Esta 4:1-7
Esta 4:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Mordekai alipojua yote yaliyotukia, alizirarua nguo zake, akavaa vazi la gunia, na kujitia majivu. Kisha, akapita katikati ya mji akilia kwa sauti ya uchungu. Alikwenda mpaka penye lango la ikulu ya mfalme, lakini hakuweza kuingia kwa sababu hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia ikulu akiwa amevaa vazi la gunia. Katika kila mkoa, mara tu amri ya mfalme ilipotangazwa, msiba mkubwa uliwakumba Wayahudi. Walifunga, wakalia na kuomboleza; na wengi wao walilala katika majivu wakiwa wamevaa magunia. Malkia Esta alipoarifiwa na matowashi na watumwa wa kike wake habari za Mordekai alihuzunika sana. Akampelekea Mordekai nguo za kuvaa badala ya vazi la gunia, lakini Mordekai akazikataa. Basi, akamwita Hathaki, mmoja wa matowashi wa mfalme aliyeteuliwa na mfalme amhudumie Esta, akamtuma kwa Mordekai kuuliza kisa na maana ya tukio hilo. Hathaki alimwendea Mordekai uwanjani, mbele ya lango la ikulu. Mordekai akamsimulia Hathaki yote yaliyokuwa yamempata, na kiasi kamili cha fedha ambayo Hamani alikuwa ameahidi kulipa katika hazina ya mfalme kama Wayahudi wote wangeangamizwa.
Esta 4:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Mordekai alipojua mambo yote yaliyofanyika, alizirarua nguo zake, akajivika gunia na kujipaka majivu, akatoka hadi katikati ya mji, akalia kwa sauti kuu ya uchungu. Pia akafika hata mbele ya mlango wa mfalme; maana hakuna awezaye kuingia ndani ya mlango wa mfalme akiwa amevaa magunia. Na katika kila mkoa, ambako amri ya mfalme na mbiu yake imewasili, palikuwako msiba mkuu kwa Wayahudi, na kufunga, na kulia, na kuomboleza; hata na wengi wakalala juu ya gunia na majivu. Basi wajakazi wake Esta, na wasimamizi wake wa nyumba, wakamjia, wakampasha habari; naye malkia akahuzunika mno; akampelekea Mordekai mavazi, ili kumvika, na kumwondolea gunia lake; lakini yeye hakukubali. Kisha Esta akamwita Hathaki, towashi mmojawapo wa mfalme, aliyemwagiza amhudumue Esta, akamtuma kwa Mordekai, ili ajue mambo hayo, na maana yake ni nini. Basi yule Hathaki akatoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanda wa mji ulipo mbele ya mlango wa mfalme. Naye Mordekai akamweleza yote yaliyompata, na hesabu ya fedha Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme, ili Wayahudi waangamizwe.
Esta 4:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Mordeikai alipojua mambo yote yaliyofanyika, alizirarua nguo zake, akajivika gunia pamoja na majivu, akatoka hata kufika katikati ya mji, akalia kwa sauti kuu ya uchungu. Pia akafika hata mbele ya mlango wa mfalme; maana hakuna awezaye kuingia ndani ya mlango wa mfalme hali amevaa magunia. Na katika kila jimbo, ambako amri ya mfalme na mbiu yake imewasili, palikuwako msiba mkuu kwa Wayahudi, na kufunga, na kulia, na kuomboleza; hata na wengi wakalala juu ya gunia na majivu. Basi wajakazi wake Esta, na wasimamizi wake wa nyumba, wakamjia, wakampasha habari; naye malkia akahuzunika mno; akampelekea Mordekai mavazi, ili kumvika, na kumwondolea gunia lake; walakini yeye asikubali. Kisha Esta akamwita Hathaki, msimamizi-wa-nyumba mmojawapo wa mfalme, aliyemwagiza amhudumu Esta, akamtuma kwa Mordekai, ili ajue mambo hayo, na maana yake ni nini. Basi yule Hathaki akatoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanda wa mji ulipo mbele ya mlango wa mfalme. Naye Mordekai akamweleza yote yaliyompata, na hesabu ya fedha Hamani aliyoahidi kulipa katika hazina ya mfalme, ili Wayahudi waangamizwe.
Esta 4:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mordekai alipojua yote yaliyokwisha kufanyika, alirarua mavazi yake, akavaa magunia na kujipaka majivu, akaenda mjini akiomboleza kwa sauti na kwa uchungu. Alienda na kusimama nje ya lango la mfalme, kwa sababu hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia akiwa amevaa magunia. Katika kila jimbo ambapo amri na agizo la mfalme lilifika, kulikuwa na maombolezo makuu miongoni mwa Wayahudi pamoja na kufunga, kulia na kuomboleza. Watu wengi wakalala juu ya magunia na majivu. Wajakazi wa Esta na matowashi walipokuja na kumwambia kuhusu Mordekai, alipatwa na huzuni kuu. Alimtumia nguo avae badala ya magunia, lakini Mordekai hakuzikubali. Ndipo Esta akamwita Hathaki, mmoja wa matowashi wa mfalme aliyekuwa amewekwa kumhudumia Esta, akamwagiza kutafuta kilichokuwa kikimtaabisha Mordekai na ni kwa nini. Basi Hathaki alitoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanja ulio wazi wa mji mbele ya lango la mfalme. Mordekai akamwambia kila kitu ambacho kimempata, pamoja na hesabu kamili ya fedha ambazo Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme kwa ajili ya maangamizi ya Wayahudi.