Mhubiri 10:1-20
Mhubiri 10:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Nzi waliokufa husababisha marashi kunuka; upumbavu kidogo hubatilisha hekima na heshima. Moyo wa mwenye hekima humwongoza kutenda yaliyo sawa; lakini mtu mpumbavu moyo wake humpotosha. Hata apitapo njiani, mpumbavu hutambulikana hivyo, humjulisha kila mtu kwamba yeye ni mpumbavu. Mtawala akikuwakia hasira, usijiuzulu; makosa makubwa huweza kufutwa ukiwa mnyenyekevu. Kuna uovu niliogundua hapa duniani, uovu unaosababishwa na watawala: Kwamba wapumbavu wanapewa kazi za madaraka ya juu, na matajiri wanachukua nafasi za mwisho. Nimeona watumwa wanapanda farasi, na wakuu wanatembea kwa miguu kama watumwa. Mchimba shimo hutumbukia mwenyewe, abomoaye ukuta huumwa na nyoka. Mchonga mawe huumizwa nayo, mkata kuni hukabiliwa na hatari. Nguvu nyingi zaidi zahitajika kwa mtumiaji shoka butu lisilonolewa, lakini kutumia hekima humfanya mtu afanikiwe. Nyoka akiuma kabla hajachochewa, mchochezi hahitajiki tena. Maneno ya mwenye hekima humnufaisha asemaye; lakini midomo ya mpumbavu humwangamiza. Mpumbavu huanza kusema kwa maneno ya kijinga, na kumaliza kauli yake kwa wazimu mbaya. Mpumbavu hububujika maneno. Binadamu hajui yatakayokuwako, wala yale yatakayotukia baada yake. Mpumbavu huchoshwa na kazi yake hata asijue njia ya kurudia nyumbani. Ole wako, ewe nchi, mtawala wako akiwa kijana, na viongozi wako wakifanya sherehe asubuhi. Heri yako, ewe nchi, mtawala wako akiwa mtu wa heshima, na viongozi wako wakifanya sherehe wakati wa kufaa, ili kujipatia nguvu na si kujilewesha. Kutokana na uvivu wa mtu, paa hubonyea; kwa sababu ya uzembe, nyumba huvuja. Chakula ni kwa ajili ya kujifurahisha, divai huchangamsha maisha; na fedha husababisha hayo yote. Usimwapize mtawala hata moyoni mwako, wala usimwapize tajiri hata chumbani mwako unakolala, kwa kuwa ndege ataisikia sauti yako, au kiumbe arukaye atatangaza maneno yako.
Mhubiri 10:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nzi waliokufa hufanya manukato ya mwuza marashi kutoa uvundo; Kadhalika upumbavu haba ni mzito kuliko hekima na heshima. Moyo wake mwenye hekima upo upande wa kulia; Bali moyo wake mpumbavu upo mkono wa kushoto. Naam, huyo mpumbavu tena, aendapo njiani, hupungukiwa na fahamu zake; hata humwambia kila mtu ya kuwa yeye ni mpumbavu. Roho yake mtawala ikiinuka kinyume chako, Usiondoke mara mahali pako ulipo; Kwa maana roho ya upole hutuliza machukizo yaliyo makubwa. Liko baa nililoliona chini ya jua, nalo ni kama kosa litokalo kwake yeye atawalaye; ya kuwa upumbavu huwekwa mahali pa juu sana, nao wakwasi hukaa mahali pa chini. Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, na wakuu wakienda kwa miguu juu ya nchi kama watumwa. Mwenye kuchimba shimo atatumbukia ndani yake; Na yeye abomoaye boma, nyoka atamwuma. Mwenye kuchonga mawe ataumizwa kwayo; Naye apasuaye miti huona hatari katika hiyo. Iwapo chuma hakipati, wala mtu hakinoi; Ndipo hana budi kutumia nguvu zaidi. Lakini yafaa kutumia hekima, na kufanikiwa. Nyoka akiuma kabla hajachezeshwa, Basi hakuna faida ya mchezeshaji. Maneno ya kinywa chake mwenye hekima yana neema; Bali midomo ya mpumbavu itammeza nafsi yake. Mwanzo wa maneno ya kinywa chake ni upuuzi; na mwisho wa usemi wake ni wazimu wenye hatari. Tena, upumbavu huongeza maneno; lakini mwanadamu hajui yatakayokuwako; nayo yatakayokuwa baada yake, ni nani awezaye kumweleza? Kazi yao wapumbavu huwachosha kila mmoja, Maana hajui hata njia ya kuuendea mji. Ole wako, nchi, iwapo mfalme wako ni kijana, Na wakuu wako hula asubuhi! Heri kwako, nchi, mfalme wako akiwa mtoto wa watu, Na wakuu wako hula wakati ufaao, Ili makusudi wapate nguvu, wala si kwa ajili ya ulevi. Kwa sababu ya uvivu paa hunepa; Na kwa ulegevu wa mikono nyumba huvuja. Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko, Na divai huyafurahisha maisha; Na fedha huleta jawabu la mambo yote. Usimlaani mfalme, la, hata katika wazo lako; Wala usiwalaani wakwasi chumbani mwako; Kwa kuwa ndege wa anga ataichukua sauti, Na mwenye mabawa ataitoa habari.
Mhubiri 10:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mainzi mafu huvundisha marhamu ya mwuza marashi; Kadhalika upumbavu haba ni mzito kuliko hekima na heshima. Moyo wake mwenye hekima upo upande wa kuume; Bali moyo wake mpumbavu upo mkono wa kushoto. Naam, huyo mpumbavu tena, aendapo njiani, hupungukiwa na fahamu zake; hata humwambia kila mtu ya kuwa yeye ni mpumbavu. Roho yake mtawala ikiinuka kinyume chako, Usiondoke mara mahali pako ulipo; Kwa maana roho ya upole hutuliza machukizo yaliyo makubwa. Liko baa nililoliona chini ya jua, nalo ni kama kosa litokalo kwake yeye atawalaye; ya kuwa upumbavu huwekwa mahali pa juu sana, nao wakwasi hukaa mahali pa chini. Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, na wakuu wakienda kwa miguu juu ya nchi kama watumwa. Mwenye kuchimba shimo atatumbukia ndani yake; Na yeye abomoaye boma, nyoka atamwuma. Mwenye kuchonga mawe ataumizwa kwayo; Naye apasuaye miti huona hatari katika hiyo. Iwapo chuma hakipati, wala mtu hakinoi; Ndipo hana budi kutumia nguvu zaidi. Walakini yafaa kutumia hekima, na kufanikiwa. Nyoka akiuma asijatumbuizwa, Basi hakuna faida ya mtumbuizi. Maneno ya kinywa chake mwenye hekima yana neema; Bali midomo ya mpumbavu itammeza nafsi yake. Mwanzo wa maneno ya kinywa chake ni upuuzi; na mwisho wa usemi wake ni wazimu wenye hatari. Tena, upumbavu huongeza maneno; lakini mwanadamu hajui yatakayokuwako; nayo yatakayokuwa baada yake, ni nani awezaye kumweleza? Kazi yao wapumbavu huwachosha kila mmoja, Maana hajui hata njia ya kuuendea mji. Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana, Na wakuu wako hula asubuhi! Heri kwako, nchi, mfalme wako akiwa mtoto wa watu, Na wakuu wako hula wakati ufaao, Ili makusudi wapate nguvu, wala si kwa ajili ya ulevi. Kwa sababu ya uvivu paa hunepa; Na kwa utepetevu wa mikono nyumba huvuja. Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko, Na divai huyafurahisha maisha; Na fedha huleta jawabu la mambo yote. Usimlaani mfalme, la, hata katika wazo lako; Wala usiwalaani wakwasi chumbani mwako; Kwa kuwa ndege wa anga ataichukua sauti, Na mwenye mabawa ataitoa habari.
Mhubiri 10:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kama vile inzi waliokufa huacha harufu mbaya kwenye manukato, ndivyo upumbavu kidogo huzidi nguvu hekima na heshima. Moyo wa mwenye hekima huelekea kuume, lakini moyo wa mpumbavu huelekea kushoto. Hata anapotembea barabarani, mpumbavu hukosa ufahamu na kudhihirisha kwa kila mmoja jinsi alivyo mpumbavu. Kama hasira ya mtawala ikiwaka dhidi yako, usiache mahali pako, utulivu huweza kuzuia makosa mengi. Kuna ubaya niliouona chini ya jua, aina ya kosa litokalo kwa mtawala: Wapumbavu kuwekwa kwenye nafasi nyingi za utawala, hali matajiri wanashika nafasi za chini. Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, wakati wakuu wakitembea kwa miguu kama watumwa. Yeye achimbaye shimo aweza kutumbukia ndani yake, yeyote abomoaye ukuta anaweza kuumwa na nyoka. Yeyote apasuaye mawe inawezekana yakamuumiza, yeyote apasuaye magogo inawezekana yakamuumiza. Kama shoka ni butu na halikunolewa, nguvu nyingi zinahitajika, lakini ustadi utaleta mafanikio. Nyoka akiuma kabla ya kuchezeshwa, mchezeshaji hatahitajika tena. Maneno yanayotoka kinywani mwa mtu mwenye hekima yana neema, bali mpumbavu huangamizwa na midomo yake mwenyewe. Mwanzoni maneno yake ni upumbavu, mwishoni ni wazimu mbaya, naye mpumbavu huzidisha maneno. Hakuna yeyote ajuaye linalokuja, ni nani awezaye kueleza ni jambo gani litakalotokea baada yake? Kazi ya mpumbavu humchosha mwenyewe, hajui njia iendayo mjini. Ole wako, ee nchi ambayo mfalme wako alikuwa mtumwa na ambayo wakuu wako hufanya karamu asubuhi. Heri wewe, ee nchi ambayo mfalme wako ni wa uzao wenye kuheshimika, na ambayo wakuu wako hula chakula kwa wakati unaofaa: wao hula ili kupata nguvu na si kwa ajili ya ulevi. Kama mtu ni mvivu, paa la nyumba huinama; kutokana na mikono milegevu, nyumba huvuja. Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko, nao mvinyo hufurahisha maisha, lakini fedha ni jawabu la mambo yote. Usimshutumu mfalme hata ikiwa ni katika mawazo yako, au kumlaani tajiri katika chumba chako cha kulala, kwa sababu ndege wa angani wanaweza kuchukua maneno yako, naye ndege anayeruka anaweza kutoa taarifa ya yale uliyosema.