Mhubiri 1:1-11
Mhubiri 1:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Yafuatayo ni maneno ya Mhubiri mwana wa Daudi, aliyekuwa mfalme huko Yerusalemu. Bure kabisa, bure kabisa, nakuambia mimi Mhubiri! Kila kitu ni bure kabisa! Binadamu hufaidi nini kwa jasho lake lote hapa duniani? Kizazi chapita na kingine chaja, lakini dunia yadumu daima. Jua lachomoza na kutua; laharakisha kwenda machweoni. Upepo wavuma kusini, wazunguka hadi kaskazini. Wavuma na kuvuma tena, warudia mzunguko wake daima. Mito yote hutiririkia baharini, lakini bahari kamwe haijai; huko ambako mito hutiririkia ndiko huko inakotoka tena. Mambo yote husababisha uchovu, uchovu mkubwa usioelezeka. Jicho halichoki kuona, wala sikio kusikia. Yaliyokuwako ndio yatakayokuwako, yaliyotendeka ndio yatakayotendeka; duniani hakuna jambo jipya. Watu husema, “Tazama jambo jipya,” kumbe lilikwisha kuwako zama za kale. Hakuna mtu anayekumbuka ya zamani wala atakayekumbuka yatakayotukia baadaye.
Mhubiri 1:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maneno ya Mhubiri mwana wa Daudi, mfalme katika Yerusalemu Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili. Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua? Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima. Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa maawio yake. Upepo huvuma kuelekea kusini, kisha huvuma kuelekea kaskazini; hugeuka daima katika mwendo wake, nao huyarudia mazunguko yake. Mito yote huingia baharini, lakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena. Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia. Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua. Je! Kuna jambo lolote ambalo watu husema juu yake, Tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi. Hakuna kumbukumbu lolote la vizazi vilivyotangulia; wala hakutakuwa na kumbukumbu lolote la vizazi vitakavyokuja, miongoni mwao wale watakaofuata baadaye.
Mhubiri 1:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maneno ya Mhubiri, mwana wa Daudi, mfalme katika Yerusalemu Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili. Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua? Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima. Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa maawio yake. Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake. Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena. Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia. Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua. Je! Kuna jambo lo lote ambalo watu husema juu yake, Tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi. Hakuna kumbukumbu lo lote la vizazi vilivyotangulia; wala hakutakuwa na kumbukumbu lo lote la vizazi vitakavyokuja, miongoni mwao wale watakaofuata baadaye.
Mhubiri 1:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Maneno ya Mhubiri, mwana wa Daudi, mfalme huko Yerusalemu: “Ubatili! Ubatili!” Mhubiri anasema. “Ubatili mtupu! Kila kitu ni ubatili.” Mwanadamu anafaidi nini kutokana na kazi yake yote anayotaabikia chini ya jua? Vizazi huja na vizazi hupita, lakini dunia inadumu milele. Jua huchomoza na jua huzama, nalo huharakisha kurudi mawioni. Upepo huvuma kuelekea kusini na kugeukia kaskazini; hurudia mzunguko huo huo, daima ukirudia njia yake. Mito yote hutiririka baharini, hata hivyo bahari kamwe haijai. Mahali mito inapotoka, huko hurudi tena. Vitu vyote vinachosha, kuliko mtu anavyoweza kusema. Jicho kamwe halitosheki kutazama, wala sikio halishibi kusikia. Kile kilichokuwepo kitakuwepo tena, kile kilichofanyika kitafanyika tena, hakuna kilicho kipya chini ya jua. Kuna kitu chochote ambacho mtu anaweza kusema, “Tazama! Kitu hiki ni kipya”? Kilikuwepo tangu zamani za kale, kilikuwepo kabla ya wakati wetu. Hakuna kumbukumbu ya watu wa zamani, hata na wale ambao hawajaja bado hawatakumbukwa na wale watakaofuata baadaye.