Mhubiri 2:1-8
Mhubiri 2:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, nikawaza; “Ngoja nijitumbukize katika starehe, nijifurahishe.” Lakini, niligundua kwamba kufanya hivyo ni bure kabisa. Nikasema kuhusu kicheko, “Ni wazimu”, na starehe “Mna faida gani?” Nilifikiria sana, namna ya kujichangamsha akili kwa divai, huku nikisukumwa na ari yangu ya kupata hekima; pia namna ya kuandamana na upumbavu ili nione yaliyo bora kabisa ambayo wanadamu wanaweza wakafanya waishipo maisha yao mafupi hapa duniani. Nilifanya mambo makuu: Nilijenga majumba na kujilimia mashamba ya mizabibu. Nilijifanyia bustani na viunga, nikapanda miti ya matunda ya kila aina. Nilijichimbia mabwawa ya maji ya kumwagilia hiyo miti. Nilinunua watumwa, wanawake kwa wanaume, na wengine wakazaliwa nyumbani mwangu. Nilikuwa na mali nyingi, makundi ya ng'ombe na kondoo wengi kuliko mtu yeyote aliyenitangulia kukaa Yerusalemu. Nilijirundikia fedha na dhahabu kutoka hazina za wafalme na toka mikoani, nami nilipata waimbaji wanaume kwa wanawake, na masuria watamaniwao.
Mhubiri 2:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili. Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini? Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ungali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao. Nikajifanyia mambo makuu; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu; nikajifanyia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna; nikajifanyia mabwawa ya maji, ya kuunyweshea msitu mlimopandwa miti michanga. Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na watumwa waliozaliwa nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng'ombe na kondoo, kuliko wote walionitangulia katika Yerusalemu; tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, wanaume kwa wanawake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana.
Mhubiri 2:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili. Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini? Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ukali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao. Nikajifanyizia kazi zilizo kubwa; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu; nikajifanyizia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna; nikajifanyizia birika za maji, ya kuunyweshea mwitu mlimopandwa miti michanga. Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na wazalia nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng’ombe na kondoo, kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, waume kwa wake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana.
Mhubiri 2:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nikafikiri moyoni mwangu, “Haya basi, nitakujaribu kwa anasa nione ni lipi lililo jema.” Lakini hilo nalo likaonekana ni ubatili. Nikasema, “Kicheko nacho ni upumbavu. Nayo matokeo ya anasa ni nini?” Nikajaribu kujifurahisha kwa mvinyo na kukumbatia upumbavu, huku bado akili yangu inaniongoza kwa hekima. Nilitaka kuona ni lipi bora watu wafanye kwa siku chache wanazoishi chini ya mbingu. Nikafanya miradi mikubwa: Nikajijengea majumba na kulima mashamba ya mizabibu. Nikatengeneza bustani na viwanja vya starehe; nikaotesha huko kila aina ya miti ya matunda. Nikajenga mabwawa ya kukusanya maji ya kunyweshea hii miti iliyokuwa inastawi vizuri. Nikanunua watumwa wa kiume na wa kike, nao watumwa wengine walizaliwa nyumbani mwangu. Pia nilikuwa na makundi ya ngʼombe, kondoo na mbuzi kuliko mtu yeyote aliyewahi kuishi Yerusalemu kabla yangu. Nikajikusanyia fedha na dhahabu, hazina za wafalme na za majimbo. Nikajipatia waimbaji wanaume na wanawake, nazo nyumba za masuria: vitu ambavyo moyo wa mwanadamu hufurahia.