Esta 7:1-4
Esta 7:1-4 Biblia Habari Njema (BHN)
Hivyo mfalme na Hamani wakaenda kula karamu na malkia Esta. Katika siku ya pili, walipokuwa wanakunywa divai, mfalme akamwuliza tena Esta, “Sasa, malkia Esta, unataka nini? Niambie, nawe utapata. Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme wangu, utapewa.” Malkia Esta akamjibu, “Kama nimepata upendeleo kwako, ewe mfalme, na ukiwa radhi kunitimizia ombi langu, haja yangu ni mimi niishi na watu wangu pia. Maana, mimi na watu wangu tumeuzwa tuuawe, kuangamizwa na kufutiliwa mbali. Kama tungeuzwa tu kuwa watumwa na watumwa wa kike, ningekaa kimya, wala nisingekusumbua. Ingawa tutakatiliwa mbali hakuna adui atakayeweza kufidia hasara hii kwa mfalme.”
Esta 7:1-4 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi mfalme na Hamani walikwenda kula karamu pamoja na malkia Esta. Mfalme akamwambia Esta tena siku ya pili pale pale penye karamu ya divai, Malkia Esta, dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utatimiziwa. Ndipo malkia Esta alipojibu, akasema, Ikiwa nimepata kibali machoni pako, Ewe Mfalme, na ikimpendeza mfalme, hebu nipewe maisha yangu kwa ombi langu, na watu wangu kwa maombi yangu. Maana tumeuzwa, mimi na watu wangu, ili tuharibiwe, na kuuawa, na kuangamia. Kama tungaliuzwa kuwa watumwa na wajakazi, ningalinyamaza; japo hata hivyo adui asingeweza kufidia hasara ya mfalme.
Esta 7:1-4 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi mfalme na Hamani walikuja kula karamu pamoja na malkia Esta. Mfalme akamwambia Esta tena siku ya pili pale pale penye karamu ya divai, Malkia Esta, dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa. Ndipo malkia Esta alipojibu, akasema, Mfalme, ikiwa nimepata kibali machoni pako, na mfalme akiona vema, nipewe maisha yangu kuwa dua yangu, na watu wangu kuwa haja yangu. Maana tumeuzwa, mimi na watu wangu, ili tuharibiwe, na kuuawa, na kuangamia. Kama tungaliuzwa kuwa watumwa na wajakazi, ningalinyamaza; ila hata hivyo msiba wetu haulinganishwi na hasara ya mfalme.
Esta 7:1-4 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi mfalme na Hamani wakaenda kula chakula pamoja na Malkia Esta. Walipokuwa wakinywa mvinyo katika siku ya pili, mfalme akauliza tena, “Malkia Esta, ni nini haja yako? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.” Kisha Malkia Esta akajibu, “Kama nimepata kibali kwako, ee mfalme, tena kama inapendeza utukufu wako, nijalie maisha yangu, hii ndiyo haja yangu. Pia uokoe watu wangu, hili ndilo ombi langu. Kwa kuwa mimi na watu wangu tumeuzwa ili tuangamizwe, tuchinjwe na tuharibiwe. Tungeuzwa tu kama watumwa wa kiume na wa kike, ningenyamaza, kwa sababu shida kiasi hicho haingetosha kumsumbua mfalme.”