Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mhubiri 8:2-15

Mhubiri 8:2-15 Biblia Habari Njema (BHN)

Tii amri ya mfalme, kwa sababu ya kiapo chako kitakatifu. Usifanye haraka kuondoka mbele yake; wala usiwe na kiburi juu ya jambo baya, maana mfalme hufanya apendavyo. Amri ya mfalme ni kauli ya mwisho; nani athubutuye kumwuliza, “Unafanya nini?” Anayetii amri hatapata madhara, na mwenye hekima atajua kuna wakati na njia. Naam, kila kitu kina wakati wake na njia yake, ingawa binadamu anakabiliwa na tatizo kubwa: Hajui ni nini kitakachotukia baadaye, kwani nani awezaye kumjulisha yatakayotukia baadaye? Hakuna mtu aliye na uwezo wa kushikilia roho yake asife; hakuna mtu aliye na uwezo juu ya siku ya kufa. Wakati wa vita hakuna kuponyoka, na uovu hauwezi kumwokoa mwovu. Haya yote nimeyaona katika uchunguzi wangu juu ya yote yanayotendwa hapa duniani, binadamu anapokuwa na uwezo wa kumkandamiza na kumdhuru binadamu mwenzake. Tena, nimewaona waovu wakizikwa, na watu waliporudi kutoka mahali patakatifu wanawasifu humohumo mjini walimotenda maovu yao. Hayo nayo ni bure kabisa. Kwa vile uovu haupatilizwi haraka, mioyo ya wanadamu hupania kutenda mabaya. Wenye dhambi hutenda maovu mara mia, hata hivyo, huendelea kuishi. Walakini, mimi najua kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, kwa sababu ya uchaji wao; lakini hakuna furaha kwa waovu. Wao watapita kama kivuli, maisha yao hayatakuwa marefu kwa sababu hawamchi Mungu. Kuna jambo moja, bure kabisa nililoligundua hapa duniani: Watu wema hutendewa wastahilivyo waovu, nao waovu hutendewa wastahilivyo watu wema. Hili nalo nasema ni bure kabisa. Basi, mimi nasisitiza kuwa mtu ni lazima afaidi raha, kwa kuwa hapa duniani hakuna kilicho kizuri zaidi kuliko kula na kunywa na kujifurahisha. Hayo ndio awezayo kufanya mtu anaposhughulika na kazi katika muda wa maisha yake aliyojaliwa na Mungu duniani.

Shirikisha
Soma Mhubiri 8

Mhubiri 8:2-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mimi nasema hivi, Uishike amri ya mfalme; na hiyo kwa sababu umeapa kwa Mungu. Usifanye haraka kutoka mbele ya uso wake; usiendelee kufanya lililo baya; maana yeye hufanya lolote limpendezalo. Kwa kuwa neno la mfalme lina nguvu; naye ni nani awezaye kumwambia huyo, Wafanya nini? Aishikaye amri hatajua neno baya; Na moyo wa mwenye hekima hujua wakati na hukumu. Kwa maana kwa kila shauri kuna wakati na hukumu; kwa sababu mashaka ya mwanadamu yaliyo juu yake ni makubwa; kwa kuwa hajui yatakayokuwako; kwa maana ni nani awezaye kumweleza jinsi yatakavyokuwa? Hakuna mwenye uwezo juu ya roho aizuie roho; Wala hana mamlaka juu ya siku ya kufa; Wala hakuna kuponyoka katika vita vile; Wala uovu hautamwokoa yule aliyeuzoea. Mambo hayo yote nimeyaona, nikatia moyo wangu katika kila kazi iliyofanyika chini ya jua. Kuna wakati ambapo mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasira yake. Pia nikaona waovu wamezikwa, nao wamefika kaburini; tena waliofanya mema wameondoka katika patakatifu, nao wamesahauliwa mjini. Hayo nayo ni ubatili. Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu huthibitishwa ndani yao ili kutenda mabaya. Ijapokuwa mwenye dhambi amefanya maovu mara mia na akazidisha siku zake; lakini hata hivyo najua hakika ya kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, wenye kicho mbele zake; lakini haitakuwa heri kwa mwovu, wala hatazidisha siku zake, zilizo kama kivuli; kwa sababu hana kicho mbele za Mungu. Kuna ubatili unaofanyika juu ya nchi, kwamba wako wenye haki nao wapatilizwa kama kwa kazi yao waovu; tena wako waovu, nao wapatilizwa kama kwa kazi yao wenye haki. Nami nikasema ya kuwa hayo nayo ni ubatili. Kisha nikaisifu furaha, kwa sababu mwanadamu hana neno lolote lililo jema chini ya jua, kuliko kula, kunywa, na kujifurahisha; maana hili atakaa nalo katika amali yake, siku zote za maisha yake alizompa Mungu chini ya jua.

Shirikisha
Soma Mhubiri 8

Mhubiri 8:2-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mimi nasema hivi, Uishike amri ya mfalme; na hiyo kwa sababu umeapa kwa Mungu. Usifanye haraka kutoka mbele ya uso wake; usiendelee kufanya lililo baya; maana yeye hufanya lo lote limpendezalo. Kwa kuwa neno la mfalme lina nguvu; naye ni nani awezaye kumwambia huyo, Wafanya nini? Aishikaye amri hatajua neno baya; Na moyo wa mwenye hekima hujua wakati na hukumu. Kwa maana kwa kila shauri kuna wakati na hukumu; kwa sababu mashaka ya mwanadamu yaliyo juu yake ni makubwa; kwa kuwa hajui yatakayokuwako; kwa maana ni nani awezaye kumweleza jinsi yatakavyokuwa? Hakuna mwenye uwezo juu ya roho aizuie roho; Wala hana mamlaka juu ya siku ya kufa; Wala hakuna kuruhusiwa katika vita vile; Wala uovu hautamwokoa yule aliyeuzoea. Mambo hayo yote nimeyaona, nikatia moyo wangu katika kila kazi iliyofanyika chini ya jua. Kuna wakati ambapo mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasira yake. Pia nikaona waovu wamezikwa, nao wamefika kaburini; tena waliofanya mema wameondoka katika patakatifu, nao wamesahauliwa mjini. Hayo nayo ni ubatili. Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu huthibitishwa ndani yao ili kutenda mabaya. Ajapokuwa mwenye dhambi amefanya maovu mara mia, akazidisha siku zake; lakini hata hivyo najua hakika ya kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, wenye kicho mbele zake; walakini haitakuwa heri kwa mwovu, wala hatazidisha siku zake, zilizo kama kivuli; kwa sababu hana kicho mbele za Mungu. Kuna ubatili unaofanyika juu ya nchi, kwamba wako wenye haki nao wapatilizwa kama kwa kazi yao waovu; tena wako waovu, nao wapatilizwa kama kwa kazi yao wenye haki. Nami nikasema ya kuwa hayo nayo ni ubatili. Kisha nikaisifu furaha, kwa sababu mwanadamu hana neno lo lote lililo jema chini ya jua, kuliko kula, na kunywa, na kucheka; na yakuwa hilo likae naye katika amali yake, siku zote za maisha yake alizompa Mungu chini ya jua.

Shirikisha
Soma Mhubiri 8

Mhubiri 8:2-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Nawaambia, Tii amri ya mfalme, kwa sababu uliapa mbele za Mungu. Usiharakishe kuondoka mbele ya mfalme. Usiendelee kutenda lililo baya, kwa maana mfalme atafanya lolote apendalo. Kwa kuwa neno la mfalme ndilo lenye mamlaka ya mwisho, nani awezaye kumwambia, “Je, wewe unafanya nini?” Yeyote anayetii agizo lake hatadhurika, moyo wa hekima utajua wakati muafaka na jinsi ya kutenda. Kwa maana kuna wakati muafaka na utaratibu wa kila jambo, ingawa huzuni ya mwanadamu huwa nzito juu yake. Kwa vile hakuna mtu ajuaye siku zijazo, ni nani awezaye kumwambia linalokuja? Hakuna mwanadamu awezaye kushikilia roho yake asife, wala hakuna mwenye uwezo juu ya siku ya kufa kwake. Kama vile hakuna yeyote arudishwaye nyuma wakati wa vita, kadhalika uovu hautawaweka huru wale wautendao. Yote haya niliyaona, nilipokuwa natafakari kila kitu kinachotendeka chini ya jua. Kuna wakati mtu hujifanya bwana juu ya wengine kwa madhara yake mwenyewe. Ndipo pia nikaona waovu wakizikwa, wale waliozoea kuingia na kutoka mahali patakatifu na kupewa sifa katika mji ambao waliyafanya haya. Hili nalo ni ubatili. Wakati hukumu juu ya tendo ovu haitekelezwi upesi, mioyo ya watu hujaa mipango ya kutenda maovu. Ingawa mtu mwovu hufanya maovu mia moja na akaendelea kuishi maisha marefu, najua kwamba itakuwa bora zaidi kwa watu wanaomwogopa Mungu, wamchao Mungu. Lakini kwa sababu waovu hawamwogopi Mungu, hawatafanikiwa, maisha yao hayatarefuka kama kivuli. Kuna kitu kingine ambacho ni ubatili kinachofanyika duniani: Watu waadilifu kupata yale yanayowastahili waovu, nao waovu kupata yale yanayowastahili waadilifu. Hili nalo pia, nasema ni ubatili. Kwa hiyo mimi ninasifu kufurahia maisha, kwa sababu hakuna kitu bora zaidi kwa mwanadamu chini ya jua kuliko kula, kunywa na kufurahi. Kisha furaha itafuatana naye kazini mwake siku zote za maisha yake ambazo amepewa na Mungu chini ya jua.

Shirikisha
Soma Mhubiri 8