Mhubiri 2:1-26
Mhubiri 2:1-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, nikawaza; “Ngoja nijitumbukize katika starehe, nijifurahishe.” Lakini, niligundua kwamba kufanya hivyo ni bure kabisa. Nikasema kuhusu kicheko, “Ni wazimu”, na starehe “Mna faida gani?” Nilifikiria sana, namna ya kujichangamsha akili kwa divai, huku nikisukumwa na ari yangu ya kupata hekima; pia namna ya kuandamana na upumbavu ili nione yaliyo bora kabisa ambayo wanadamu wanaweza wakafanya waishipo maisha yao mafupi hapa duniani. Nilifanya mambo makuu: Nilijenga majumba na kujilimia mashamba ya mizabibu. Nilijifanyia bustani na viunga, nikapanda miti ya matunda ya kila aina. Nilijichimbia mabwawa ya maji ya kumwagilia hiyo miti. Nilinunua watumwa, wanawake kwa wanaume, na wengine wakazaliwa nyumbani mwangu. Nilikuwa na mali nyingi, makundi ya ng'ombe na kondoo wengi kuliko mtu yeyote aliyenitangulia kukaa Yerusalemu. Nilijirundikia fedha na dhahabu kutoka hazina za wafalme na toka mikoani, nami nilipata waimbaji wanaume kwa wanawake, na masuria watamaniwao. Naam, nikawa mkuu, mkuu kuwapita wote waliopata kuwako Yerusalemu kabla yangu; na hekima yangu ikakaa ndani mwangu. Kila macho yangu yalichokitamani nilikipata. Moyo wangu sikuunyima raha yoyote ile; kwa kuwa moyo wangu ulifurahia niliyotenda, na hili lilikuwa tuzo la jasho langu. Kisha nikafikiria yote niliyokuwa nimefanya kwa mikono yangu, jinsi nilivyotoa jasho katika kufanya hayo. Nikagundua kwamba yote yalikuwa bure kabisa; ilikuwa ni sawa na kufukuza upepo, hapakuwapo faida yoyote chini ya mbingu. Basi, nikaanza kufikiria maana ya kuwa na hekima, kuwa mwendawazimu, na kuwa mpumbavu. Nilijiuliza, “Mtawala mpya anaweza kufanya kitu gani?” Basi, mimi nikagundua kwamba hekima ni bora kuliko upumbavu, kama mwanga ulivyo bora kuliko giza. Mwenye hekima anayo macho, huona aendako, lakini mpumbavu hutembea gizani. Hata hivyo, nikatambua kwamba mwenye hekima na mpumbavu mwisho wao ni uleule. Basi, nikasema moyoni mwangu, “Yatakayompata mpumbavu yatanipata na mimi pia. Kwa nini, basi, nimekuwa na hekima kiasi chote hiki?” Nikajibu, nikiwaza, “Hayo nayo ni bure kabisa.” Maana hakuna amkumbukaye mwenye hekima, wala amkumbukaye mpumbavu, kwani siku zijazo wote watasahaulika. Jinsi mwenye hekima afavyo ndivyo afavyo mpumbavu! Kwa hiyo, nikayachukia maisha, maana yote yatendekayo duniani yalinisikitisha. Yote yalikuwa bure kabisa; nilikuwa nikifukuza upepo. Nilichukia kazi yangu yote niliyokuwa nimefanya hapa duniani, kuona kwamba ilinipasa nimwachie mtu ambaye atatawala baada yangu. Tena, ni nani ajuaye kwamba atakuwa mwenye hekima au atakuwa mpumbavu? Hata hivyo, yeye atamiliki yote niliyofanya kwa kutumia hekima yangu hapa duniani. Pia hayo yote ni bure kabisa. Basi, nilipofikiria tena juu ya yote niliyofanya duniani, nilikata tamaa. Maana, wakati mwingine mtu ambaye amefanya kazi kwa kutumia hekima, akili na maarifa yake, humwachia mtu mwingine afurahie matunda ya kazi ambayo hakuitolea jasho. Pia hilo nalo ni bure kabisa; ni jambo baya sana. Mtu anafaidi nini kutokana na kazi zake zote, na juhudi anazohangaika nazo duniani? Kwa sababu maisha yake yote yamejaa taabu, na kazi yake ni mahangaiko matupu; hata usiku akili yake haipumziki! Hayo nayo ni bure kabisa. Hakuna chema kimfaacho binadamu, isipokuwa kula na kunywa na kuifurahia kazi yake. Hili nalo nimeliona kuwa latoka kwa Mungu, maana usipojaliwa na Mungu, huwezi kupata chakula wala kujifurahisha. Mungu humjalia mtu apendezwaye naye hekima, akili na furaha; lakini humpa mwenye dhambi kazi ya kuvuna na kurundika, kisha akampa anayempendeza yeye Mungu. Yote hayo pia ni bure kabisa; ni sawa na kufukuza upepo.
Mhubiri 2:1-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili. Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini? Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ungali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao. Nikajifanyia mambo makuu; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu; nikajifanyia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna; nikajifanyia mabwawa ya maji, ya kuunyweshea msitu mlimopandwa miti michanga. Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na watumwa waliozaliwa nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng'ombe na kondoo, kuliko wote walionitangulia katika Yerusalemu; tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, wanaume kwa wanawake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana. Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo. Wala sikuyanyima macho yangu chochote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yoyote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote. Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kufukuza upepo, wala faida hakuna chini ya jua. Nikageuka ili kuipambanua hekima, na wazimu na upumbavu. Kwa maana mtu amfuataye mfalme afanye nini? Lilo hilo tu lililokwisha kufanywa. Ndipo nilipoona ya kuwa kweli hekima hupita upumbavu, kwa kadiri nuru ipitavyo giza; macho yake mwenye hekima yamo kichwani mwake, lakini mpumbavu huenda gizani; ila hata hivyo nikatambua ya kwamba ni tukio moja la mwisho liwapatalo wote sawasawa. Nikasema moyoni mwangu, Kama limpatavyo mpumbavu, ndivyo litakavyonipata mimi nami; basi, kwa nini nikawa na hekima zaidi? Nikasema moyoni mwangu ya kuwa hayo nayo ni ubatili. Maana hakuna kumbukumbu la milele la mwenye hekima, wala la mpumbavu; kwa sababu siku zijazo wote pia watakuwa wamekwisha kusahauliwa. Na mwenye hekima, jinsi gani anavyokufa sawasawa na mpumbavu! Basi, nikauchukia uhai; kwa sababu kazi inayotendeka chini ya jua ilikuwa mbaya kwangu; yaani, mambo yote ni ubatili na kufukuza upepo. Nami nikaichukia kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua; maana sina budi kumwachia yeye atakayenifuata. Naye ni nani ajuaye kama huyo atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo atatawala juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo, ambamo ndani yake mimi nimeonesha hekima chini ya jua. Hayo nayo ni ubatili. Kwa hiyo nikageuka kukata tamaa moyoni mwangu juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua. Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu. Kwa maana mtu hupata nini kwa kazi yake yote, na kwa juhudi ya moyo wake alivyojitahidi chini ya jua? Kwa kuwa siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni; naam, hata usiku moyoni mwake hamna raha. Hayo nayo ni ubatili. Mwanadamu hapati jema kupita kula na kunywa, na kuiburudisha roho yake kwa mema katika kazi yake. Hayo nayo niliona ya kwamba hutoka mkononi mwa Mungu. Kwa maana ni nani awezaye kula au kujiburudisha kuliko mimi? Kwa sababu Mungu humpa yeye aliyemridhia hekima na maarifa na furaha; bali mkosaji humpa taabu, ili kukusanya na kututa, apate kumpa huyo ambaye Mungu amridhia. Hayo nayo ni ubatili na kufukuza upepo.
Mhubiri 2:1-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili. Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini? Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ukali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao. Nikajifanyizia kazi zilizo kubwa; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu; nikajifanyizia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna; nikajifanyizia birika za maji, ya kuunyweshea mwitu mlimopandwa miti michanga. Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na wazalia nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng’ombe na kondoo, kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, waume kwa wake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana. Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo. Wala sikuyanyima macho yangu cho chote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yo yote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote. Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kujilisha upepo, wala faida hakuna chini ya jua. Nikageuka ili kuipambanua hekima, na wazimu na upumbavu. Kwa maana mtu amfuataye mfalme afanye nini? Lilo hilo tu lililokwisha kufanywa. Ndipo nilipoona ya kuwa kweli hekima hupita upumbavu, kwa kadiri nuru ipitavyo giza; macho yake mwenye hekima yamo kichwani mwake, lakini mpumbavu huenda gizani; ila hata hivyo nikatambua ya kwamba ni tukio moja la mwisho liwapatalo wote sawasawa. Nikasema moyoni mwangu, Kama limpatavyo mpumbavu, ndivyo litakavyonipata mimi nami; basi, kwa nini nikawa na hekima zaidi? Nikasema moyoni mwangu ya kuwa hayo nayo ni ubatili. Maana hakuna kumbukumbu la milele la mwenye hekima, wala la mpumbavu; kwa sababu siku zijazo wote pia watakuwa wamekwisha kusahauliwa. Na mwenye hekima, jinsi gani anavyokufa sawasawa na mpumbavu! Basi, nikauchukia uhai; kwa sababu kazi inayotendeka chini ya jua ilikuwa mbaya kwangu; yaani, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo. Nami nikaichukia kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua; maana sina budi kumwachia yeye atakayenifuata. Naye ni nani ajuaye kama huyo atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo atatawala juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo, ambamo ndani yake mimi nimeonyesha hekima chini ya jua. Hayo nayo ni ubatili. Kwa hiyo nikageuka kukata tamaa moyoni mwangu juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua. Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu. Kwa maana mtu hupata nini kwa kazi yake yote, na kwa juhudi ya moyo wake alivyojitahidi chini ya jua? Kwa kuwa siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni; naam, hata usiku moyoni mwake hamna raha. Hayo nayo ni ubatili. Mwanadamu hapati jema kupita kula na kunywa, na kuiburudisha roho yake kwa mema katika kazi yake. Hayo nayo naliona ya kwamba hutoka mkononi mwa Mungu. Kwa maana ni nani awezaye kula au kujiburudisha kuliko mimi? Kwa sababu Mungu humpa yeye aliyemridhia hekima na maarifa na furaha; bali mkosaji humpa taabu, ili kukusanya na kututa, apate kumpa huyo ambaye Mungu amridhia. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo.
Mhubiri 2:1-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nikafikiri moyoni mwangu, “Haya basi, nitakujaribu kwa anasa nione ni lipi lililo jema.” Lakini hilo nalo likaonekana ni ubatili. Nikasema, “Kicheko nacho ni upumbavu. Nayo matokeo ya anasa ni nini?” Nikajaribu kujifurahisha kwa mvinyo na kukumbatia upumbavu, huku bado akili yangu inaniongoza kwa hekima. Nilitaka kuona ni lipi bora watu wafanye kwa siku chache wanazoishi chini ya mbingu. Nikafanya miradi mikubwa: Nikajijengea majumba na kulima mashamba ya mizabibu. Nikatengeneza bustani na viwanja vya starehe; nikaotesha huko kila aina ya miti ya matunda. Nikajenga mabwawa ya kukusanya maji ya kunyweshea hii miti iliyokuwa inastawi vizuri. Nikanunua watumwa wa kiume na wa kike, nao watumwa wengine walizaliwa nyumbani mwangu. Pia nilikuwa na makundi ya ngʼombe, kondoo na mbuzi kuliko mtu yeyote aliyewahi kuishi Yerusalemu kabla yangu. Nikajikusanyia fedha na dhahabu, hazina za wafalme na za majimbo. Nikajipatia waimbaji wanaume na wanawake, nazo nyumba za masuria: vitu ambavyo moyo wa mwanadamu hufurahia. Nikawa maarufu sana kuliko mtu mwingine yeyote aliyepata kuishi Yerusalemu kabla yangu. Katika haya yote bado nikawa nina hekima. Sikujinyima kitu chochote ambacho macho yangu yalikitamani, hakuna anasa niliyounyima moyo wangu. Moyo wangu ulifurahia kazi zangu zote, hii ilikuwa thawabu ya kazi zangu zote. Hata hivyo nilipokuja kuangalia yote ambayo mikono yangu ilikuwa imefanya na yale niliyotaabika kukamilisha, kila kitu kilikuwa ni ubatili, ni kukimbiza upepo; hapakuwa na faida yoyote chini ya jua. Kisha nikageuza mawazo yangu kufikiria hekima, wazimu na upumbavu. Ni nini zaidi mtu anayetawala baada ya mfalme anachoweza kufanya ambacho hakijafanywa? Nikaona kuwa hekima ni bora kuliko upumbavu, kama vile nuru ilivyo bora kuliko giza. Mtu mwenye hekima ana macho katika kichwa chake, lakini mpumbavu anatembea gizani; lakini nikaja kuona kwamba wote wawili hatima yao inafanana. Kisha nikafikiri moyoni mwangu, “Hatima ya mpumbavu itanipata mimi pia. Nitafaidi nini basi kwa kuwa na hekima?” Nikasema moyoni mwangu, “Hili nalo ni ubatili.” Kwa maana kwa mtu mwenye hekima, kama ilivyo kwa mpumbavu, hatakumbukwa kwa muda mrefu, katika siku zijazo wote watasahaulika. Kama vile ilivyo kwa mpumbavu, mtu mwenye hekima pia lazima atakufa! Kwa hiyo nikachukia maisha, kwa sababu kazi inayofanyika chini ya jua ilikuwa masikitiko kwangu. Yote hayo ni ubatili, ni kukimbiza upepo. Nikachukia kila kitu nilichokuwa nimetaabikia chini ya jua, kwa sababu ni lazima nimwachie yule ajaye baada yangu. Nani ajuaye kama atakuwa ni mtu mwenye hekima au mpumbavu? Lakini hata hivyo yeye ndiye atakayetawala kazi zote ambazo nimemiminia juhudi na ustadi chini ya jua. Hili nalo ni ubatili. Kwa hiyo moyo wangu ukaanza kukata tamaa juu ya kazi yangu yote niliyoifanya kwa taabu chini ya jua. Kwa kuwa mtu anaweza kufanya kazi yake kwa hekima, maarifa na ustadi, kisha analazimika kuacha vyote alivyo navyo kwa mtu mwingine ambaye hajavifanyia kazi. Hili nalo pia ni ubatili tena ni balaa kubwa. Mtu atapata nini kwa taabu yote na kuhangaika kwa bidii katika kazi anayotaabikia chini ya jua? Siku zake zote kazi yake ni maumivu na masikitiko, hata usiku akili yake haipati mapumziko. Hili nalo pia ni ubatili. Hakuna kitu bora anachoweza kufanya mtu zaidi ya kula na kunywa na kuridhika katika kazi yake. Hili nalo pia, ninaona, latokana na mkono wa Mungu, kwa sababu pasipo yeye, ni nani awezaye kula na kufurahi? Kwa yule mtu anayempendeza Mungu, Mungu humpa hekima, maarifa na furaha, bali kwa mwenye dhambi Mungu humpa kazi ya kukusanya na kuhifadhi utajiri ili Mungu ampe yule anayempenda. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.