Esta 5:6-11
Esta 5:6-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Walipokuwa wanakunywa divai, mfalme akamwuliza tena Esta: “Unataka nini? Niambie, nawe utapata. Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme wangu, utapewa.” Esta akamjibu, “Ombi langu ni hili: Kama u radhi, ewe mfalme, kukubali ombi langu, basi, naomba wewe na Hamani mje kesho kwenye karamu nyingine nitakayowaandalieni. Wakati huo nitakujulisha ombi langu.” Hamani alitoka huko karamuni mwenye furaha tele na moyo mkunjufu. Lakini alipomwona Mordekai penye lango la ikulu, hasimami wala hampi heshima, Hamani akawaka hasira. Hata hivyo, alijizuia, akaenda zake nyumbani. Halafu akawaalika nyumbani kwake rafiki zake, na kumwomba Zereshi mkewe ajiunge nao. Ndipo akaanza kuelezea juu ya utajiri aliokuwa nao, wana aliokuwa nao, jinsi mfalme alivyompandisha cheo, na jinsi alivyopewa madaraka zaidi kuliko maofisa wengine wote wa mfalme.
Esta 5:6-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi mfalme akamwambia Esta pale penye karamu ya divai, Dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utatimiziwa. Esta akajibu, na kusema, Dua yangu ni hii, na haja yangu ni hii, Ikiwa nimepata kibali machoni pa mfalme, na mfalme akiona vema kunipa niombalo, na kunitimizia haja yangu, na aje tena mfalme na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia, nami kesho nitafanya kama vile mfalme alivyosema. Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kunyenyekea mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai. Lakini Hamani akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma watu kuwaita marafiki zake na Zereshi mkewe. Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa watoto wake, na pia mambo yote ambayo mfalme amemfanikisha kwayo, na jinsi alivyompandisha cheo juu ya wakuu na watumishi wa mfalme.
Esta 5:6-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi mfalme akamwambia Esta pale penye karamu ya divai, Dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa. Esta akajibu, na kusema, Dua yangu ni hii, na haja yangu ni hii, Ikiwa nimepata kibali machoni pa mfalme, na mfalme akiona vema kunipa niombalo, na kunifanyizia haja yangu, na aje tena mfalme na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia, nami kesho nitafanya kama vile mfalme alivyosema. Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kutetemeka mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai. Walakini Hamani akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma kuwaita rafiki zake na Zereshi mkewe. Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa watoto wake, nayo mambo yote pia ambayo mfalme amemfanikisha katika hayo, na jinsi alivyompandisha juu ya maakida na watumishi wa mfalme.
Esta 5:6-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Walipokuwa wakinywa mvinyo mfalme akamuuliza Esta tena, “Sasa haja yako ni nini? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.” Esta akajibu, “Haja yangu na ombi langu ni hili: Kama mfalme ameona vyema, nami nimepata kibali kwake, na ikimpendeza mfalme kunipa ombi langu na kunitimizia haja yangu, mfalme na Hamani waje kwangu kesho katika karamu nitakayowaandalia. Kisha nitajibu swali la mfalme.” Hamani alitoka siku hiyo kwa furaha na moyo mchangamfu. Lakini alipomwona Mordekai langoni mwa mfalme na kuona kwamba hakusimama wala hakuonesha hofu mbele yake, alijawa na ghadhabu dhidi ya Mordekai. Hata hivyo, Hamani alijizuia akaenda zake nyumbani. Akawaita pamoja rafiki zake na Zereshi, mkewe. Hamani akajisifia kwao juu ya utajiri wake mwingi, wanawe wengi na kwa njia zote ambazo mfalme amemheshimu kwazo na jinsi alivyomweka juu ya wakuu na maafisa wengine.