakayowajia watu wangu? Au kuyatazama maangamizi ya jamaa zangu?
Esta 8:3-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena Esta akasema na mfalme mara ya pili, akaanguka miguuni pake, akamsihi kwa machozi ayaondoe madhara ya Hamani, Mwagagi, na shauri alilowafanyia Wayahudi. Ndipo mfalme alipomnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu. Basi Esta akaondoka, akasimama mbele ya mfalme. Akasema, Mfalme akiona vema, nami nikiwa nimepata kibali machoni pake, na neno likionekana jema mbele ya mfalme, nami nikimpendeza machoni pake, iandikwe kuzitangua barua za Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuziandika ili kuwaangamiza Wayahudi walioko katika majimbo yote ya mfalme. Kwa maana niwezeje kuyaona mabaya yatakayowajia watu wangu? Au niwezeje kuyatazama maangamizo ya jamaa zangu?
Esta 8:3-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Esta alimsihi tena mfalme, akianguka miguuni pake na kulia. Akamwomba akomeshe mpango mwovu wa Hamani Mwagagi ambao alikuwa ameupanga dhidi ya Wayahudi. Kisha mfalme alimnyooshea Esta fimbo yake ya utawala ya dhahabu naye aliinuka na kusimama mbele yake. Esta akasema, “Ikimpendeza mfalme, nami nikipata kibali, naye akiona ni jambo lililo sawa kunitendea, na akipendezwa nami, basi iandikwe amri ya kuzitangua barua zile Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, alizotunga na kuandika kuangamiza Wayahudi katika majimbo yote ya mfalme. Kwa maana nitawezaje kuvumilia kuona maafa yakiwapata watu wangu? Nitawezaje kuvumilia kuona maangamizi ya jamaa zangu?”