Esta 8:1-8
Esta 8:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku hiyohiyo, mfalme Ahasuero alimkabidhi malkia Esta mali yote ya Hamani, adui ya Wayahudi. Esta akamjulisha mfalme kwamba Mordekai ni jamaa yake. Basi, tangu wakati huo, Mordekai akaruhusiwa kumwona mfalme. Mfalme akaivua pete yake ya mhuri aliyokuwa amemnyanganya Hamani, akampa Mordekai. Esta naye akampa Mordekai mamlaka juu ya mali ya Hamani. Kisha Esta akazungumza tena na mfalme; akajitupa chini, miguuni pa mfalme, huku analia, akamsihi mfalme aukomeshe mpango mbaya ambao Hamani, wa uzao wa Agagi, alikuwa amepanga dhidi ya Wayahudi. Mfalme akamnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu, naye Esta akasimama na kusema, “Ukipenda, ewe mfalme, na kama unanijali na ukiona inafaa, tafadhali, toa tangazo la kufutilia mbali mipango ambayo Hamani alikuwa ameamuru itekelezwe. Mipango hiyo ni ile ya mwana wa Hamedatha, mzaliwa wa Agagi, aliyopanga ili kuwaangamiza Wayahudi wote katika mikoa yote. Maana, ninawezaje kuvumilia kuona watu wangu wanaangamizwa na jamaa zangu wanauawa?” Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, yule Myahudi, “Tazameni! Nimempa Esta mali yake Hamani, naye wamekwisha mnyonga kwa sababu ya njama zake dhidi ya Wayahudi. Mwaweza kuwaandikia Wayahudi lolote mpendalo. Tena mwaweza kuandika kwa jina langu na kutumia mhuri wa kifalme, kwa sababu tangazo ambalo limetolewa kwa jina la mfalme na kupigwa mhuri wa mfalme, haliwezi kubatilishwa.”
Esta 8:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ile mfalme Ahasuero alimpa malkia Esta nyumba yake Hamani, yule adui ya Wayahudi. Mordekai naye akaja mbele ya mfalme; kwa maana Esta alikuwa amedhihirisha alivyomhusu. Basi mfalme akaivua pete yake, aliyompokonya Hamani, akampa Mordekai. Naye Esta akamweka Mordekai kuwa juu ya mlango wake Hamani. Tena Esta akasema na mfalme mara ya pili, akaanguka miguuni pake, akamsihi kwa machozi ayaondoe madhara ya Hamani, Mwagagi, na shauri alilowafanyia Wayahudi. Ndipo mfalme alipomnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu. Basi Esta akaondoka, akasimama mbele ya mfalme. Akasema, Mfalme akiona vema, nami nikiwa nimepata kibali machoni pake, na neno likionekana jema mbele ya mfalme, nami nikimpendeza machoni pake, na iandikwe amri kuzitangua barua za Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuziandika ili kuwaangamiza Wayahudi walioko katika mikoa yote ya mfalme. Maana, ninawezaje kustahimili kuyaona mabaya yatakayowajia watu wangu? Au kuyatazama maangamizi ya jamaa zangu? Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, Myahudi, akasema, Tazama, nimekwisha kumpa Esta nyumba yake Hamani, naye mwenyewe wamekwisha kumtundika juu ya mti, kwa sababu aliwatia mikono Wayahudi. Basi nanyi pia waandikieni Wayahudi vyovyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie mhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa mhuri kwa pete ya mfalme, hakuna awezaye kulitangua.
Esta 8:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ile mfalme Ahasuero alimpa malkia Esta nyumba yake Hamani, yule adui ya Wayahudi. Mordekai naye akahudhuria mbele ya mfalme; kwa maana Esta alikuwa amedhihirisha alivyomhusu. Basi mfalme akaivua pete yake, aliyompokonya Hamani, akampa Mordekai. Naye Esta akamweka Mordekai kuwa juu ya mlango wake Hamani. Tena Esta akasema na mfalme mara ya pili, akaanguka miguuni pake, akamsihi kwa machozi ayaondoe madhara ya Hamani, Mwagagi, na shauri alilowafanyia Wayahudi. Ndipo mfalme alipomnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu. Basi Esta akaondoka, akasimama mbele ya mfalme. Akasema, Mfalme akiona vema, nami nikiwa nimepata kibali machoni pake, na neno likionekana jema mbele ya mfalme, nami nikimpendeza machoni pake, iandikwe kuzitangua barua za Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuziandika ili kuwaangamiza Wayahudi walioko katika majimbo yote ya mfalme. Kwa maana niwezeje kuyaona mabaya yatakayowajia watu wangu? Au niwezeje kuyatazama maangamizo ya jamaa zangu? Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, Myahudi, kusema, Tazama, nimekwisha kumpa Esta nyumba yake Hamani, naye mwenyewe wamekwisha kumtundika juu ya mti, kwa sababu aliwatia mikono Wayahudi. Basi waandikieni Wayahudi pia vyo vyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie muhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme hakuna awezaye kulitangua.
Esta 8:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku ile ile Mfalme Ahasuero akampa Malkia Esta shamba la Hamani, adui wa Wayahudi. Naye Mordekai akaja mbele ya mfalme, kwa kuwa Esta alikuwa amesema jinsi anavyohusiana naye. Mfalme akaivua pete yake ya muhuri, ambayo alikuwa amemnyangʼanya Hamani, akampa Mordekai, naye Esta akamweka Mordekai asimamie shamba la Hamani. Esta alimsihi tena mfalme, akianguka miguuni pake na kulia. Akamwomba akomeshe mpango mwovu wa Hamani Mwagagi ambao alikuwa ameupanga dhidi ya Wayahudi. Kisha mfalme alimnyooshea Esta fimbo yake ya utawala ya dhahabu naye aliinuka na kusimama mbele yake. Esta akasema, “Ikimpendeza mfalme, nami nikipata kibali, naye akiona ni jambo lililo sawa kunitendea, na akipendezwa nami, basi iandikwe amri ya kuzitangua barua zile Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, alizotunga na kuandika kuangamiza Wayahudi katika majimbo yote ya mfalme. Kwa maana nitawezaje kuvumilia kuona maafa yakiwapata watu wangu? Nitawezaje kuvumilia kuona maangamizi ya jamaa zangu?” Mfalme Ahasuero akawajibu Malkia Esta na Mordekai Myahudi, “Kwa sababu Hamani aliwashambulia Wayahudi, nimetoa shamba la Hamani kwa Esta, naye ameangikwa kwenye mti wa kunyongea. Basi andika amri nyingine kwa jina la mfalme kwa ajili ya Wayahudi kama unavyoona vyema, kisha uifunge kwa kutia muhuri kwa pete ya mfalme kwa kuwa hakuna andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme linaloweza kutanguliwa.”