Mhubiri 12:1-14
Mhubiri 12:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Umkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku na miaka ambapo utasema: “Sifurahii tena vitu hivyo!” Umkumbuke kabla ya wakati ambapo kwako mwanga wa jua utafifia; mwezi na nyota haviangazi tena, nayo mawingu yametanda tena baada ya mvua. Wakati ambapo mikono inayokulinda inatetemeka, miguu yako imara imepindika, meno yako ya kusagia hayafai kwa uchache, na macho ya kuchungulia dirishani yamefifia. Wakati ambapo milango ya masikio yako imezibika, na sauti za visagio ni hafifu; lakini usiku hata kwa sauti ya ndege utagutuka. Wakati huo utaogopa kupanda mahali pa juu na kutembea barabarani ni kitisho; wakati miti ya mlozi inachanua na panzi wanashiba, lakini wewe hutakuwa na hamu tena. Wakati huo binadamu anapaswa kwenda katika makao yake ya milele, nao waombolezaji watapitapita barabarani. Wakati huo uzi wa dhahabu utakatika, bakuli la dhahabu litapasuka, mtungi wa maji utavunjikia kisimani, kadhalika na gurudumu la kuvutia maji. Nawe vumbi utarudia udongoni ulimotolewa na roho yako itamrudia Mungu aliyeiumba. Mimi Mhubiri nasema: Yote ni bure kabisa! Yote ni bure. Basi, zaidi ya kuwa na hekima yake, Mhubiri aliwafundisha watu ujuzi. Alizipima, akazichunguza na kuzirekebisha methali kwa ustadi mwingi. Mhubiri alijitahidi kupata maneno ya kupendeza, akaandika kwa ufasaha maneno ya kweli. Misemo ya wenye hekima ni kama michokoo na methali zilizokusanywa pamoja na mchungaji mmoja ni kama vigingi vilivyopigiliwa imara ardhini. Zaidi ya hayo, mwanangu, jihadhari! Kuandika vitabu hakuna mwisho na kusoma kwingi huchokesha mwili. Baada ya hayo yote yaliyokwisha semwa bado kuna hili linalotakiwa: Mche Mungu, na uzishike amri zake; kwa sababu hilo ndilo jukumu aliloumbiwa binadamu. Maana, Mungu atahukumu matendo yetu yote, hata yale yanayotendwa kwa siri, yawe mema au mabaya.
Mhubiri 12:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo. Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua; Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetemeka; Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza; Na milango kufungwa katika njia kuu; Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; Na mtu kushtuka kwa sauti ya ndege; Nao binti za kuimba watapunguzwa; Naam, wataogopa kilichoinuka Na vitisho vitakuwapo njiani; Na mlozi utachanua maua; Na panzi atakuwa ni mzigo mzito; Na pilipili hoho itapasuka; Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele, Nao waombolezao wazunguka njiani. Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani; Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa. Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili! Lakini, kwa sababu huyo Mhubiri alikuwa na hekima, aliendelea kuwafundisha watu maarifa, naam, akatafakari, akachunguza, akatunga mithali nyingi. Huyo Mhubiri akachunguza ili apate kuona maneno yapendezayo, na yale yaliyoandikwa kwa unyofu, yaani, maneno ya kweli. Maneno yao wenye hekima huwa mfano wa michokoo; na kama misumari iliyogongomewa sana; ndivyo yalivyo maneno yao walio wakuu wa makusanyiko, ambayo yatoka kwa mchungaji mmoja. Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wowote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili. Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.
Mhubiri 12:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo. Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua; Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza; Na milango kufungwa katika njia kuu; Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; Nao binti za kuimba watapunguzwa; Naam, wataogopa kilichoinuka Na vitisho vitakuwapo njiani; Na mlozi utachanua maua; Na panzi atakuwa ni mzigo mzito; Na pilipili hoho itapasuka; Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele, Nao waombolezao wazunguka njiani. Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani; Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa. Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili! Walakini, kwa sababu huyo Mhubiri alikuwa na hekima, aliendelea kuwafundisha watu maarifa, naam, akatafakari, akatafuta-tafuta, akatunga mithali nyingi. Huyo Mhubiri akatafuta-tafuta ili apate kuona maneno yapendezayo, na yale yaliyoandikwa kwa unyofu, yaani, maneno ya kweli. Maneno yao wenye hekima huwa mfano wa michokoo; na kama misumari iliyogongomewa sana; ndivyo yalivyo maneno yao walio wakuu wa makusanyiko, ambayo yatoka kwa mchungaji mmoja. Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili. Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.
Mhubiri 12:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku za taabu, wala haijakaribia miaka utakaposema, “Mimi sifurahii hiyo”: kabla jua na nuru, nao mwezi na nyota havijatiwa giza, kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua; siku ile walinzi wa nyumba watakapotetemeka, nao watu wenye nguvu watakapojiinamisha, wakati wasagao watakapokoma kwa sababu ya uchache, nao wachunguliao madirishani kutiwa giza; wakati milango ya kuingia barabarani itakapofungwa na sauti ya kusaga kufifia; wakati watu wataamshwa kwa sauti ya ndege, lakini nyimbo zao zote zikififia; wakati watu watakapoogopa kilichoinuka juu na hatari zitakazokuwepo barabarani; wakati mlozi utakapochanua maua na panzi kujikokota nawe usiwe na shauku ya kitu chochote. Ndipo mwanadamu aiendea nyumba yake ya milele nao waombolezaji wakizunguka barabarani. Mkumbuke Muumba wako: kabla haijakatika kamba ya fedha, au bakuli la dhahabu halijavunjika; kabla mtungi kuvunjika kwenye chemchemi, au gurudumu kuvunjika kisimani, nayo mavumbi kurudi ardhini yalikotoka, na roho kurudi kwa Mungu aliyeitoa. Mhubiri asema, “Ubatili! Ubatili! Kila kitu ni ubatili!” Mhubiri hakuwa tu na hekima, bali aliwagawia watu maarifa pia. Alitafakari na kutafiti na akaweka katika utaratibu mithali nyingi. Mhubiri alitafiti ili kupata maneno sahihi na kila alichoandika kilikuwa sawa na kweli. Maneno ya wenye hekima ni kama mchokoro, mithali zao zilizokusanywa pamoja ni kama misumari iliyopigiliwa ikawa imara, yaliyotolewa na Mchungaji mmoja. Zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo. Hakuna mwisho wa kutunga vitabu vingi, nako kusoma sana huuchosha mwili. Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa: Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au baya.