Mhubiri 4:1-16
Mhubiri 4:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha nikaona udhalimu wote unaofanyika duniani. Watu wanaokandamizwa hulia machozi, lakini hakuna yeyote anayewafariji. Wakandamizaji wao wana nguvu, ndiyo sababu hakuna wa kuwafariji. Basi, nikafikiri moyoni kuwa wafu waliokwenda wasikorudi, wana nafuu zaidi kuliko watu walio hai. Lakini ana heri zaidi kuliko wafu na walio hai, yule ambaye bado hajazaliwa na kuona maovu yote yanayotendwa hapa duniani. Tena niligundua kwamba juhudi zote za mtu na ujuzi wake katika kazi vyatokana na kuoneana wivu. Hayo nayo ni bure kabisa; ni sawa na kufukuza upepo. Mpumbavu hafanyi kazi na mwisho hujiua kwa njaa. Ni afadhali kuwa na kidogo tu, pamoja na amani moyoni, kuliko kuwa na mengi, pamoja na taabu; sawa tu na kufukuza upepo. Tena, niliona jambo moja bure kabisa duniani. Nilimwona mtu mmoja asiye na mwana wala ndugu; hata hivyo, haachi kufanya kazi; hatosheki kamwe na mali yake; wala hatulii na kujiuliza: “Ninamfanyia nani kazi na kujinyima starehe?” Hilo nalo ni bure kabisa; ni shughuli inayosikitisha. Ni afadhali kuwa wawili kuliko mtu kuwa peke yake. Kwa sababu wawili watapata tuzo la kazi yao. Ikijatokea mmoja akaanguka, huyo mwenzake atamwinua. Lakini ole wake aliye peke yake akianguka! Huyo hatakuwa na mtu wa kumwinua! Hali kadhalika, wawili wakilala pamoja watapata joto; lakini mtu akiwa peke yake atajipatiaje joto? Mtu akiwa peke yake aweza kushindwa na adui, lakini wakiwa wawili watamkabili na kumshinda adui. Kamba tatu zikisokotwa pamoja hazikatiki kwa urahisi. Afadhali kijana maskini mwenye hekima kuliko mfalme mzee mpumbavu, ambaye hasikilizi shauri jema; hata ikiwa alikuwa mfungwa na sasa ni mfalme, au alizaliwa maskini na sasa ni mfalme. Niliwaona watu wote waishio duniani, hata yule kijana ambaye angechukua nafasi ya mfalme. Idadi ya watu haikuwa na kikomo, naye aliwatawala wote. Hata hivyo, wale wanaozaliwa baadaye hawatamfurahia. Hakika hayo nayo ni bure kabisa na kufukuza upepo.
Mhubiri 4:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha nikarudi na kuona udhalimu wote unaotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, lakini wale walikuwa hawana mfariji. Kwa hiyo nikawasifu wafu waliokwisha kufa kuliko wenye uhai walio hai bado; naam, zaidi ya hao wote nikamwita heri yeye asiyekuwako bado, ambaye hakuyaona mabaya yanayotendeka chini ya jua. Tena nikagundua kuwa juhudi zote, na ustadi wote katika kazi, hutokana na mtu kumwonea mwingine wivu. Hayo nayo ni ubatili na kufukuza upepo. Mpumbavu huikunja mikono yake, Naye hula chakula chake mwenyewe; Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kufukuza upepo. Kisha nikarudi tena, na kuona ubatili chini ya jua. Kuna mtu aliye peke yake, wala hana mwenzi wake; naam, hana mwana wala ndugu; hata hivyo amali yake haina mwisho, wala macho yake hayashibi utajiri. Basi asema, Ni kwa ajili ya nani nafanya kazi, na kujinyima nafsi yangu mema? Hayo nayo ni ubatili, naam, ni taabu kubwa. Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Kwa sababu wana tuzo njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kupata moto? Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watamstahimili; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi. Heri kijana maskini mwenye hekima Kuliko mfalme mzee mpumbavu ambaye hajui tena kupokea maonyo. Kwa maana anaweza kutoka gerezani kutawala; hata ikiwa alizaliwa akiwa maskini katika ufalme. Nikawaona wote walio hai waendao chini ya jua, ya kwamba walishikamana na huyo kijana, huyo wa pili aliyesimama badala ya mfalme. Hawakuwa na kikomo hao watu wote, hao wote ambao alikuwa juu yao; lakini hata hivyo wale wafuatao baada yake hawatamfurahia. Hakika hayo pia ni ubatili, na kufukuza upepo.
Mhubiri 4:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha nikarudi na kuona madhalimu yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, walakini wale walikuwa hawana mfariji. Kwa hiyo nikawasifu wafu waliokwisha kufa kuliko wenye uhai walio hai bado; naam, zaidi ya hao wote nikamwita heri yeye asiyekuwako bado, ambaye hakuyaona mabaya yanayotendeka chini ya jua. Tena nikafikiri amali zote, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana na mwenzake. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo. Mpumbavu huikunja mikono yake, Naye hula chakula chake mwenyewe; Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kujilisha upepo. Kisha nikarudi tena, na kuona ubatili chini ya jua. Kuna mtu aliye peke yake, wala hana wa pili wake; naam, hana mwana wala ndugu; hata hivyo amali yake haina mwisho, wala macho yake hayashibi utajiri. Basi asema, Ni kwa ajili ya nani nafanya kazi, na kujinyima nafsi yangu mema? Hayo nayo ni ubatili, naam, ni taabu kubwa. Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto? Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi. Heri kijana maskini mwenye hekima Kuliko mfalme mzee mpumbavu. ambaye hajui tena kupokea maonyo. Kwa maana kutoka gerezani alikuja kumiliki; naam, hata katika ufalme wake alizaliwa hali ya umaskini. Nikawaona wote walio hai waendao chini ya jua, ya kwamba walishikamana na huyo kijana, huyo wa pili aliyesimama badala ya yule. Hawakuwa na kikomo hao watu wote, hao wote ambao alikuwa juu yao; lakini hata hivyo wale wafuatao baada yake hawatamfurahia. Hakika hayo pia ni ubatili, na kujilisha upepo.
Mhubiri 4:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nikatazama tena nikaona uonevu wote uliokuwa unafanyika chini ya jua: Nikaona machozi ya waliodhulumiwa, wala hawana mfariji; uwezo ulikuwa upande wa wale wanaowadhulumu, lakini hawakuwa na mfariji. Nami nikasema kwamba wafu, waliokwisha kufa, wana furaha kuliko watu walio hai, ambao bado wanaishi. Lakini aliye bora kuliko hao wawili ni yule ambaye hajazaliwa bado, ambaye hajaona ule uovu unaofanyika chini ya jua. Tena nikaona kuwa kazi zote na mafanikio yote huchipuka kutokana na wivu wa mtu kwa jirani yake. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo. Mpumbavu hukunja mikono yake na kujiangamiza mwenyewe. Afadhali konzi moja pamoja na utulivu kuliko konzi mbili pamoja na taabu na kukimbiza upepo. Tena nikaona kitu kingine kilicho ubatili chini ya jua: Kulikuwa na mtu aliye peke yake, hakuwa na mwana wala ndugu. Hapakuwa na mwisho wa kazi yake; hata hivyo macho yake hayakutosheka na utajiri wake. Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani, nami kwa nini ninajinyima kufurahia?” Hili pia ni ubatili, ni shughuli yenye taabu! Wawili ni afadhali kuliko mmoja, kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao: Kama mmoja akianguka, mwenzake atamwinua. Lakini ni jambo la kuhuzunisha kwa mtu yule aangukaye naye hana wa kumwinua! Pia, kama wawili wakilala pamoja watapashana joto. Lakini ni vipi mtu aweza kujipasha joto mwenyewe? Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa, watu wawili wanaweza kumkabili adui na kumshinda. Kamba ya nyuzi tatu haikatiki kwa urahisi. Afadhali kijana maskini mwenye hekima kuliko mfalme mzee mpumbavu ambaye hajui tena kupokea maonyo. Kijana huyo angeweza kutokea gerezani akapata ufalme, au angeweza kuwa amezaliwa katika umaskini kwenye huo ufalme. Nikaona kwamba wote walioishi na kutembea chini ya jua walimfuata kijana, aliyepokea ufalme. Hapakuwa na kikomo cha watu wote aliowatawala. Lakini wale waliokuja baadaye hawakufurahia kazi ya yule aliyepokea ufalme. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.