Esta 3:5-15
Esta 3:5-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Hamani aliwaka hasira alipojua kwamba Mordekai hamwinamii wala hamsujudii. Tena alipogundua kuwa Mordekai alikuwa Myahudi, aliamua kwamba kumwadhibu peke yake haitoshi. Basi akala njama kuwaangamiza Wayahudi wote, watu wa ukoo wa Mordekai, katika utawala wa mfalme Ahasuero. Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa mfalme Ahasuero, mnamo mwezi wa kwanza uitwao Nisani, Hamani aliagiza kura (yaani Purimu) ifanywe kupata siku na mwezi ambapo angetekeleza njama zake. Basi, kura ikaangukia siku ya kumi na nne ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari. Basi, Hamani akamwambia mfalme: “Wapo watu wa taifa fulani walioko kila mahali katika utawala wako, nao wako katika kila mkoa. Watu hao wana sheria zilizo tofauti kabisa na za watu wengine. Isitoshe, wao hawazitii sheria zako, kwa hiyo haikufaidi chochote kuwavumilia. “Ukipenda, ewe mfalme, amri na itolewe, watu hawa waangamizwe. Nami naahidi, kama utaamuru hivyo, nitatoa kiasi cha kilo 10,000 za fedha ziwekwe katika hazina ya mfalme.” Mfalme akaivua pete yake, ambayo ilitumiwa kupigia mhuri matangazo, akampa adui wa Wayahudi Hamani mwana wa Hamedatha wa uzao wa Agagi. Ndipo mfalme akamwambia Hamani, “Umepewa watu wote na hizo fedha, tumia upendavyo.” Basi, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza, Hamani aliwaita makatibu wote wa mfalme, akawapa tangazo ambalo alitaka litafsiriwe kwa kila lugha na kila namna ya maandishi katika utawala huo, halafu nakala zisambazwe kwa watawala wote, wakuu wa mikoa yote, na viongozi wa makabila – kufuatana na lugha zinazotumika kwao. Tangazo hilo lilitolewa kwa jina la mfalme Ahasuero, na kupigwa mhuri kwa pete yake. Matarishi walizipeleka nyaraka hizo kwa kila mkoa katika utawala huo. Tangazo hilo lilisema kwamba kwa siku moja tu, yaani siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari, Wayahudi wote – vijana kwa wazee, wanawake kwa watoto, wote lazima wauawe, waangamizwe na kufutiliwa mbali, na mali zao zote zichukuliwe. Taarifa hiyo ilitakiwa iandikwe hadharani katika kila mkoa, ili kila mtu ajiandae kwa ajili ya siku hiyo. Kwa amri ya mfalme, tangazo hili lilitolewa katika mji mkuu wa Susa, nao matarishi wakalitangaza katika mikoa yote. Mfalme na Hamani walikaa chini kunywa wakati watu mjini Susa wanafadhaika.
Esta 3:5-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hamwinamii wala kumsujudia, alighadhibika sana. Akaona haitoshi kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila lake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai. Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hadi mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari. Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna watu wa taifa moja waliotawanyika na kukaa kila mahali katikati ya watu wa mataifa walioko katika mikoa yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimetofautiana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao. Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta elfu kumi za fedha mikononi mwa watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme. Ndipo mfalme alipoivua pete yake ya kupigia mhuri kutoka mkononi, akampa Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi. Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema. Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza; na barua zikaandikwa, kama vile Hamani alivyoagiza, kwa wakuu wa mfalme, na wakuu wa mikoa, na wakuu wa kila taifa; kila mkoa kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; zikaandikwa kwa jina la mfalme Ahasuero, na kutiwa mhuri kwa pete yake. Barua zikapelekwa kwa mikono ya matarishi mpaka mikoani yote ya mfalme kuwaangamiza Wayahudi wote, na kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee, watoto wachanga na wanawake pia, siku moja, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili ndio mwezi wa Adari; na kuyapora mali yao. Nakala ya andiko hilo ilitakiwa kutolewa katika kila mkoa, ili kuwaarifu watu wote wajiandae kwa ajili ya siku hiyo. Matarishi wakaondoka wakaenda haraka kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Shushani ngomeni. Mfalme na Hamani wakaketi ili kunywa divai; bali mji wa Shushani ukafadhaika.
Esta 3:5-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana. Akaona si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila yake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai. Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hata mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari. Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna taifa moja waliotawanyika na kukaa mahali mahali katikati ya mataifa walioko katika majimbo yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimefarakana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao. Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha mikononi mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme. Ndipo mfalme alipoivua pete yake mkononi, akampa Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi. Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema. Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza; na barua zikaandikwa, kama vile Hamani alivyoagiza vyote, kwa maakida wa mfalme, na maliwali waliokuwa juu ya kila jimbo, na wakuu wa kila taifa; kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; zikaandikwa kwa jinsi la mfalme Ahasuero, na kutiwa muhuri kwa pete yake. Barua zikapelekwa kwa mikono ya matarishi mpaka majimbo yote ya mfalme kuwaangamiza Wayahudi wote, na kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee, watoto wachanga na wanawake pia, siku moja, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili ndio mwezi wa Adari; na kuyachukua mali yao kuwa nyara. Nakili ya andiko, ya kupigwa mbiu katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote wawe tayari siku ile ile. Matarishi wakaondoka wakaenda haraka kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Shushani ngomeni. Mfalme na Hamani wakaketi ili kunywa divai; bali mji wa Shushani ukafadhaika.
Esta 3:5-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hamani alipoona kuwa Mordekai hampigii magoti wala kumpa heshima, alighadhibika. Hata hivyo, baada ya kujulishwa watu wa Mordekai ni akina nani, alibadili wazo la kumuua Mordekai peke yake. Badala yake Hamani alitafuta njia ya kuwaangamiza watu wote wa Mordekai, yaani Wayahudi, walio katika ufalme wote wa Ahasuero. Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Mfalme Ahasuero, katika mwezi wa kwanza uitwao Nisani, walipiga puri (yaani kura) mbele ya Hamani ili kuchagua siku na mwezi. Kura ikaangukia kwenye mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari. Kisha Hamani akamwambia Mfalme Ahasuero, “Wako watu fulani wameenea na kutawanyika miongoni mwa watu katika majimbo yote ya ufalme wako, ambao desturi zao ni tofauti na zile za watu wengine wote, nao hawatii sheria za mfalme. Haifai mfalme kuwavumilia watu hawa. Kama inampendeza mfalme, itolewe amri kuwaangamiza, nami nitaweka talanta elfu kumi za fedha katika hazina ya mfalme kwa ajili ya watu watakaoshughulikia jambo hili.” Basi mfalme alichukua pete yake ya muhuri kutoka kidole chake na kumpa Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, adui wa Wayahudi. Mfalme akamwambia Hamani, “Baki na fedha yako na uwatendee hao watu utakavyo.” Kisha siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza waandishi wa mfalme waliitwa. Wakaandika barua kwa kila jimbo na katika kila lugha ya watu kama agizo la Hamani lilivyotoka kwa mfalme, kwa watawala wa majimbo mbalimbali, na wakuu wa watu mbalimbali. Hizi ziliandikwa kwa jina la Mfalme Ahasuero mwenyewe na kutiwa muhuri wa pete yake mwenyewe. Barua zilipelekwa na tarishi katika majimbo yote ya mfalme zikiwa na amri ya kuharibu, kuua na kuangamiza Wayahudi wote, wadogo kwa wakubwa, wanawake na watoto wadogo, siku moja, yaani siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, na pia kuteka nyara vitu vyao. Nakala ya andiko la amri ilipaswa kutolewa kama sheria katika kila jimbo, na kufahamishwa kwa watu wa kila taifa ili waweze kuwa tayari kwa siku ile. Kwa kuharakishwa na amri ya mfalme, matarishi walienda na andiko lilitolewa katika mji wa ngome ya Shushani. Mfalme na Hamani waliketi na kunywa, lakini mji wa Shushani ulifadhaika.