Mhubiri 6:1-11
Mhubiri 6:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Nimeona jambo moja ovu hapa duniani, linalowakandamiza watu: Mungu humjalia mtu utajiri, mali na heshima, asitindikiwe kitu chochote anachotamani, lakini hampi uwezo wa kuvifurahia vitu hivyo; badala yake, mgeni fulani atavifaidi. Hilo nalo ni bure kabisa; ni jambo la mateso makali. Mtu akiweza kuzaa watoto 100, na akaishi maisha marefu, lakini kama mtu huyo hafurahii maisha yake, wala hafanyiwi mazishi basi nasema mtoto aliyezaliwa amekufa ni afadhali kuliko mtu huyo. Mtoto mfu hafaidiki chochote kwa kuzaliwa; yeye hutokomea gizani, akasahaulika. Zaidi ya hayo, mtoto wa namna hiyo hakupata kuuona mwanga wa jua wala kutambua chochote. Hata hivyo, huyo mtoto angalau hupata pumziko ambapo yule mtu hapati. Ingawa mtu huyo ataishi miaka elfu mbili, lakini hafurahii maisha, basi ni kama huyo mtoto wote wawili huenda mahali pamoja. Kazi yote ya mtu ni kwa ajili ya kupata chakula, lakini tamaa yake ya kula haitoshelezwi kamwe. Je, mtu mwenye hekima anayo nafuu zaidi kuliko mpumbavu? Na mtu maskini hupata faida gani akijua namna ya kuyakabili maisha? Hayo nayo ni bure kabisa; ni sawa na kufukuza upepo. Afadhali kuridhika na ulicho nacho kuliko kuhangaika kwa kutamani kitu kingine. Kila kitu kinachotukia kilikwisha pangwa hapo awali; hali ya binadamu inajulikana, na tunajua kwamba mnyonge hawezi kubishana na mtu mwenye nguvu zaidi. Maneno mengi hayana faida, hayamwinui binadamu.
Mhubiri 6:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kuna baa nililoliona mimi chini ya jua, nalo linawalemea wanadamu kwa uzito; mtu aliyepewa na Mungu mali, ukwasi, na heshima, hata asipungukiwe na kitu chochote kwa nafsi yake, katika yote anayoyatamani lakini Mungu hamwezeshi kula katika hizo; bali mgeni hula. Hayo ndiyo ubatili hasa, nayo ni ugonjwa mbaya. Mtu akizaa watoto mia moja, akaishi miaka mingi, hata siku za maisha yake zikiwa nyingi, lakini nafsi yake haikushiba mema; tena ikiwa, zaidi ya hayo, amekosa maziko; mimi nasema, Heri mimba iliyoharibika kuliko huyo; yaani, hiyo huja katika ubatili, na huenda gizani, nalo jina lake limefunikwa giza; tena, haikuliona jua wala kulifahamu; basi, hii imepata kustarehe kuliko yule; naam, ajapoishi miaka elfu mara mbili, asijiburudishe kwa mema; je! Wote hawaendi mahali pamoja? Juhudi zote za binadamu ni kwa kinywa chake, Lakini hamu yake haitosheleki. Kwa maana mwenye hekima hupata faida gani kuliko mpumbavu? Au maskini ana nini kuliko yeye ajuaye kwenda mbele ya walio hai? Heri kuona kwa macho, Kuliko kutangatanga kwa tamaa. Hayo nayo ni ubatili, na kufukuza upepo. Na awe kitu chochote, aliitwa jina lake zamani za kale, naye amejulikana kuwa ndiye mwanadamu; wala hawezi kabisa kushindana na yeye aliye na uwezo kuliko yeye mwenyewe. Basi, kwa kuwa kuna mambo mengi yaongezayo ubatili, mwanadamu hufaidiwa nini?
Mhubiri 6:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kuna baa nililoliona mimi chini ya jua, nalo linawalemea wanadamu kwa uzito; mtu aliyepewa na Mungu mali, ukwasi, na heshima, hata asipungukiwe na kitu cho chote kwa nafsi yake, katika yote anayoyatamani walakini Mungu hamwezeshi kula katika hizo; bali mgeni hula. Hayo ndiyo ubatili hasa, nayo ni ugonjwa mbaya. Mtu akizaa watoto mia, akaishi miaka mingi, nazo siku za maisha yake ni nyingi, lakini nafsi yake haikushiba mema; tena ikiwa, zaidi ya hayo, amekosa maziko; mimi nasema, Heri mimba iliyoharibika kuliko huyo; yaani, hiyo huja katika ubatili, na huenda gizani, nalo jina lake limefunikwa giza; tena, haikuliona jua wala kulifahamu; basi, hii imepata kustarehe kuliko yule; naam, ajapoishi miaka elfu mara mbili, asijiburudishe kwa mema; je! Wote hawaendi mahali pamoja? Kazi yote ya binadamu ni kwa kinywa chake, Walakini hata hivyo nafsi yake hashibi. Kwa maana mwenye hekima hupata faida gani kuliko mpumbavu? Au maskini ana nini kuliko yeye ajuaye kwenda mbele ya walio hai? Heri kuona kwa macho, Kuliko kutanga-tanga kwa tamaa. Hayo nayo ni ubatili, na kujilisha upepo. Na awe kitu cho chote, aliitwa jina lake zamani za kale, naye amejulikana kuwa ndiye mwanadamu; wala hawezi kabisa kushindana na yeye aliye na uwezo kuliko yeye mwenyewe. Basi, kwa kuwa kuna mambo mengi yaongezayo ubatili, mwanadamu hufaidiwa nini?
Mhubiri 6:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nimeona ubaya mwingine chini ya jua, nao unalemea sana wanadamu: Mungu humpa mwanadamu utajiri, mali na heshima, hivyo hakukosa chochote moyo wake unachokitamani. Lakini Mungu hamwezeshi kuvifurahia, badala yake mgeni ndiye anayevifurahia. Hili ni ubatili, ni ubaya unaosikitisha. Mtu anaweza kuwa na watoto mia moja naye akaishi miaka mingi, lakini haidhuru kuwa ataishi muda mrefu kiasi gani, kama hawezi kufurahia mafanikio yake na kwamba hapati mazishi ya heshima, ninasema afadhali mtoto aliyezaliwa akiwa amekufa kuliko yeye. Kuzaliwa kwake hakuna maana, huondokea gizani na gizani jina lake hufunikwa. Ingawa hakuwahi kuliona jua wala kujua kitu chochote, yeye ana pumziko kuliko mtu huyo: Hata kama huyo mtu ataishi miaka elfu mara mbili na zaidi, lakini akashindwa kufurahia mafanikio yake, je, wote hawaendi sehemu moja? Juhudi zote za binadamu ni kwa ajili ya kinywa chake, hata hivyo hamu yake kamwe haitoshelezwi. Mtu mwenye hekima ana faida gani zaidi ya mpumbavu? Mtu maskini anapata faida gani kwa kujua jinsi ya kujistahi mbele ya watu wengine? Ni bora kile ambacho jicho linakiona kuliko hamu isiyotoshelezwa. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo. Lolote lililopo limekwisha kupewa jina, naye mwanadamu alivyo ameshajulikana; hakuna mtu awezaye kushindana na mwenye nguvu kuliko yeye. Maneno yanavyokuwa mengi, ndivyo yanavyokosa maana, Je, hilo linamfaidia vipi yeyote?