Esta 3:7-11
Esta 3:7-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa mfalme Ahasuero, mnamo mwezi wa kwanza uitwao Nisani, Hamani aliagiza kura (yaani Purimu) ifanywe kupata siku na mwezi ambapo angetekeleza njama zake. Basi, kura ikaangukia siku ya kumi na nne ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari. Basi, Hamani akamwambia mfalme: “Wapo watu wa taifa fulani walioko kila mahali katika utawala wako, nao wako katika kila mkoa. Watu hao wana sheria zilizo tofauti kabisa na za watu wengine. Isitoshe, wao hawazitii sheria zako, kwa hiyo haikufaidi chochote kuwavumilia. “Ukipenda, ewe mfalme, amri na itolewe, watu hawa waangamizwe. Nami naahidi, kama utaamuru hivyo, nitatoa kiasi cha kilo 10,000 za fedha ziwekwe katika hazina ya mfalme.” Mfalme akaivua pete yake, ambayo ilitumiwa kupigia mhuri matangazo, akampa adui wa Wayahudi Hamani mwana wa Hamedatha wa uzao wa Agagi. Ndipo mfalme akamwambia Hamani, “Umepewa watu wote na hizo fedha, tumia upendavyo.”
Esta 3:7-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hadi mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari. Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna watu wa taifa moja waliotawanyika na kukaa kila mahali katikati ya watu wa mataifa walioko katika mikoa yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimetofautiana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao. Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta elfu kumi za fedha mikononi mwa watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme. Ndipo mfalme alipoivua pete yake ya kupigia mhuri kutoka mkononi, akampa Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi. Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema.
Esta 3:7-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hata mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari. Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna taifa moja waliotawanyika na kukaa mahali mahali katikati ya mataifa walioko katika majimbo yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimefarakana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao. Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha mikononi mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme. Ndipo mfalme alipoivua pete yake mkononi, akampa Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi. Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema.
Esta 3:7-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Mfalme Ahasuero, katika mwezi wa kwanza uitwao Nisani, walipiga puri (yaani kura) mbele ya Hamani ili kuchagua siku na mwezi. Kura ikaangukia kwenye mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari. Kisha Hamani akamwambia Mfalme Ahasuero, “Wako watu fulani wameenea na kutawanyika miongoni mwa watu katika majimbo yote ya ufalme wako, ambao desturi zao ni tofauti na zile za watu wengine wote, nao hawatii sheria za mfalme. Haifai mfalme kuwavumilia watu hawa. Kama inampendeza mfalme, itolewe amri kuwaangamiza, nami nitaweka talanta elfu kumi za fedha katika hazina ya mfalme kwa ajili ya watu watakaoshughulikia jambo hili.” Basi mfalme alichukua pete yake ya muhuri kutoka kidole chake na kumpa Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, adui wa Wayahudi. Mfalme akamwambia Hamani, “Baki na fedha yako na uwatendee hao watu utakavyo.”