Esta 1:4-11
Esta 1:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, kwa muda wa miezi sita, Ahasuero akaonesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na fahari ya utawala wake. Muda huo ulipomalizika, mfalme aliwaandalia karamu watu wote wa mji mkuu wa Susa, wakubwa kwa wadogo. Karamu hiyo iliyochukua muda wa siku saba, ilifanyika uani, katika bustani ya ikulu. Mahali hapo palikuwa pamepambwa kwa mapazia ya pamba ya rangi nyeupe na vitambaa vya rangi ya buluu. Mapazia hayo yalikuwa yamefungiwa pete za fedha kwa kamba za kitani safi za zambarau, na kuninginizwa kwenye nguzo za marumaru. Makochi ya dhahabu na fedha yalikuwa yamewekwa kwenye sakafu iliyotengenezwa kwa vijiwe vya rangi, marumaru, lulumizi na mawe ya thamani. Watu walipewa vinywaji katika vikombe mbalimbali vya dhahabu, naye mfalme alikuwa mkarimu sana wa divai ya kifalme. Kila mtu alikunywa akashiba; mfalme alikuwa ametoa maagizo kwa watumishi wa ikulu wamhudumie kila mtu kadiri ya mahitaji yake. Wakati huo huo, malkia Vashti naye aliwaandalia akina mama karamu ndani ya ikulu ya Ahasuero. Siku ya saba ya karamu hiyo, mfalme Ahasuero, akiwa amejaa furaha kutokana na divai aliyokuwa amekunywa, aliwaita matowashi saba waliomhudumia yeye binafsi: Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi. Aliwaamuru hao wamlete kwake malkia Vashti, akiwa amevaa taji yake ya kimalkia. Malkia huyo alikuwa na sura ya kuvutia sana, hivyo mfalme alitaka kuwaonesha wageni wake na viongozi uzuri wake.
Esta 1:4-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaonesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na heshima ya enzi yake bora siku nyingi, yaani siku mia moja na themanini. Hata siku hizo zilipotimia, mfalme akawafanyia karamu watu wote waliokuwapo huko Shushani mji mkuu, wakubwa kwa wadogo, muda wa siku saba, katika ukumbi wa bustani ya ngome ya mfalme. Palikuwa na mapazia ya bafta, nyeupe na samawati, yamefungiwa kamba za kitani safi za rangi ya zambarau kwa pete za fedha na nguzo za marumaru; pia na vitanda vilikuwa vya dhahabu na fedha juu ya sakafu yenye nakshi ya vito vyekundu, marumaru, lulu za manjano na nyeusi na mawe ya thamani. Wakawanywesha kileo katika vyombo mbalimbali vya dhahabu, na divai tele ya kifalme, kufuatana na ukarimu wa ufalme; Walikunywa kama ilivyoamriwa, bila kushurutishwa; maana mfalme aliwaagiza watumishi wahudumie kila mtu kadiri ya mahitaji yake. Naye Vashti, malkia, akawafanyia karamu wanawake ndani ya nyumba ya kifalme ya mfalme Ahasuero. Katika siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale Matowashi saba, wasimamizi wa nyumba saba waliohudumu mbele zake, wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, akiwa amevaa taji la kifalme; ili kuwaonesha watu na wakuu uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso.
Esta 1:4-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaonyesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na heshima ya enzi yake bora siku nyingi, maana siku mia na themanini. Hata siku hizo zilipotimia, mfalme akawafanyia karamu watu wote waliokuwapo huko Shushani ngomeni, wakubwa kwa wadogo, muda wa siku saba, katika behewa la bustani ya ngome ya mfalme. Palikuwa na mapazia ya bafta, nyeupe na samawi, yamefungiwa kamba za kitani safi za rangi ya zambarau kwa pete za fedha na nguzo za marumaru; pia na vitanda vilikuwa vya dhahabu na fedha juu ya sakafu ya marumaru, mawe mekundu, na meupe, na ya manjano, na meusi. Wakawanywesha kileo katika vyombo vya dhahabu, na vile vyombo vilikuwa mbalimbali, na divai tele ya namna ya kifalme, sawasawa na ukarimu wa mfalme; kunywa kulikuwa kama ilivyoamriwa, bila sharti; maana ndivyo mfalme alivyowaagiza watumishi-wa-nyumbani, kila mtu afanye apendavyo. Tena Vashti, malkia, naye akawafanyia karamu wanawake ndani ya nyumba ya kifalme ya mfalme Ahasuero. Hata siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale wasimamizi-wa-nyumba saba waliohudumu mbele za mfalme Ahasuero, wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, amevaa taji ya kifalme; ili kuwaonyesha watu na maakida uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso.
Esta 1:4-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa muda wa siku mia moja na themanini mfalme alionesha utajiri mwingi wa ufalme wake, fahari na utukufu wa enzi yake. Siku hizo zilipopita, mfalme alifanya karamu kwa muda wa siku saba, katika bustani ya ndani katika jumba la kifalme, kwa ajili ya watu wote kuanzia mdogo hadi mkubwa, waliokuwa katika ngome ya mji wa Shushani. Bustani ilikuwa na mapazia ya kitani nyeupe na buluu, yaliyofungiwa kamba za kitani nyeupe na kitambaa cha zambarau, kwenye pete za fedha juu ya nguzo za marumaru. Kulikuwa na viti vya dhahabu na vya fedha vilivyokuwa vimewekwa kwenye ile sakafu iliyotengenezwa kwa mawe ya rangi, marumaru, lulumizi na mawe mengine ya thamani. Vyombo vya dhahabu vilitumika kwa watu kunywea mvinyo, kila kimoja tofauti na kingine, naye mfalme akatoa mvinyo kwa wingi kwa kadiri ya ukarimu wake. Kwa amri ya mfalme kila mgeni aliruhusiwa kunywa alichotaka, kwa kuwa mfalme alitoa maagizo kwa watumishi wote kugawa mvinyo kila mtu kwa jinsi alivyotaka. Malkia Vashti pia akawafanyia wanawake karamu katika jumba la kifalme la Mfalme Ahasuero. Siku ya saba, wakati Mfalme Ahasuero alikuwa amesisimka roho yake kwa mvinyo, aliamuru matowashi saba waliokuwa wakimhudumia, yaani Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi, kumleta Malkia Vashti mbele ya mfalme akiwa amevaa taji lake la kifalme, ili aoneshe uzuri wake kwa watu na wakuu, kwa kuwa alikuwa ni mzuri kumtazama.