Esta 1:10-18
Esta 1:10-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya saba ya karamu hiyo, mfalme Ahasuero, akiwa amejaa furaha kutokana na divai aliyokuwa amekunywa, aliwaita matowashi saba waliomhudumia yeye binafsi: Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi. Aliwaamuru hao wamlete kwake malkia Vashti, akiwa amevaa taji yake ya kimalkia. Malkia huyo alikuwa na sura ya kuvutia sana, hivyo mfalme alitaka kuwaonesha wageni wake na viongozi uzuri wake. Lakini matowashi hao walipomweleza malkia amri ya mfalme, Vashti alikataa kutii. Jambo hilo lilimwudhi sana mfalme, akawa anawaka hasira moyoni. Ilikuwa desturi ya mfalme kupata mawaidha kutoka kwa wenye hekima, hivyo aliwaita wanasheria na mahakimu ili wamshauri la kufanya. Washauri wake wa kawaida walikuwa Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Maresi, Marsena na Memukani – viongozi saba wa Persia na Media waliokuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake. Aliwauliza hivi: “Je, kulingana na sheria, afanyiwe nini malkia Vashti? Maana, nimewatuma matowashi wangu kwake, lakini yeye amekataa kuitii amri yangu, mimi mfalme Ahasuero!” Hapo Memukani akamwambia mfalme na viongozi wake, “Licha ya kumkosea mfalme, malkia Vashti amewakosea viongozi na kila mtu katika mikoa ya mfalme Ahasuero! Tendo hili la malkia Vashti litajulikana na wanawake wote, nao watawadharau waume zao, wakisema: ‘Mfalme Ahasuero aliamuru malkia Vashti aje kwake, lakini yeye akakataa.’ Leo hii, mabibi wa Persia na Media ambao wamesikia alivyofanya malkia Vashti, watakuwa wanawaeleza viongozi wako; hivyo dharau na chuki vitajaa kila mahali.
Esta 1:10-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale Matowashi saba, wasimamizi wa nyumba saba waliohudumu mbele zake, wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, akiwa amevaa taji la kifalme; ili kuwaonesha watu na wakuu uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso. Bali Vashti, malkia, hakutii amri ya mfalme, alikataa kuja kama alivyoamriwa na mfalme kupitia kwa matowashi; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake. Basi mfalme akawaambia wenye hekima, waliojua sheria; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu; na karibu naye wameketi Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale wakuu saba wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme; akawauliza, Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi wa nyumba? Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na wakuu, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na wakuu wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero. Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja. Hata na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliozisikia habari za tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maofisa wote wa mfalme. Hivyo kutatokea dharau nyingi na ghadhabu tele.
Esta 1:10-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale wasimamizi-wa-nyumba saba waliohudumu mbele za mfalme Ahasuero, wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, amevaa taji ya kifalme; ili kuwaonyesha watu na maakida uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso. Bali Vashti, malkia, alikataa kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake. Basi mfalme akawaambia wenye hekima, walio na elimu ya nyakati; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu; na karibu naye wameketi Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale maakida saba wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme; akawauliza, Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba? Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na maakida, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na maakida wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero. Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja. Hata na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliokwisha kuzisikia habari za tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maakida wote wa mfalme. Hivyo kutatokea dharau nyingi na ghadhabu tele.
Esta 1:10-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku ya saba, wakati Mfalme Ahasuero alikuwa amesisimka roho yake kwa mvinyo, aliamuru matowashi saba waliokuwa wakimhudumia, yaani Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi, kumleta Malkia Vashti mbele ya mfalme akiwa amevaa taji lake la kifalme, ili aoneshe uzuri wake kwa watu na wakuu, kwa kuwa alikuwa ni mzuri kumtazama. Lakini wakati watumishi walipotoa amri ya mfalme, Malkia Vashti alikataa kuja. Ndipo mfalme alighadhibika, na hasira yake ikawaka. Kwa kuwa ilikuwa desturi ya mfalme kupata ushauri kwa wataalamu katika mambo ya sheria na haki, alizungumza na watu wenye busara, ambao walijua nyakati, nao waliokuwa karibu na mfalme ni Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena na Memukani, wakuu saba wa Uajemi na Umedi waliokuwa na nafasi ya pekee kwa mfalme nao walikuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake. Mfalme akauliza, “Kulingana na sheria, Malkia Vashti anapaswa kutendewa nini? Malkia hakutii amri ya Mfalme Ahasuero ambayo matowashi walimpelekea.” Kisha Memukani akajibu mbele ya mfalme na wakuu, “Malkia Vashti si kwamba amemkosea mfalme tu bali pia amewakosea wakuu wote na watu wa himaya yote ya Mfalme Ahasuero. Kwa maana tendo hili la malkia litajulikana kwa wanawake wote, kwa hiyo watawadharau waume zao na kusema, ‘Mfalme Ahasuero aliagiza Malkia Vashti aletwe mbele yake, lakini alikataa.’ Siku ya leo, wanawake wa wakuu wa Uajemi na Umedi ambao wamesikia kuhusu tabia ya malkia watawatendea wakuu wote wa mfalme vivyo hivyo. Hapatakuwa na mwisho wa dharau na ugomvi.