Mhubiri 8:1-9
Mhubiri 8:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Nani aliye kama mwenye hekima? Nani ajuaye hali halisi ya vitu? Hekima humletea mtu tabasamu, huubadilisha uso wake mwenye huzuni. Tii amri ya mfalme, kwa sababu ya kiapo chako kitakatifu. Usifanye haraka kuondoka mbele yake; wala usiwe na kiburi juu ya jambo baya, maana mfalme hufanya apendavyo. Amri ya mfalme ni kauli ya mwisho; nani athubutuye kumwuliza, “Unafanya nini?” Anayetii amri hatapata madhara, na mwenye hekima atajua kuna wakati na njia. Naam, kila kitu kina wakati wake na njia yake, ingawa binadamu anakabiliwa na tatizo kubwa: Hajui ni nini kitakachotukia baadaye, kwani nani awezaye kumjulisha yatakayotukia baadaye? Hakuna mtu aliye na uwezo wa kushikilia roho yake asife; hakuna mtu aliye na uwezo juu ya siku ya kufa. Wakati wa vita hakuna kuponyoka, na uovu hauwezi kumwokoa mwovu. Haya yote nimeyaona katika uchunguzi wangu juu ya yote yanayotendwa hapa duniani, binadamu anapokuwa na uwezo wa kumkandamiza na kumdhuru binadamu mwenzake.
Mhubiri 8:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ni nani aliye kama mwenye hekima; Naye ni nani ajuaye kufasiri neno? Hekima ya mtu humwangaza uso wake, Na ugumu wa uso wake hubadilika. Mimi nasema hivi, Uishike amri ya mfalme; na hiyo kwa sababu umeapa kwa Mungu. Usifanye haraka kutoka mbele ya uso wake; usiendelee kufanya lililo baya; maana yeye hufanya lolote limpendezalo. Kwa kuwa neno la mfalme lina nguvu; naye ni nani awezaye kumwambia huyo, Wafanya nini? Aishikaye amri hatajua neno baya; Na moyo wa mwenye hekima hujua wakati na hukumu. Kwa maana kwa kila shauri kuna wakati na hukumu; kwa sababu mashaka ya mwanadamu yaliyo juu yake ni makubwa; kwa kuwa hajui yatakayokuwako; kwa maana ni nani awezaye kumweleza jinsi yatakavyokuwa? Hakuna mwenye uwezo juu ya roho aizuie roho; Wala hana mamlaka juu ya siku ya kufa; Wala hakuna kuponyoka katika vita vile; Wala uovu hautamwokoa yule aliyeuzoea. Mambo hayo yote nimeyaona, nikatia moyo wangu katika kila kazi iliyofanyika chini ya jua. Kuna wakati ambapo mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasira yake.
Mhubiri 8:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ni nani aliye kama mwenye hekima; Naye ni nani ajuaye kufasiri neno? Hekima ya mtu humng’ariza uso wake, Na ugumu wa uso wake hubadilika. Mimi nasema hivi, Uishike amri ya mfalme; na hiyo kwa sababu umeapa kwa Mungu. Usifanye haraka kutoka mbele ya uso wake; usiendelee kufanya lililo baya; maana yeye hufanya lo lote limpendezalo. Kwa kuwa neno la mfalme lina nguvu; naye ni nani awezaye kumwambia huyo, Wafanya nini? Aishikaye amri hatajua neno baya; Na moyo wa mwenye hekima hujua wakati na hukumu. Kwa maana kwa kila shauri kuna wakati na hukumu; kwa sababu mashaka ya mwanadamu yaliyo juu yake ni makubwa; kwa kuwa hajui yatakayokuwako; kwa maana ni nani awezaye kumweleza jinsi yatakavyokuwa? Hakuna mwenye uwezo juu ya roho aizuie roho; Wala hana mamlaka juu ya siku ya kufa; Wala hakuna kuruhusiwa katika vita vile; Wala uovu hautamwokoa yule aliyeuzoea. Mambo hayo yote nimeyaona, nikatia moyo wangu katika kila kazi iliyofanyika chini ya jua. Kuna wakati ambapo mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasira yake.
Mhubiri 8:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ni nani aliye kama mtu mwenye hekima? Ni nani ajuaye maelezo ya mambo? Hekima hungʼarisha uso wa mtu na kubadili ugumu wa uso wake. Nawaambia, Tii amri ya mfalme, kwa sababu uliapa mbele za Mungu. Usiharakishe kuondoka mbele ya mfalme. Usiendelee kutenda lililo baya, kwa maana mfalme atafanya lolote apendalo. Kwa kuwa neno la mfalme ndilo lenye mamlaka ya mwisho, nani awezaye kumwambia, “Je, wewe unafanya nini?” Yeyote anayetii agizo lake hatadhurika, moyo wa hekima utajua wakati muafaka na jinsi ya kutenda. Kwa maana kuna wakati muafaka na utaratibu wa kila jambo, ingawa huzuni ya mwanadamu huwa nzito juu yake. Kwa vile hakuna mtu ajuaye siku zijazo, ni nani awezaye kumwambia linalokuja? Hakuna mwanadamu awezaye kushikilia roho yake asife, wala hakuna mwenye uwezo juu ya siku ya kufa kwake. Kama vile hakuna yeyote arudishwaye nyuma wakati wa vita, kadhalika uovu hautawaweka huru wale wautendao. Yote haya niliyaona, nilipokuwa natafakari kila kitu kinachotendeka chini ya jua. Kuna wakati mtu hujifanya bwana juu ya wengine kwa madhara yake mwenyewe.