Esta 4:4-12
Esta 4:4-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Malkia Esta alipoarifiwa na matowashi na watumwa wa kike wake habari za Mordekai alihuzunika sana. Akampelekea Mordekai nguo za kuvaa badala ya vazi la gunia, lakini Mordekai akazikataa. Basi, akamwita Hathaki, mmoja wa matowashi wa mfalme aliyeteuliwa na mfalme amhudumie Esta, akamtuma kwa Mordekai kuuliza kisa na maana ya tukio hilo. Hathaki alimwendea Mordekai uwanjani, mbele ya lango la ikulu. Mordekai akamsimulia Hathaki yote yaliyokuwa yamempata, na kiasi kamili cha fedha ambayo Hamani alikuwa ameahidi kulipa katika hazina ya mfalme kama Wayahudi wote wangeangamizwa. Alimpa pia nakala moja ya tangazo lililokuwa limetolewa mjini Susa kuhusu kuangamizwa kwa Wayahudi, akamwomba amchukulie Esta, amweleze hali ilivyo, na kumwambia aende kumsihi mfalme na kumwomba awahurumie Wayahudi, watu wake Esta. Hathaki akaenda akamweleza Esta yote aliyosema Mordekai. Naye Esta akamwambia Hathaki arudi akamwambie Mordekai, “Watumishi wote wa mfalme na raia wa mikoa yote wanajua ya kwamba mtu yeyote yule akiingia katika ua wa ndani na kumwona mfalme bila kuitwa, huyo ni lazima auawe. Anayeweza kunusurika ni yule tu ambaye mfalme atamnyoshea fimbo yake ya dhahabu ili kumsalimisha. Kumbe mimi sijaitwa na mfalme, yapata mwezi mzima sasa.” Mordekai alipopata ujumbe wa Esta
Esta 4:4-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi wajakazi wake Esta, na wasimamizi wake wa nyumba, wakamjia, wakampasha habari; naye malkia akahuzunika mno; akampelekea Mordekai mavazi, ili kumvika, na kumwondolea gunia lake; lakini yeye hakukubali. Kisha Esta akamwita Hathaki, towashi mmojawapo wa mfalme, aliyemwagiza amhudumue Esta, akamtuma kwa Mordekai, ili ajue mambo hayo, na maana yake ni nini. Basi yule Hathaki akatoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanda wa mji ulipo mbele ya mlango wa mfalme. Naye Mordekai akamweleza yote yaliyompata, na hesabu ya fedha Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme, ili Wayahudi waangamizwe. Pia akampa na nakala ya andiko la mbiu ya kuwaangamiza, iliyotangazwa Shushani, ili amwoneshe Esta, na kumweleza; tena amwagize aingie kwa mfalme, kumsihi na kuwaombea watu wake. Basi Hathaki akaja, akamwambia Esta maneno ya Mordekai. Ndipo Esta akasema na Hathaki, akamtuma tena kwa Mordekai, kusema, Watumishi wote wa mfalme wanajua sana, hata na watu wa majimbo ya mfalme, ya kwamba mtu yeyote, akiwa mwanamume au mwanamke, atakayemjia mfalme katika ua wa ndani, wala hakuitwa, kuna sheria moja kwake, ni kwamba auawe; isipokuwa yeye ambaye mfalme atamnyoshea fimbo ya dhahabu, ili aishi; wala mimi sikuitwa niingie kwa mfalme yapata siku thelathini. Basi wakamwambia Mordekai maneno ya Esta.
Esta 4:4-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi wajakazi wake Esta, na wasimamizi wake wa nyumba, wakamjia, wakampasha habari; naye malkia akahuzunika mno; akampelekea Mordekai mavazi, ili kumvika, na kumwondolea gunia lake; walakini yeye asikubali. Kisha Esta akamwita Hathaki, msimamizi-wa-nyumba mmojawapo wa mfalme, aliyemwagiza amhudumu Esta, akamtuma kwa Mordekai, ili ajue mambo hayo, na maana yake ni nini. Basi yule Hathaki akatoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanda wa mji ulipo mbele ya mlango wa mfalme. Naye Mordekai akamweleza yote yaliyompata, na hesabu ya fedha Hamani aliyoahidi kulipa katika hazina ya mfalme, ili Wayahudi waangamizwe. Pia akampa na nakili ya andiko la mbiu ya kuwaangamiza, iliyotangazwa Shushani, ili amwonyeshe Esta, na kumweleza; tena amwagize aingie kwa mfalme, kumsihi na kuwaombea watu wake. Basi Hathaki akaja, akamwambia Esta maneno ya Mordekai. Ndipo Esta akasema na Hathaki, akamtuma tena kwa Mordekai, kusema, Watumwa wote wa mfalme wanajua sana, hata na watu wa majimbo ya mfalme, ya kwamba mtu ye yote, akiwa mwanamume au mwanamke, atakayemjia mfalme katika ua wa ndani, wala hakuitwa, kuna sheria moja kwake, ni kwamba auawe; isipokuwa yeye ambaye mfalme atamnyoshea fimbo ya dhahabu, ili aishi; wala mimi sikuitwa niingie kwa mfalme yapata siku thelathini. Basi wakamwambia Mordekai maneno ya Esta.
Esta 4:4-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wajakazi wa Esta na matowashi walipokuja na kumwambia kuhusu Mordekai, alipatwa na huzuni kuu. Alimtumia nguo avae badala ya magunia, lakini Mordekai hakuzikubali. Ndipo Esta akamwita Hathaki, mmoja wa matowashi wa mfalme aliyekuwa amewekwa kumhudumia Esta, akamwagiza kutafuta kilichokuwa kikimtaabisha Mordekai na ni kwa nini. Basi Hathaki alitoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanja ulio wazi wa mji mbele ya lango la mfalme. Mordekai akamwambia kila kitu ambacho kimempata, pamoja na hesabu kamili ya fedha ambazo Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme kwa ajili ya maangamizi ya Wayahudi. Akampa nakala ya andiko la amri kwa ajili ya maangamizi yao, lililokuwa limechapishwa huko Shushani, kumwonesha Esta na kumwelezea. Mordekai akamwambia towashi amshawishi Esta kwenda mbele ya mfalme kuomba rehema na kumsihi kwa ajili ya watu wake. Hathaki akarudi kwa Esta na kumwarifu alilolisema Mordekai. Kisha Esta akamwamuru Hathaki amweleze Mordekai, “Maafisa wote wa mfalme na watu wa majimbo ya ufalme wanajua kuwa mwanaume au mwanamke yeyote ambaye ataingia kumwona mfalme katika ua wa ndani bila kuitwa, mfalme ana sheria moja tu: Atauawa. Njia pekee kinyume na hili ni mfalme kumnyooshea fimbo ya dhahabu ili aishi. Lakini siku thelathini zimepita tangu nilipoitwa kwenda kwa mfalme.” Wakati Mordekai aliarifiwa maneno ya Esta