Esta 2:20-23
Esta 2:20-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Esta alikuwa bado hajajitambulisha ukoo wala kabila lake kama Mordekai alivyokuwa amemwonya asifanye hivyo; naye Esta alimtii kama alivyokuwa akimtii wakati wa utoto wake, alipolelewa naye. Wakati Mordekai alipokuwa anaketi penye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, wawili baadhi ya matowashi wa mfalme waliokuwa walinzi wa milango ya vyumba vya mfalme, waliudhika kiasi cha kula njama kumuua mfalme Ahasuero. Mordekai aliingamua njama hiyo, akamjulisha malkia Esta, naye Esta akampasha habari mfalme. Uchunguzi ulipofanywa, iligunduliwa kuwa ni kweli; basi, watu hao wawili wakatundikwa kwenye mti wa kuulia. Habari kuhusu tukio hilo iliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.
Esta 2:20-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Esta alikuwa hajadhihirisha jamaa yake wala kabila yake, kama vile Mordekai alivyomwagiza; kwa maana Esta alikuwa akiyashika maagizo ya Mordekai, vile vile kama wakati alipolelewa naye. Ikawa siku zile, Mordekai alipokuwa akiketi mlangoni pa mfalme, wawili kati ya matowashi wake mfalme, Bigthana na Tereshi, waliolinda milango ya vyumba vya mfalme, walikasirika sana, wakataka kumwua mfalme Ahasuero. Basi Mordekai akapata kulijua jambo hilo, naye akamjulisha Esta, malkia; naye Esta akamwambia mfalme habari hiyo kwa jina la Mordekai. Na jambo hilo lilipochunguzwa, na hakika ikapatikana, hao wote wawili wakatundikwa juu ya mti. Hayo pia yakaandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.
Esta 2:20-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Esta alikuwa hajadhihirisha jamaa yake wala kabila yake, kama vile Mordekai alivyomwagiza; kwa maana Esta alikuwa akiyashika maagizo ya Mordekai, vile vile kama wakati alipolelewa naye. Ikawa siku zile, Mordekai alipokuwa akiketi mlangoni pa mfalme, wawili katika wasimamizi wake mfalme, Bigthana na Tereshi, wangoje mlango, walighadhibika, wakataka kumpelekea mikono mfalme Ahasuero. Basi Mordekai akapata kulijua jambo hilo, naye akamjulisha Esta, malkia; naye Esta akamwambia mfalme habari hiyo kwa jina la Mordekai. Na jambo hilo lilipochunguzwa, na hakika ikapatikana, hao wote wawili wakatundikwa juu ya mti. Hayo pia yakaandikwa katika kitabu cha taarifa mbele ya mfalme.
Esta 2:20-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini Esta alikuwa ameficha siri ya asili yake na uraia wake, kama Mordekai alivyokuwa amemwambia, kwa maana aliendelea kufuata maelekezo ya Mordekai kama alivyokuwa akifanya alipokuwa akimlea. Ikawa Mordekai alipokuwa ameketi kwenye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, maafisa wawili wa mfalme waliokuwa walinzi wa lango, walikasirika na kupanga njama ya kumuua Mfalme Ahasuero. Lakini Mordekai aligundua hila hii na kumwambia Malkia Esta, ambaye baadaye alimwarifu mfalme, huku akimsifu Mordekai. Taarifa hiyo ilipochunguzwa na kuonekana kuwa kweli, maafisa hao wawili waliangikwa juu ya miti ya kunyongea. Haya yote yaliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.