Esta 3:1-11
Esta 3:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya mambo hayo, mfalme Ahasuero alimpandisha cheo Hamani, akawa waziri mkuu. Hamani alikuwa mwanawe Hamedatha, na wa uzao wa Agagi. Mfalme aliamuru maofisa wote wa serikali yake wamtii Hamani kwa kumwinamia na kumsujudia. Lakini Mordekai, hakumwinamia wala kumsujudia. Maofisa kadhaa wa mfalme waliokuwa penye lango la mfalme, wakamwuliza Mordekai, “Mbona wewe waidharau amri ya mfalme?” Kila siku walimshauri aache tabia hiyo, lakini Mordekai hakukubaliana nao. Alikataa kufanya hivyo kwa madai kwamba yeye ni Myahudi na kwa hiyo hawezi kumsujudia Hamani. Basi, wakamwarifu Hamani ili waone kama ataivumilia tabia ya Mordekai. Hamani aliwaka hasira alipojua kwamba Mordekai hamwinamii wala hamsujudii. Tena alipogundua kuwa Mordekai alikuwa Myahudi, aliamua kwamba kumwadhibu peke yake haitoshi. Basi akala njama kuwaangamiza Wayahudi wote, watu wa ukoo wa Mordekai, katika utawala wa mfalme Ahasuero. Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa mfalme Ahasuero, mnamo mwezi wa kwanza uitwao Nisani, Hamani aliagiza kura (yaani Purimu) ifanywe kupata siku na mwezi ambapo angetekeleza njama zake. Basi, kura ikaangukia siku ya kumi na nne ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari. Basi, Hamani akamwambia mfalme: “Wapo watu wa taifa fulani walioko kila mahali katika utawala wako, nao wako katika kila mkoa. Watu hao wana sheria zilizo tofauti kabisa na za watu wengine. Isitoshe, wao hawazitii sheria zako, kwa hiyo haikufaidi chochote kuwavumilia. “Ukipenda, ewe mfalme, amri na itolewe, watu hawa waangamizwe. Nami naahidi, kama utaamuru hivyo, nitatoa kiasi cha kilo 10,000 za fedha ziwekwe katika hazina ya mfalme.” Mfalme akaivua pete yake, ambayo ilitumiwa kupigia mhuri matangazo, akampa adui wa Wayahudi Hamani mwana wa Hamedatha wa uzao wa Agagi. Ndipo mfalme akamwambia Hamani, “Umepewa watu wote na hizo fedha, tumia upendavyo.”
Esta 3:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya hayo mfalme Ahasuero alimpandisha cheo Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, akamwinua, akamwekea kiti chake juu ya wakuu wote waliokuwapo pamoja naye. Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi langoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo mfalme alivyoamuru wamfanyie. Lakini Mordekai hakumwinamia, wala kumsujudia. Basi watumishi wa mfalme walioketi langoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waivunja amri ya mfalme? Ikawa, waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi. Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hamwinamii wala kumsujudia, alighadhibika sana. Akaona haitoshi kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila lake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai. Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hadi mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari. Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna watu wa taifa moja waliotawanyika na kukaa kila mahali katikati ya watu wa mataifa walioko katika mikoa yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimetofautiana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao. Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta elfu kumi za fedha mikononi mwa watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme. Ndipo mfalme alipoivua pete yake ya kupigia mhuri kutoka mkononi, akampa Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi. Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema.
Esta 3:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baada ya hayo mfalme Ahasuero alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, akampandisha, akamwekea kiti chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye. Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali Mordekai hakuinama, wala kumsujudia. Basi watumishi wa mfalme walioketi mlangoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme? Ikawa, waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi. Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana. Akaona si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila yake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai. Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hata mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari. Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna taifa moja waliotawanyika na kukaa mahali mahali katikati ya mataifa walioko katika majimbo yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimefarakana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao. Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha mikononi mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme. Ndipo mfalme alipoivua pete yake mkononi, akampa Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi. Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema.
Esta 3:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya matukio haya, Mfalme Ahasuero alimheshimu Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, akampandisha na kumpa kiti chake cha heshima cha juu sana kuliko wakuu wengine wote. Maafisa wote wa mfalme waliokaa langoni mwa mfalme walipiga magoti na kumpa Hamani heshima, kwa kuwa mfalme alikuwa ameamuru hili kuhusu Hamani. Lakini Mordekai hakumpigia magoti wala kumheshimu. Kisha maafisa wa mfalme waliokuwa langoni mwa mfalme walimuuliza Mordekai, “Kwa nini hutii agizo la mfalme?” Siku baada ya siku walizungumza naye lakini hakukubali. Kwa hiyo walimweleza Hamani kuona kama tabia ya Mordekai itaweza kuvumiliwa, kwa maana alikuwa amewaambia kuwa yeye ni Myahudi. Hamani alipoona kuwa Mordekai hampigii magoti wala kumpa heshima, alighadhibika. Hata hivyo, baada ya kujulishwa watu wa Mordekai ni akina nani, alibadili wazo la kumuua Mordekai peke yake. Badala yake Hamani alitafuta njia ya kuwaangamiza watu wote wa Mordekai, yaani Wayahudi, walio katika ufalme wote wa Ahasuero. Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Mfalme Ahasuero, katika mwezi wa kwanza uitwao Nisani, walipiga puri (yaani kura) mbele ya Hamani ili kuchagua siku na mwezi. Kura ikaangukia kwenye mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari. Kisha Hamani akamwambia Mfalme Ahasuero, “Wako watu fulani wameenea na kutawanyika miongoni mwa watu katika majimbo yote ya ufalme wako, ambao desturi zao ni tofauti na zile za watu wengine wote, nao hawatii sheria za mfalme. Haifai mfalme kuwavumilia watu hawa. Kama inampendeza mfalme, itolewe amri kuwaangamiza, nami nitaweka talanta elfu kumi za fedha katika hazina ya mfalme kwa ajili ya watu watakaoshughulikia jambo hili.” Basi mfalme alichukua pete yake ya muhuri kutoka kidole chake na kumpa Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, adui wa Wayahudi. Mfalme akamwambia Hamani, “Baki na fedha yako na uwatendee hao watu utakavyo.”