Mhubiri 4:4-8
Mhubiri 4:4-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Tena niligundua kwamba juhudi zote za mtu na ujuzi wake katika kazi vyatokana na kuoneana wivu. Hayo nayo ni bure kabisa; ni sawa na kufukuza upepo. Mpumbavu hafanyi kazi na mwisho hujiua kwa njaa. Ni afadhali kuwa na kidogo tu, pamoja na amani moyoni, kuliko kuwa na mengi, pamoja na taabu; sawa tu na kufukuza upepo. Tena, niliona jambo moja bure kabisa duniani. Nilimwona mtu mmoja asiye na mwana wala ndugu; hata hivyo, haachi kufanya kazi; hatosheki kamwe na mali yake; wala hatulii na kujiuliza: “Ninamfanyia nani kazi na kujinyima starehe?” Hilo nalo ni bure kabisa; ni shughuli inayosikitisha.
Mhubiri 4:4-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena nikagundua kuwa juhudi zote, na ustadi wote katika kazi, hutokana na mtu kumwonea mwingine wivu. Hayo nayo ni ubatili na kufukuza upepo. Mpumbavu huikunja mikono yake, Naye hula chakula chake mwenyewe; Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kufukuza upepo. Kisha nikarudi tena, na kuona ubatili chini ya jua. Kuna mtu aliye peke yake, wala hana mwenzi wake; naam, hana mwana wala ndugu; hata hivyo amali yake haina mwisho, wala macho yake hayashibi utajiri. Basi asema, Ni kwa ajili ya nani nafanya kazi, na kujinyima nafsi yangu mema? Hayo nayo ni ubatili, naam, ni taabu kubwa.
Mhubiri 4:4-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena nikafikiri amali zote, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana na mwenzake. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo. Mpumbavu huikunja mikono yake, Naye hula chakula chake mwenyewe; Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kujilisha upepo. Kisha nikarudi tena, na kuona ubatili chini ya jua. Kuna mtu aliye peke yake, wala hana wa pili wake; naam, hana mwana wala ndugu; hata hivyo amali yake haina mwisho, wala macho yake hayashibi utajiri. Basi asema, Ni kwa ajili ya nani nafanya kazi, na kujinyima nafsi yangu mema? Hayo nayo ni ubatili, naam, ni taabu kubwa.
Mhubiri 4:4-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Tena nikaona kuwa kazi zote na mafanikio yote huchipuka kutokana na wivu wa mtu kwa jirani yake. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo. Mpumbavu hukunja mikono yake na kujiangamiza mwenyewe. Afadhali konzi moja pamoja na utulivu kuliko konzi mbili pamoja na taabu na kukimbiza upepo. Tena nikaona kitu kingine kilicho ubatili chini ya jua: Kulikuwa na mtu aliye peke yake, hakuwa na mwana wala ndugu. Hapakuwa na mwisho wa kazi yake; hata hivyo macho yake hayakutosheka na utajiri wake. Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani, nami kwa nini ninajinyima kufurahia?” Hili pia ni ubatili, ni shughuli yenye taabu!