Mhubiri 5:10-16
Mhubiri 5:10-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Apendaye fedha hatatosheka na fedha; wala atamaniye mali hata akiipata hatatosheka. Hilo nalo ni bure kabisa. Ongezeko la mali huleta ongezeko la walaji, naye mwenye mali yamfaa nini isipokuwa kuitazama tu mali yake? Usingizi wa kibarua ni mtamu, awe ameshiba au amekula kidogo tu. Lakini usingizi wa tajiri ni wa wasiwasi daima, maana ziada ya mali yake humsumbua usiku kucha. Tena, nimeona jambo moja ovu sana duniani: Mtu alijirundikia mali ikawa hatari kwake. Kwa bahati mbaya, mali hiyo iliharibiwa katika matumizi mabaya, mwisho, mtu huyo hakuwa na chochote mkononi na alikuwa na mwana. Kama vile binadamu alivyokuja duniani uchi toka tumboni mwa mama yake, ndivyo atakavyorudi uchi huko alikotoka. Hataweza kuchukua hata sehemu ndogo ya mapato ya kazi yake. Hili nalo ni jambo baya sana. Atarudi kama alivyokuja. Amejisumbua kufukuza upepo, akatoka jasho bure.
Mhubiri 5:10-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba nyongeza. Hayo pia ni ubatili. Mali yakiongezeka, hao walao nao wanaongezeka na mwenyewe hufaidiwa nini, ila kuyatazama kwa macho yake tu? Usingizi wake kibarua ni mtamu, awe amekula kidogo, au awe amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi. Kuna balaa mbaya sana niliyoiona chini ya jua, nayo ni hii, mali alizoziweka mwenyewe kwa kujinyima; na mali hizo zimepotea kwa bahati mbaya; naye akiwa amezaa mwana, hamna kitu mkononi mwake. Alivyotoka tumboni mwa mamaye, atakwenda tena tuputupu kama alivyokuja; asichume kitu chochote kwa ajili ya kazi yake, hata akichukue mkononi mwake. Hiyo ndiyo balaa mbaya sana, ya kwamba kama vile alivyokuja, vivyo hivyo atakwenda zake; naye amefaidiwa nini mwenye kujitaabisha kwa ajili ya upepo?
Mhubiri 5:10-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba nyongeza. Hayo pia ni ubatili. Mali yakiongezeka, hao walao nao waongezeka na mwenyewe hufaidiwa nini, ila kuyatazama kwa macho yake tu? Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi. Kuna na balaa mbaya sana niliyoiona chini ya jua, nayo ni hii, mali alizoziweka mwenyewe kwa kujinyima; na mali hizo zimepotea kwa bahati mbaya; naye akiwa amezaa mwana, hamna kitu mkononi mwake. Alivyotoka tumboni mwa mamaye, atakwenda tena tupu-tupu kama alivyokuja; asichume kitu cho chote kwa ajili ya kazi yake, hata akichukue mkononi mwake. Hiyo ndiyo balaa mbaya sana, ya kwamba kama vile alivyokuja, vivyo hivyo atakwenda zake; naye amefaidiwa nini mwenye kujitaabisha kwa ajili ya upepo?
Mhubiri 5:10-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yeyote apendaye fedha kamwe hatosheki na fedha; yeyote apendaye utajiri kamwe hatosheki na kipato chake. Hili nalo pia ni ubatili. Mali ikiongezeka, ndivyo walaji wanavyoongezeka. Hii nayo inamfaidia nini mwenye mali isipokuwa ni kushibisha macho yake? Usingizi wa kibarua ni mtamu, awe amekula kidogo au kingi, lakini wingi wa mali humnyima tajiri usingizi. Nimeshaona uovu mzito chini ya jua: Utajiri uliolimbikizwa na kuleta madhara kwa mwenye mali; au utajiri uliopotea kwa bahati mbaya, kiasi kwamba wakati akiwa na mwana hakuna chochote kilichobaki kwa ajili yake. Mtu hutoka tumboni mwa mama yake uchi, naye jinsi alivyokuja vivyo hivyo huondoka. Hachukui chochote kutokana na kazi yake ambacho anaweza kukibeba mkononi mwake. Hili nalo ni baya la kusikitisha: Kama vile mtu ajavyo, vivyo hivyo huondoka, naye anapata faida gani, maadamu hutaabika kwa ajili ya upepo?