Waefeso 3:1-13
Waefeso 3:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Kutokana na hayo, mimi Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu, namwomba Mungu. Bila shaka mmekwisha sikia kwamba Mungu, kwa neema yake, alinikabidhi kazi hii niifanye kwa faida yenu. Mimi nilijulishwa kwa njia ya ufunuo mpango wake uliofichika. (Nimeandika kwa ufupi juu ya jambo hili, nanyi mkiyasoma maneno yangu mtaweza kujua jinsi ninavyoielewa siri hiyo ya Kristo). Zamani watu hawakujulishwa siri hiyo; lakini sasa Mungu amewajulisha mitume na manabii wake watakatifu kwa njia ya Roho. Siri yenyewe ni hii: Kwa njia ya Injili watu wa mataifa mengine wanapata sehemu yao pamoja na Wayahudi katika zile baraka za Mungu; wao ni viungo vya mwili uleule, na wanashiriki ahadi ileile aliyofanya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Mimi nimefanywa kuwa mtumishi wa Injili kwa neema ya pekee aliyonijalia Mungu kwa uwezo wake mkuu. Mimi ni mdogo kuliko watu wote wa Mungu; lakini amenijalia neema yake, ili niwahubirie watu wa mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; tena niwaangazie watu wote waone jinsi mpango wa Mungu uliofichika unavyotekelezwa. Mungu aliye Muumba wa vitu vyote alificha hiyo siri yake tangu milele, kusudi sasa, kwa njia ya kanisa, wakuu na wenye enzi wa mbinguni wapate kuitambua hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi. Mungu alifanya jambo hilo kufuatana na azimio lake la milele ambalo amelifanya kwa njia ya Kristo Yesu Bwana wetu. Basi, kwa kuungana na Kristo na kwa imani kwake, sisi tunathubutu kumwendea Mungu kwa matumaini. Kwa hiyo, nawaombeni msife moyo kwa sababu ya mateso ninayopata kwa ajili yenu, maana hayo ni kwa ajili ya utukufu wenu.
Waefeso 3:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa; ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nilijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache. Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii nyakati hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; Injili hiyo ambayo nilifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake. Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nilipewa neema hii ya kuwahubiria Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini. Basi naomba msikate tamaa kwa sababu ya dhiki zangu kwa ajili yenu, zilizo utukufu wenu.
Waefeso 3:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa; ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache. Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake. Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini. Basi naomba msikate tamaa kwa sababu ya dhiki zangu kwa ajili yenu, zilizo utukufu kwenu.
Waefeso 3:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa sababu hii, mimi Paulo, ni mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi watu wa Mataifa. Kwa hakika mmekwisha kusikia kuhusu ile huduma ya neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu, yaani ile siri iliodhihirishwa kwangu kupitia ufunuo, kama nilivyotangulia kuandika kwa kifupi. Kwa kusoma haya, basi mtaweza kuelewa ufahamu wangu katika siri ya Kristo. Siri hii haikudhihirishwa kwa wanadamu katika vizazi vingine kama vile sasa ilivyodhihirishwa na Roho kwa mitume na manabii watakatifu wa Mungu. Siri hii ni kwamba, kupitia kwa Injili, watu wa Mataifa ni warithi pamoja na Israeli, viungo vya mwili mmoja na washiriki pamoja wa ahadi katika Kristo Yesu. Nimekuwa mtumishi wa Injili hii kwa kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa nguvu yake itendayo kazi. Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii: ili niwahubirie watu wa Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Kristo, na kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa tangu zamani katika Mungu, aliyeumba vitu vyote. Ili sasa kupitia kwa kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho, sawasawa na kusudi lake la milele alilolitimiza katika Kristo Yesu Bwana wetu. Ndani yake na kupitia kwa imani katika yeye twaweza kumkaribia Mungu kwa uhuru na kwa ujasiri. Kwa hiyo, nawaomba msikate tamaa kwa sababu ya mateso yangu kwa ajili yenu, hayo ni utukufu wenu.