Mhubiri 7:1-14
Mhubiri 7:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Sifa njema ni bora kuliko marashi ya thamani. Siku ya kufa ni bora kuliko siku ya kuzaliwa. Afadhali kwenda kwenye matanga, kuliko kwenda kwenye karamu, kwa sababu walio hai yawapasa kukumbuka kwamba kifo chatungojea sisi sote. Huzuni ni afadhali kuliko kicheko maana, huzuni ya uso ni faida ya moyo. Moyo wa mwenye hekima huthamini matanga, lakini moyo wa mpumbavu hupenda raha. Afadhali kusikia maonyo ya wenye hekima kuliko kusikiliza nyimbo za wapumbavu. Maana, kicheko cha mpumbavu ni kama mlio wa miiba motoni. Hayo nayo ni bure kabisa. Mwenye hekima akimdhulumu mtu; hujifanya mwenyewe kuwa mpumbavu kupokea rushwa hupotosha akili. Mwisho wa jambo ni afadhali kuliko mwanzo wake; mvumilivu rohoni ni bora kuliko mwenye majivuno. Usiwe mwepesi wa hasira, maana, hasira hukaa ndani ya wapumbavu. Usiulize, “Kwa nini nyakati za kale zilikuwa bora kuliko za sasa?” Huulizi hivyo kwa kutumia hekima. Hekima ni ya thamani kubwa kama urithi; ni muhimu kwa wale wote walio hai. Kulindwa na hekima ni kama kulindwa na fedha. Faida ya maarifa ni kwamba hekima hulinda maisha ya mtu aliye nayo. Tafakarini vema kazi yake Mungu; ni nani awezaye kunyosha alichopinda Mungu? Katika siku za fanaka uwe na furaha; katika siku za maafa utafakari jambo hili: Fanaka, pia maafa, Mungu amefanya hiyo ya kwanza iambatane na ya pili ili binadamu asiweze kujua yatakayotukia baada yake.
Mhubiri 7:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Heri sifa njema kuliko manukato ya thamani; Na siku ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa. Heri kuiendea nyumba ya matanga, Kuliko kuiendea nyumba ya karamu. Kwa maana huo ndio mwisho wa wanadamu wote, naye aliye hai atautia moyoni mwake. Huzuni ni afadhali kuliko kicheko, Maana simanzi ya uso ni faida ya moyo. Moyo wake mwenye hekima umo nyumbani mwa matanga, bali moyo wake mpumbavu umo nyumbani mwa furaha. Heri kusikia laumu ya wenye hekima, Kuliko mtu kusikia wimbo wa wapumbavu; Maana kama mlio wa miiba chini ya sufuria, Ndivyo kilivyo kicheko cha mpumbavu. Hayo nayo ni ubatili. Kweli jeuri humpumbaza mwenye hekima, Na rushwa huuharibu ufahamu. Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi. Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu. Usiseme, Kwa nini siku za kale zilikuwa ni bora kuliko siku hizi? Maana si kwa hekima unauliza hili. Hekima ni njema kama urithi; Naam, nayo ni bora kwao walionalo jua. Kwa maana ulinzi wa hekima ni kama ulinzi wa fedha na ubora wa maarifa ni kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo. Tafakari vema kazi yake Mungu; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye? Siku ya kufanikiwa ufurahi, Na siku ya mabaya ufikiri. Mungu ameifanya hiyo moja kwenda sambamba na hiyo ya pili, ili mwanadamu asipate kulijua neno lolote litakalofuata baada yake.
Mhubiri 7:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Heri sifa njema kuliko marhamu nzuri; Na siku ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa. Heri kuiendea nyumba ya matanga, Kuliko kuiendea nyumba ya karamu. Kwa maana huo ndio mwisho wa wanadamu wote, naye aliye hai atautia moyoni mwake. Huzuni ni afadhali kuliko kicheko, Maana simanzi ya uso ni faida ya moyo. Moyo wake mwenye hekima umo nyumbani mwa matanga, bali moyo wake mpumbavu umo nyumbani mwa furaha. Heri kusikia laumu ya wenye hekima, Kuliko mtu kusikia wimbo wa wapumbavu; Maana kama mlio wa miiba chini ya sufuria, Ndivyo kilivyo kicheko cha mpumbavu. Hayo nayo ni ubatili. Kweli jeuri humpumbaza mwenye hekima, Na rushwa huuharibu ufahamu. Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi. Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu. Usiseme, Kwani siku za kale kupita siku hizi? Maana si kwa hekima uulizavyo neno hilo. Hekima ni njema, mfano wa urithi; Naam, nayo ni bora kwao walionao jua. Kwa maana hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi; na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo. Tafakari vema kazi yake Mungu; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye? Siku ya kufanikiwa ufurahi, Na siku ya mabaya ufikiri. Mungu ameifanya hiyo moja kwenda sambamba na hiyo ya pili, ili mwanadamu asipate kulijua neno lo lote litakalofuata baada yake.
Mhubiri 7:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Afadhali sifa nzuri kuliko manukato safi, nayo siku ya kufa kuliko ya kuzaliwa. Afadhali kwenda kwenye nyumba ya msiba kuliko kwenda kwenye nyumba ya karamu, kwa kuwa kifo ni hatima ya kila mwanadamu, imewapasa walio hai kuliweka hili mioyoni mwao. Huzuni ni afadhali kuliko kicheko, kwa sababu uso wenye huzuni wafaa kwa moyo. Moyo wa wenye hekima uko katika nyumba ya msiba, lakini moyo wa wapumbavu uko katika nyumba ya anasa. Afadhali kusikia karipio la mtu mwenye hekima, kuliko kusikiliza wimbo wa wapumbavu. Kama ilivyo kuvunjika kwa miiba chini ya sufuria, ndivyo kilivyo kicheko cha wapumbavu. Hili nalo pia ni ubatili. Dhuluma humfanya mtu mwenye hekima kuwa mpumbavu, nayo rushwa huuharibu moyo. Mwisho wa jambo ni bora kuliko mwanzo wake, uvumilivu ni bora kuliko kiburi. Usiwe mwepesi kukasirika rohoni mwako, kwa kuwa hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu. Usiseme, “Kwa nini siku za kale zilikuwa bora kuliko siku hizi?” Kwa maana si hekima kuuliza maswali kama hayo. Hekima, kama ulivyo urithi, ni kitu chema na huwafaidia wale walionalo jua. Hekima ni ulinzi kama fedha ilivyo ulinzi, lakini faida ya maarifa ni hii: kwamba hekima huhifadhi maisha ya aliye nayo. Tafakari kile Mungu alichokitenda: Nani awezaye kunyoosha kile ambacho yeye amekipinda? Nyakati zikiwa nzuri, ufurahi, lakini nyakati zikiwa mbaya, tafakari hili: Mungu amefanya hiyo moja; naam, pia na hiyo nyingine. Kwa hiyo, mwanadamu hawezi kugundua kitu chochote kuhusu maisha yake ya baadaye.