Esta 5:9-14
Esta 5:9-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Hamani alitoka huko karamuni mwenye furaha tele na moyo mkunjufu. Lakini alipomwona Mordekai penye lango la ikulu, hasimami wala hampi heshima, Hamani akawaka hasira. Hata hivyo, alijizuia, akaenda zake nyumbani. Halafu akawaalika nyumbani kwake rafiki zake, na kumwomba Zereshi mkewe ajiunge nao. Ndipo akaanza kuelezea juu ya utajiri aliokuwa nao, wana aliokuwa nao, jinsi mfalme alivyompandisha cheo, na jinsi alivyopewa madaraka zaidi kuliko maofisa wengine wote wa mfalme. Hamani akaendelea kujitapa, “Isitoshe malkia Esta hakumwalika mtu mwingine yeyote pamoja na mfalme isipokuwa mimi tu. Hata kesho pia, ametualika mimi na mfalme. Lakini yote haya hayaniridhishi iwapo nitaendelea kumwona yule Myahudi Mordekai penye lango la ikulu.” Basi, Zereshi, mkewe, na marafiki zake, wakamshauri hivi: “Kwa nini asitengenezewe mti wa kuulia, wenye urefu wa mita ishirini na mbili? Kesho asubuhi, unaweza kuzungumza na mfalme ili Mordekai auawe juu yake, kisha uende ukale karamu na mfalme kwa furaha.” Wazo hilo lilimfurahisha Hamani, naye akatengeneza mti wa kuulia.
Esta 5:9-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kunyenyekea mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai. Lakini Hamani akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma watu kuwaita marafiki zake na Zereshi mkewe. Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa watoto wake, na pia mambo yote ambayo mfalme amemfanikisha kwayo, na jinsi alivyompandisha cheo juu ya wakuu na watumishi wa mfalme. Zaidi ya hayo Hamani akasema, Naye malkia Esta hakumkaribisha mtu yeyote pamoja na mfalme katika karamu aliyoiandaa, ila mimi peke yangu; hata na kesho pia nimealikwa naye pamoja na mfalme. Bali haya yote yanifaa nini, niendeleapo kumwona yule Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa mfalme? Basi Zereshi mkewe na marafiki wote wa Hamani wakamwambia, Na kitengenezwe kiunzi cha mti wa kunyongea wa urefu wa mikono hamsini, na kesho asubuhi useme na mfalme ili Mordekai atundikwe juu yake; ndipo utakapoingia kwa furaha pamoja na mfalme karamuni. Basi ushauri huu ukamridhisha Hamani, akautengeneza mti wa kunyongea.
Esta 5:9-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kutetemeka mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai. Walakini Hamani akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma kuwaita rafiki zake na Zereshi mkewe. Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa watoto wake, nayo mambo yote pia ambayo mfalme amemfanikisha katika hayo, na jinsi alivyompandisha juu ya maakida na watumishi wa mfalme. Zaidi ya hayo Hamani akasema, Naye malkia Esta hakumkaribisha mtu ye yote pamoja na mfalme katika karamu aliyoiandaa, ila mimi peke yangu; hata na kesho pia nimealikwa naye pamoja na mfalme. Bali haya yote yanifaa nini, pindi nimwonapo yule Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa mfalme? Basi Zereshi mkewe akamwambia, na rafiki zake wote, Na ufanyizwe mti wa mikono hamsini urefu wake, na kesho asubuhi useme na mfalme ili Mordekai atundikwe juu yake; ndipo utakapoingia kwa kicheko pamoja na mfalme karamuni. Basi neno likampendeza Hamani, akaufanyiza ule mti.
Esta 5:9-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hamani alitoka siku hiyo kwa furaha na moyo mchangamfu. Lakini alipomwona Mordekai langoni mwa mfalme na kuona kwamba hakusimama wala hakuonesha hofu mbele yake, alijawa na ghadhabu dhidi ya Mordekai. Hata hivyo, Hamani alijizuia akaenda zake nyumbani. Akawaita pamoja rafiki zake na Zereshi, mkewe. Hamani akajisifia kwao juu ya utajiri wake mwingi, wanawe wengi na kwa njia zote ambazo mfalme amemheshimu kwazo na jinsi alivyomweka juu ya wakuu na maafisa wengine. Hamani akaongeza, “Si hayo tu. Mimi ndiye mtu pekee ambaye Malkia Esta amemwalika kumsindikiza mfalme kwenye karamu aliyomwandalia. Naye amenialika pamoja na mfalme kesho. Lakini haya yote hayanipi kuridhika iwapo ninaendelea kumwona yule Myahudi Mordekai akiketi kwenye lango la mfalme.” Zereshi mkewe na rafiki zake wote wakamwambia, “Tengeneza mahali pa kuangika watu kimo chake dhiraa hamsini, kisha kesho asubuhi mwombe mfalme Mordekai aangikwe juu yake. Ndipo uende na mfalme kwenye karamu kwa furaha.” Shauri hili lilimpendeza Hamani, naye akajenga mahali pa kuangika watu.