Esta 2:7-11
Esta 2:7-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Alikuwa na binamu, Esta, ambaye jina lake la Kiebrania lilikuwa Hadasa. Esta alikuwa msichana mzuri wa sura na umbo. Wazazi wake walipofariki, Mordekai alimchukua Esta, akamlea kama binti yake. Amri ya mfalme ilipotangazwa hadharani, wasichana wengi walipelekwa Susa, mji mkuu, wakawekwa chini ya ulinzi wa Hegai. Esta naye, alipelekwa kwenye ikulu ya mfalme, akawekwa chini ya uangalizi wa Hegai, yule mwangalizi wa wanawake. Hegai alipendezwa na Esta hata kiasi cha kumpendelea. Bila kupoteza wakati, alimpa Esta mafuta na chakula maalumu. Isitoshe, alimhamishia mahali pazuri kabisa katika nyumba hiyo ya wanawake, akamteulia watumwa wa kike saba kutoka ikulu ya mfalme, wamhudumie. Esta alikuwa hajajitambulisha ukoo wala kabila lake, maana Mordekai alikuwa amemwonya asifanye hivyo. Kila siku Mordekai alipitapita mbele ya ua wa nyumba hiyo ya wanawake ili apate kujua hali ya Esta na mambo ambayo yangempata.
Esta 2:7-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo nzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake. Basi amri ya mfalme na mbiu yake iliposikiwa, wasichana wengi wakakusanyika huko Susa, mji mkuu mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake. Yule mwanamwali akampendeza, akapokea fadhili kwake; naye akampa upesi vifaa vya utakaso, pamoja na chakula chake, na vijakazi saba wa nyumbani mwa mfalme ili wamhudumie. Pia akamhamisha yeye na vijakazi wake akawaweka mahali pazuri katika nyumba ya wanawake. Naye Esta hakudhihirisha kabila yake wala jamaa yake, kwa maana ndivyo alivyomwagiza Mordekai asiwadhihirishe. Na yule Mordekai akawa akitembea kila siku mbele ya ua wa nyumba ya wanawake, ili ajue hali yake Esta, na yale yatakayompata.
Esta 2:7-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo mzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake yeye. Basi ikawa, wakati iliposikiwa amri ya mfalme na mbiu yake, wasichana wengi wakakusanyika huko Shushani ngomeni mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake. Yule mwanamwali akampendeza, akapokea fadhili kwake; naye akampa upesi vifaa vya utakaso, pamoja na posho zake, na vijakazi saba walio haki yake, wa nyumbani mwa mfalme. Pia akamhamisha yeye na vijakazi wake akawaweka mahali pazuri katika nyumba ya wanawake. Walakini Esta hakudhihirisha kabila yake wala jamaa yake, kwa maana ndivyo alivyomwagiza Mordekai asiwadhihirishe. Na yule Mordekai akawa akitembea kila siku mbele ya ua wa nyumba ya wanawake, ili ajue hali yake Esta, na hayo yatakayompata.
Esta 2:7-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mordekai alikuwa na binamu yake msichana aliyeitwa Hadasa, ambaye alimlea kwa kuwa hakuwa na baba wala mama. Msichana huyu, ambaye pia alijulikana kwa jina la Esta, alikuwa na umbo na sura ya kupendeza, naye Mordekai alimtunza kama binti yake mwenyewe baada ya baba yake na mama yake kufariki. Agizo na amri ya mfalme ilipotangazwa, wanawali wengi waliletwa kwenye ngome ya mji wa Shushani na kuwekwa chini ya uangalizi wa Hegai. Pia Esta alipelekwa katika jumba la mfalme na akakabidhiwa kwa Hegai, aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake. Msichana huyu alimpendeza na kupata kibali mbele zake. Mara moja akaanza kumpa matunzo ya urembo na chakula maalum. Alimpa Esta vijakazi saba waliochaguliwa kutoka jumba la kifalme, na kumhamishia yeye pamoja na vijakazi wake katika sehemu bora zaidi katika nyumba ya wanawake. Esta alikuwa hajadhihirisha uraia wake na asili yake, kwa sababu Mordekai alikuwa amemkataza kufanya hivyo. Kila siku Mordekai alikuwa akitembeatembea karibu na ua wa nyumba ya wanawake kujua Esta alivyoendelea na kuona yaliyokuwa yakitendeka kwake.